in , , ,

Ni nani huyu Rais mpya wa soka Kenya?

WAKATI kukiwa na wasiwasi kuhusiana na uwezo wa majirani zetu Kenya kuwa tayari kwa mashindano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), Shirikisho la soka nchini humo limepata sura mpya ya uongozi kwa kipindi kingine kijacho. Itakumbukwa kuwa Kenya ni mwenyeji mwenza wa AFCON mwaka 2027 akishirikiana na Tanzania na Uganda, hivyo kabla ya fainali hizo kutakuwa na zile zinazohusisha wachezaji wa ndani yaani CHAN mwaka 2025. 

Kenya ina kibarua kigumu kuthibitisha inakidhi vigezo vya kuwa na viwanja bora kwa kanuni za CAF na ambavyo vitatumika kwenye mashindano hayo. Viwanja viwili vinavyotarajiwa ni Moi Kasarani na Nyayo Stadium bado vipo katika matengenezo lakini imeibuka hali ya wasiwasi kama vitakuwa tayari kabla ya Desemba 31,2024. Wadau wa michezo nchini Kenya hivi karibuni wameshuhudia uchaguzi mkuu wa viongozi wa kuingia Shirikisho la Soka nchini humo, FKF. 

TANZANIASPORTS inaangazia mshindi wa nafasi ya urais wa shirikisho hilo kuwa ni nani katika sekta ya michezo nchini humo na kubainisha jinsi nyota wa Ligi ya Mabingwa Ulaya alivyochagiza ushindi wake na kuibua matumaini mapya kwa mashabiki wa soka nchini Kenya.

Ushindi mgumu

Rais mpya wa Shirikisho la soka Kenya ni Hussein Mohammed ambaye aliwapiga mweleka washindani wake wa karibu Nick Mwendwa, Barry Otieno na Doris Petra. Ushindi wa rais huyo ulikuja katika raundu ya pili baada ya kushindikana katika awamu ya kwanza. Hussein Mohammed alishinda katika duru la pili ya upigaji wa kura na kuhitimisha rasmi utawala wa miaka nane wa Nick Mwendwa.Β 

Matokeo yaliyotangazwa katika ukumbi wa ndani wa wa uwanja wa Moi Kasarani Hussein Mohammed alichaguliwa kuwa Rais mpya  wa Shirikisho la Soka la Kenya baada ya kupata kura 67 katika duru la pili la upigaji kura. Uchaguzi huo uliingia katika duru la pili ili kumwezesha mshindi kupata asilimia 50 ya kura zote 90 za wajumbe. Katika duru la kwanza Hussein Mohammed alipata kura 42 ikilinganishwa na 31 za Doris Petra,Cleophas Shimanyula alipata kura 4 na 10 za Barry Otieno. Kwa ushindi huo ndiye atakuwa bosi wa makao makuu ya soka yaliyopo Goal Project. Siku chache baada ya kuchaguliwa kuongoza shirikisho la soka nchini humo Husserin Mohammed alitembelea ofisi za FKF

Je Hussein Mohammed ni nani?

Rais huyo mpya wa FKF ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni la Extreme Sports Limited  na ana umri wa miaka 47. Kampuni yake inajushughulisha na masuala ya matamasha ya michezo kwa vijana. Kama ya ushindi huo Hussein Mohammed alikuwa naibu mwenyekiti wa klabu ya Murang’a Seal F.C inayoshiriki Ligi Kuu Kenya (KPL). Pia amewahi kufanya kazi katika kampuni la simu la Safaricom akiwa mkurugenzi wa uendeshaji,mwenyekiti wa Youth Agenda ambayo ni asasi ya kiraia, na mwenyekiti wa Kamati ya fedha ya Harambee Stars mwaka 2010. 

Hii ilikuwa ni mara ya pili kwa Hussein Mohammed kuwania nafasi hiyo baada ya kuangushwa na Sam Nywameya katika uchaguzi wa mwaka 2011 wakati huo akiwa na umri miaka 34 pekee. Kabla ya kushinda nafasi hiyo alilazimika kwenda mahakamani kupinga kuenguliwa kwake, ndipo mahakama ikampa ushindi wa kugombea urais wa FKF.

