in

Waliombeba Injinia Hersi watakuja kumshusha!

HERSI

Inawezekana kwa kiasi kikubwa mpaka sasa hivi mashabiki wa Yanga wanatamani sana kumuona Yusuph Manji akirejea kwenye klabu ya Yanga. Huyu ndiye mtu ambaye aliwapa furaha enzi za utawala wake pale Jangwani.

Huyu ndiye mtu pekee ambaye alifanya kila linalowezekana ili kuunda timu imara ya Yanga. Timu ambayo ilishinda makombe matatu mfululizo ya ligi kuu Tanzania bara. Timu ambayo ilifanya vyema kwenye michuano ya kimataifa ya vilabu ya CAT.

Ndiyo timu ambayo ilifika hatua ya mahindi ya kombe la shirikisho barani Afrika. Vyote hivi viliwezekana kwa sababu ndani ya Yanga kulikuwepo na wachezaji bora ambao walitengeneza timu imara ya Yanga.

Wachezaji ambao kwa sasa wanaonekana hawapo tena kwenye timu ya Yanga kitu ambacho kimesababisha klabu ya Simba kuwa mtawala mkuu wa ligi kuu. Kwa misimu mitatu mfululizo Simba imekuwa bingwa wa ligi kuu Tanzania bara bila upinzani mkubwa.

Ubovu wa Yanga umewafanya mashabiki wa Yanga kuwa tamaa ya kuiona timu yao siku moja ikiwa na kikosi imara kama kikosi ambacho Yusuph Manji alikitengeneza kutoka kwenye koti lake la pesa.

Wanatamani kuiona Yanga iliyokuwa na uwezo wa kushindana kwenye michuano ya kimataifa ya CAF kama kipindi kile ambacho Yusuph Manji aliwezesha kuifanya Yanga itoe upinzani mkali mpaka kwa timu kubwa Afrika kama Al Ahly tena Misri.

Wamekuwa na tamaa ya kuiona Yanga ikishinda makombe matatu mfululizo ya ligi kuu Tanzania bara. Wamechoka kuwa wanyonge mbele ya Simba. Wamechoka kuona Simba ikiwa na ubabe ndani na nje ya uwanja. Wanatamani kuurudisha ubabe wao mbele ya Simba.

Ndiyo maana kila anayekuja ndani ya Yanga kwa ahadi ya kuwapa kitu bora ndani ya timu kwa wao huyo mtu huonekana kama mfalme haswa. Sikushangaa jana walivyombeba Injia Hersi kwa sababu walimuona ni Mfalme wao.

Sikuona kabisa ajabu kwa sababu muda huu wana njaa . Wanatamani kula chakula washibe. Kila wanapomuona mtu mwenye chakula huwa wanamwabudu kwa kiasi kikubwa.

Kuna kitu kimoja ambacho Injinia Hersi anatakiwa kukifahamu. Wale mashabiki ambao jana walimbeba, walimbeba wakiwa na maana moja tu. Mashabiki wale walikuwa wanamwambia Injinia Hersi kuwa Yanga inatakiwa kuwa juu kama yeye alivyokuwa juu baada ya kubebwa jana.  

Yeye ndiye anayetakiwa kwa sasa kuibeba Yanga vyema. Kitu pekee ambacho kitaondoa ile furaha ya jana ya mashabiki kwa Injinia Hersi ni yeye kushindwa kuifanya Yanga kuwa juu hapo ndipo utakuwa muda sahihi kwa mashabiki kumshusha chini Injinia Hersi.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Wachezaji wetu

Nini chanzo wachezaji wetu kurudi kutoka Ulaya?

Mohamed Dewji

Dewji Hakujibu swali la Uwekezaji