in

Nani kuibuka kinara wa mabao Yanga?

Dar young africans

DAVID Molinga ndiye mshambuliaji wa mwisho wa Yanga kupachika mabao 15 kwa msimu mmoja. Huyu ndiye ameacha alama ya upachikaji mabao ambayo hadi sasa washambuliaji watatu wa Yanga Yacouba Sogne,Michael Sarpong na Ditram Nchimbi wameshindwa kufikia. Ni Yacouba pekee amemaliza msimu akiwa na mabao nane.

Na sasa aliyekuwa mshambuliaji wa Horoya ya Guinea, Heritier Makambo amerejea katika timu yake ya zamani, Yanga ambapo amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo ya mitaa ya Jangwani na Twiga jijini Dar es salaam. Makambo ni kati ya washambuliaji ambao wamewahi kung’ara katika kikosi cha Yanga miaka nyuma kabla ya kuuzwa. Nyota huyo ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)

Kurejea kwake kunaibua swali moja tu ikiwa nyota huyo ataonesha makali kama ilivyokuwa awamu ya kwanza ya uchezaji wake katika timu ya Yanga. Makambo anarejea Yanga ambayo ilikuwa inakabiliwa na ukame wa mabao msimu uliopita.

Mfungaji anayeongoza kikosini ni mshambuliaji Yacouba Sogne ambaye alimaliza msimu akiwa na mabao 8. Washambuliaji wengine kikosini Ditram Nchimbi na Michael Sarpong hawakufua dafu kabisawala kuibeba timu hiyo hivyo kukosa ubingwa kwa mara nne mfululizo na kuwashuhudia watani wao wa jadi Simba wakiibuka mabingwa.

Wakati Yanga ikikabiliwa na ukame wa mabao, wenzao Simba walikuwa na safu kali ya ushambuliaji ambayo ilifunga mabao 44 msimu uliopita, wakiongozwa na nahodha John Bocco,Chris Mugalu na Meddie Kagere, pamoja na winga Luis Miquissone.

Simba walikuwa na machaguo mazuri katika safu ya ushambuliaji lakini kwa upande wao Yanga hawakuwa na uwezo wa kupachika mabao ya kutosha.

Siri ya ushindi wa Simba katika Ligi Kuu Tanzania Bara imejikita katika idadi kubwa ya mabao ya kufunga. Simba wamechukua ubigwa mara nne mfululizo kwa sababu ya kufunga mabao mengi.

Msimu miwili mfululizo walitoa mfungaji bora, Meddie Kagere, ambaye alipachika mabao 23 (katika msimu wa 2018/2019) na mengine 22 (katika msimu wa 2019/2020). Msimu wa 2020/2021 mfungaji bora ni John Bocco mwenye mabao 15.

Hivyo utaona Simba wamekuwa na safu kali ya ushambuliaji kuliko Yanga. Kwahiyo kwa misimu minne mfululizo safu ya ushambuliaji ya Yanga imeshindwa kufurukuta katika Ligi Kuu.

Mshambuliaji wa mwisho kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu kutoka Yanga alikuwa David Molinga aliyepachika wavuni mabao 15 katika msimu wa 2019/2020. Heritier Makambo katika msimu 2017/2018 alipachika wavuni mabao 17.

Ukiacha Makambo na Molinga, washambuliaji kadhaa wamepita Yanga, lakini hakuna aliyefikisha idadi ya mabao ya Makambo. Kwahiyo uamuzi wa Yanga kumrudisha nyota wa wazamani ni pamoja na kukumbuka mchango wake, huku akiwa amepoteza nafasi katika kikosi cha Horoya.

Sasa swali moja linaloulizwa kwa sasa na wadau wa kandanda nchini Tanzania ni namna gani Makambo anaweza kukomesha ufalme wa washambuliaji wa Simba?