Kibarua kigumu kinachomsubiri

Kati ya majukumu makubwa ambayo rais Mpya atakabiliana nayo ni kuhakikisha anainua kiwango cha soka la Kenya. Wakati wa kampeni Hussein Mohammed alisema anao mpango kabambe wa kuhakikisha shirikisho la soka linawafanyia mambo makubwa wadau wa soka na kulifikisha katika ngazi za juu zaidi kuliko kipindi cha mtangulizi wake. 

Kwanza anatakiwa kuhakikisha Kenya haipokonywi uenyeji wa fainali za CHAN kwani matumaini ya wengi ni kuona FKF na serikali zinasaidiana kuhakikisha wanakamilisha matakwa ya CAF kabla ya tarehe 31 mwezi huu. Kumekuwa na uvumi kuwa huenda Kenya ikapoteza nafasi yake na kwenda Rwanda kutokana na kasi ndogo ya maandalizi ikiwemo viwanja viwili muhimu. Lakini rais mpya ana matumaini kushawishi CAF kuendelea kuiamini Kenya katika uenyeji huo. Ili kusisitiza kuwa wana shauku ya kukamilisha matakwa ya CAF, waziri wa michezo Kipchumba Murkomen na rais wa FKF  wiki hii walitarajiwa kuzindua Kamati ya maandalizi. FKF pia wanatakiwa kuandaa timu ya Taifa Harambee Stars kwa ajili ya mashindano hayo ili iwe yenye ushindani kwenye CHAN. 

Pili, ikumbukwe Kenya haijafanya vizuri kuanzia ngazi ya vilabu hadi timu za Taifa kiasi cha mashabiki kususia kwenda viwanja vya soka. Jambo lingine ni ubora wa Ligi Kuu. Kwa muda mrefu Ligi ya Kenya imekuwa katika hali mbaya na vilabu vyake havipigi hatua kwenye mashindano ya CAF. 

Kutokana na kudorora kwa timu zake kumefanya ukanda wa Afrika mashariki utegemee mafanikio ya timu za Tanzania. Kwa msingi huo rais mpya anatakiwa kuhakikisha Ligi ya Kenya inaimarika na kuvutia wawekezaji wapya wenyeji na wageni ili kuinua kiwnago cha soka. Mbaya zaidi hata kwenye takwimu za ubora za FIFA, Kenya imeachwa mbali na Tanzania. Kimsingi ubora wa Ligi unatafsiri moja kwa moja jinsi timu ya Taifa inavyofanikiwa kwenye mashindano ya AFCON. Changamoto nyingine kubwa ni upangaji wa matokeo jambo ambalo linadhoofisha Ligi ya Kenya. Kumekuwa na matatizo hayo ambayo uongozi uliopita haukuchukua hatua kubwa kukabiliana nalo.

Abebwa na nyota wa Inter Milan

Katika kinyang’anyiro hicho Hussein Mohammed alikuwa sambamba na mgombea mwenza na nyota wa zamani wa Kenya, McDonald Mariga. Nyota huyo wa zamani wa Kenya, alikuwa mchezaji wa klabu ya Inter Milan ilipokuwa inanolewa na kocha Jose Mourinho. Inter Milan ni miongoni mwa vilabu imara kwenye Ligi Kuu ya Italia maarufu kama Seire A. Mariga akiwa mchezaji wa kiungo mkabaji aliandika rekodi ya aina yake kuwa wa kwanza toka kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Umaarufu wa nyota huyo na uzeofu wake tokana na kucheza Italia, England na kwingineko Ulaya unatarajiwa kuwafungulia milango wachezaji na wadau wa Kenya kuvuna maarifa aliyonayo na hivyo kuipaisha soka la Kenya.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Mambo muhimu kuimarisha Ligi Kuu Tanzania

Tanzania Sports

Adhabu ya Refa imewapa ushindi Simba