*Aahidi ‘kuwachinja’ usajili ujao
Panga la Kocha Jose Mourinho linaelekezwa kwa wachezaji Fernando Torres, Samuel Eto’o na David Luiz anayesisitiza hana wachezaji na atatumia fedha za mauzo yao kununua wenye hadhi ya kukaa Chelsea.
Ni majuzi tu Mourinho alimkejeli Eto’o akisema anadhani umri wake ni miaka 35 na sio 32, akisema kimsingi hana mshambuliaji wa kufaa, na sasa amesema atafanya ‘uchinjaji’ wa uhakika majira ya usajili yakifika baada ya kumalizika ligi kuu mwezi ujao.
Mourinho amefikia hatua ya kufikiria kumtoa kwa mkopo Torres (30) Â ikiwa hatapata mnunuzi wa mchezaji huyo wa Hispania aliyesajiliwa kwa kuweka rekodi ya pauni milioni 50 enzi hizo akitokea Liverpool 2007 alikojiunga 2001 akitoka nyumbani kwao, Atletico Madrid.
Kuna habari kwamba Atletico wanataka kumrejesha kundini na  Inter Milan wangependa kumsajili mchezaji huyo, lakini hakuna hata moja kati ya klabu hizo zilizo tayari kumlipa mshahara wa pauni 175,000 kwa wiki anaopata sasa wala kutoa dau la pauni milioni 20 kwa Chelsea kwa ajili ya usajili wake.
Mourinho amechukizwa na matokeo ya wikiendi ya timu yake kufungwa 1-0 na vibonde Crystal Palace, huku washambuliaji wake wakishindwa kabisa kuzifumania nyavu na sasa anasema magarasa yote atayaweka kwenye gari na kwenda kuyapiga mnada ng’ambo.
Chelsea imeweka kipaumbele chake kwa mshambuliaji wa Atletico, Diego Costa na dili linaandaliwa ili pamoja na fedha watakazotoa kwa klabu hiyo ya Madrid, Torres naye achanganywe humo. Costa ana kipengele kinachomruhusu kuhama ikiwa klabu itafikia dau la pauni milioni 32.
Eto’o pia anatarajiwa kuuzwa au kutolewa kwa mkopo, lakini kwa sasa Mourinho anatarajia kwamba Mcameroon huyo atakuwa amepona ili acheze nafasi ya Torres kwenye mechi dhidi ya Paris Saint Germain usiku wa Jumatano hii.
Luiz (26) kwa upande wake alicheza hovyo Jumamosi kiasi cha kuondoshwa uwanjani baada ya nusu ya kwanza na amewekwa kwenye fungu la kuuzwa ili kumpatia Mourinho pauni milioni 32 za kununua kifaa cha maana. Mourinho anapenda zaidi kuwatumia Ramires na Nemanja Matic kwenye kiungo hivyo atawaacha Frank Lampard na Luiz wakisugua benchi Jumatano hii.
Luiz hata hivyo anaweza kuwa na wakati mzuri msimu ujao kwa sababu Barcelona na Bayern Munich wamekuwa wakimtaka tangu msimu uliopita, ambapo inadhaniwa kwa mfumo wao wa uchezaji atawafaa, tofauti na ilivyo Stamford Bridge. Raia huyo wa Brazil aliyesajiliwa Januari 2011 hajapata nafasi ya kudumu tangu Mourinho amerudi klabuni hapo mwaka jana.
Wakati huo huo, Kocha wa Napoli, Rafa Benitez amemponda tena Mourinho, akisema ni mtaalamu kwa kufeli katika soka ya Ulaya, na ametabiri kwamba Chelsea hawatafika mbali kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo Mourinho amesema anaamini mechi dhidi ya PSG itawaamsha vijana wake waliovunjika moyo baada ya kuchapwa na Palace Jumamosi. Mourinho aliingia uwanjani kuwapa moyo baada ya mpira kwisha, akimnyanyua Gary Cahill aliyekuwa akilia na kubaki amekaa kwenye nyasi.
Comments
Loading…