Ndio maswali ni mengi kwanini mchezaji Benard Morrison ameendelea kuganda Yanga SC. Yupo nchini kwa ajili ya matibabu ya goti lakini anatibiwa na daktari wa viungo wa klabu hiyo. Huko alikosajiliwa FAR Rabat hakuna madaktari wazuri wa kumtibu? Mchezaji Benard Morrison aliondoka Yanga SC msimu uliopita na kwenda kuungana na kocha Mohamed Nabi ambaye pia aliwahi kuhudumu kwenye klabu hiyo na wote kukutana nchini Morocco kwenye hiyo klabu ya FAR Rabat. Mapenzi aliyonayo mchezaji huyo pamoja na majeraha yake lakini amekuwa akihudhuria viwanjani na kushuhudia michezo kadhaa ya Yanga ikicheza ikiwemo ule wa Ligi Kuu NBC PL, dhidi ya Dodoma Jiji FC.
KUTUA YANGA SC
Hii ni kumbukumbu fupi kuhusu mchezaji huyu alivyojiunga na Mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Yanga SC kisha baadae kutimkia nchini Morocco. Ujio wa mchezaji huyu ulitokana na kocha Luc Eymael aliyewahi kuifundisha timu hiyo kabla ya kuondoka kwani ndiye aliyeushauri uongozi wa Yanga kumsajili Benard Morrison kwani ndiye aliyekuwa akimfahamu vyema mchezaji huyo. Morrison Kabla ya kujiunga na Yanga, alikuwa ameshaachana na masuala ya mpira na alikuwa kijijini kwao Ghana akijihusisha na masuala ya kilimo. Msimu wake wa mwisho kusakata kabumbu ulikuwa mwaka 2016 kwenye klabu ya Orland Pirates ya Afrika Kusini na baadae aliachana nayo. Ulipofika msimu wa 2020 ikawa bahati tena kwa mchezaji huyo kupata usajili ndipo Yanga ilipomleta nchini na kumtangaza kama mchezaji wao. Alijua kukonga nyoyo za Wana Yanga wengi kwa ile staili yake ya kuupanda mpira na kuwafanya mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kupita mitaani kifua mbele wakiamini wamempata mtu wa kuitetea bendera yao kwani kwa wakati huo Yanga walikuwa ni kama yatima mbele ya watani zao Simba SC ambao walikuwa wakitamba kwa kutwaa makombe huku wachezaji kama Medie Kagere, Clatous Chama wakiifanya Simba SC kuwa mwiba Mkali.
KISANGA CHAKE
Hapa habari inaenda kuwa tofauti baada ya Benard Morrison kuichapa Simba SC bao moja ambalo liliipa Yanga SC ushindi na kuondoka na alama tatu muhimu mchezo wa Ligi Kuu huku goli hilo likipachikwa jina na wadau mbalimbali wa soka kama Mkuki wa Sumu. Ilikuwa dakika ya 44′ ya mchezo huo wa Derby ya Kariakoo mpira uliotokana na adhabu ndogo yaani faulo na kumshinda mlinda lango Aishi Salum Manula na kujaa wavuni. Baada ya mchezo ule hadithi ilibadilika kabisa kwani watani zao Simba, waliingia kwenye rada za kuisaka saini ya Morrison na kufanikiwa kuipata saini ile. Haikuwa rahisi kwani iliwalazimu watu wazima kukesha makao makuu ya mpira wa Miguu Tanzania ‘TFF’ kusubiri hatima ya maamuzi kuona nani alishinda kesi ya kimkataba kati ya Benad Morrison ama Yanga kwani ilimlazimu mchezaji huyo kuwapeleka kwenye kamati ya usajili ya TFF baada ya kuona klabu ya Yanga haikuwa tayari kumwachia huku Benard Morrison akidai kuwa alisaini mkata wa mwaka mmoja kwaiyo alikuwa huru kusaini timu yoyote. Kwahiyo klabu ya Simba SC ikapewa haki ya kumtumia Morrison kama mchezaji wao na rasmi akaanza kuvaa uzi mwekundu na mweupe.
VITUKO VYAKE
Ilikuwa Agosti 8, 2020 Benard Morrison akajiunga rasmi na Wekundu wa Msimbazi Simba SC akitokea Yanga, hapa ilikuwa chungu kwa mashabiki wa Yanga walipoanza kumuona kipenzi chao akiwatumikia wapinzani wao wakubwa, tukio ambalo liliwauma zaidi ni lile la Benard, kuchukua mpira na kuuweka ndani ya Bukta yake Kisha kuanza kutembea kwenye mwendo kama mtu mwenye ugonjwa wa busha, kufanya vile ilikuwa ni kama dhihaka kwa mashabiki wa Yanga ambao walikuwa wakitupa maneno ya utani kwa wana Simba kwa kusema, kikowapi mbona mchezaji mwenye hachezi ni mgonjwa. Maisha yale yale aliyoyaishi Yanga, hakuyaacha aliyahamishia na Simba, kama vile kutoroka kambini usiku na kwenda kusikojulikana, fujo za hapa na pale na ule utukutu wake ukawa kero kubwa kwa CEO wa Madam Barbrah Hassan, kabla ya kuachia ngazi na kutaka timu kuachana naye.
KURUDI TENA YANGA
Katika mshangao wa wengi, klabu ya Yanga SC ikamrudisha tena kundini mchezaji Benard Morrison akitokea Simba SC. Ilikuwa Julai 4, 2022 pale Yanga ilipokubali kumruhusu Mtukufu Morrison kurejea kwenye timu kwani kufanya hivyo kuliweza kuwagawa baadhi ya Wanachama na mashabiki kwani wengine waliamini kutokana na aina ya vituko vyake vile, hakupaswa kusajiliwa tena kwenye timu yao, hakuwa na nafasi tena. Pamoja na kelele zile Viongozi waliweka pamba masikioni na kuendelea na mchezaji huyo. Hata hivyo hakudumu sana klabuni hapo kwani mwishoni mwa msimu wa 2023, Yanga SC ilimpa mkono wa kwa heri mchezaji huyo kwa kutumia neno maarufu la THANK YOU ambalo lilitumika kuachana na baadhi ya wachezaji wao, huku yeye akienda kujiunga na klabu ya FAR Rabat ya nchini Morocco.
Kabla ya kujiunga na Yanga SC. Benard Morrison aliweza kuvitumikia vilabu kadhaa, kama vile, Ashanti Gold, As Vita Club, Orland Pirates, DC Motema Mapembe, Simba SC, FAR Rabat na Yanga SC, yenyewe.
ASANTE MORRISON
Mtukutu Benard Morrison kwa sasa ni mali ya FAR Rabat ya Morocco, amehudumu hapo kwa kipindi kifupi sana kabla ya kupata jeraha la goti. Yupo nchini ndani ya klabu ya Yanga SC kwa kutibu jeraha lake hilo la goti ingawa watu wengi wamejiuliza maswali mengi, kwani klabu ya FAR Rabat haina madaktari wa kumtibu, hata hivyo utakumbuka baadhi ya kauli za mchezaji huyu na mapenzi aliyonayo kwa nchi yenu kwani kuna siku aliwahi kumuomba Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ampatie uraia ili aweze kuitumikia timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’. Taarifa zinadai Morrison bado yupo sana nchini mpaka pale atakapopata unafuu wa jeraha lake hilo la goti.
Comments
Loading…