Kama wapishi wa mabao kwa Yanga wapo Yacouba Sogne, Deus Kaseke, Feisal Salum,Farid Mussa na wengine lakini je watamudu kuipaisha safiu ya ushambuliaji iliyodorora kwa misimu minne? Bila shaka majibu ya maswali hayo yatapatikana ifikapo mwezi Mei mwaka 2022 wakati Ligi Kuu ikielekea ukingoni.

Aidha, uamuzi wa Yanga kumrudia Makambo unaonesha bayana kukosa mshambuliaji sahihi mwenye ubora wa kuitumikia Yanga nchini. Vilevile swali jingine la kujiuliza, je tatizo la kufeli limetokana na mifumo ya makocha waliopewa jukumu la kuinoa timu hiyo kwa nyakati tofauti walikosa mbinu za kuwatumia washambuliaji waliokuwa nao?

Hadi sasa tunaweza kusema Yanga wanajaribu kucheza kamari kwa Makambo kwa sababu hawana uhakika kama ataweza kuonesha cheche kama msimu wa 2017-2018 alipoibuka kuwa mfungaji bora.

Msimu ujao pia Yanga watakuwa na kibarua kigumu cha kushiriki mashindano ya kimataifa katika nafasi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hivyo basi kw anamna yoyote ile wanahitajika kuwa na kikosi cheny uchu wa ushindi, huku washambuliaji wao wakiwa na uwezo mkubwa ikiwa wanataka kufika mbali.

Ifahamike Tanzania itawakilishwa na timu nne katika mashindano ya CAF mwaka huu; Simba,Yanga, Azam na Biashara United zitawakilisha katika mashindano mawili; Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Azam FC na Biashara United ndizo zitawakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho. Kwa upande mwingine ushindani uliopo katika timu za Ligi Kuu Tanzania ni sababu nyingine inayoibiua swali ikiwa Heritier Makambo atamudu kurejesha ufalme wake wa kupchika mabao.

Timu nyingi zimekuwa na ushindani mkubwa kuweza kuhimili kasi,ubora na uwezo wa kusakata kabumbu katika Ligi Kuu. Vipaji vinavyoibuka katika maeneo ya mabeki,makipa,viungo na washambuliaji ni sababu nyingine inayoweza kumnyima ufalme Makambo.

Wachezaji wa viwango vya juu kutoka nje ya nchi wamekuwa wakimiminika kusajiliwa katika timu mbalimbali za Ligi Kuu, hiyo ina maana wanaleta mbinu na ubora wa zaidi tofauti na misimu minne iliyopita.

Awali nimesema kurejea kwa Makambo ni kama kamari, inanikumbusha ujio wa aliyewahi kuwa kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo ambaye aliporejea nchini aliajiriwa kuwa kocha wa Yanga.

Ujio wa Maximo uliongozwa na fikra za miaka ya nyuma aliyoinoa Taifa Stars hivyo akamleta mshambuliaji wake Jaja kucheza staili ya Gaudence Mwaikimba yaani mshambuliaji mmoja mbele, huku timu ikicheza soka la kujihami zaidi.

Hata hivyo mbinu hiyo ilikuja wakatisoka la Tanzania lilikuwa limebadilika kwa kiasi kikubwa hivyo kumlazimu Maximo kufikiri mpya ili kurekebisha makosa ya kudhani kuja na Jaja angetibu ukame wa mabao Yanga.

Na sasa Makambo anajiunga na Yanga yenye washambuliaji ambao wameshindwa kufikisha hata mabao 10 kwa msimu. Kinara wao Yacouba Sogne naye haonekani kama atakuwa mkali zaidi lakini angalau yeye kuliko wengine kama Nchimbi na Sarpong.

Hata hivyo haijulikani ni mfumo upi utakaotumiwa na kocha Nasredinne Nabi katika kikosi chake na kuwafanya washambuliaji wake kupachika mabao ya kutosha msimu ujao.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Mbappe

Kama si pesa basi Mbappe atatafuta mataji

Lionel Messi

Messi anaondoka, lakini anakwenda wapi?