in , , ,

Mjadala wa Liverpool kuacha vigogo nje

Rodgers kakosea kuacha vigogo Liverpool?

*wachambuzi mbali mbali waongea*

Wachambuzi wa soka wameanza kujadili uamuzi wa Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers wa kuacha vigogo wa kikosi cha kwanza katika mechi kubwa dhidi ya Real Madrid, ambapo Reds waliishia kwa kufungwa 1-0.

Nahodha Steven Gerard naye alijikuta akiwa benchi pamoja na wenzake, baada ya kucheza hovyo walipokabiliana na Newcastle kwenye mechi iliyotangulia. Wengine walioachwa nje ni mshambuliaji wa kati, Mario Balotelli, Raheem Sterling, Jordan Henderson na Philippe Coutinho.

Mchambuzi wa soka wakati wa mechi, Garry Lineker baada ya kuona orodha ya wachezaji wa Liverpool, alidai kwamba ni sawa na Rodgers kukubali kushindwa hivyo kuanzisha timu dhaifu kama kukata tamaa.

Hata hivyo, Rodgers amejibu akisema hakuona kwamba mechi hiyo dhidi ya mabingwa wa Ulaya ilikuwa kubwa kiasi cha kuwaanzisha hao wanaosemwa kuwa ni majina makubwa, na wala haikuwa kujaribisha kamari, bali ni mpango wake tu.

“Kuchagua timu dhaifu katika mashindano makubwa ya Ulaya, hasa dhidi ya Real Madrid, ni jambo lisilo sahihi kwa klabu ya hadhi ya Liverpool. Ningekuwa mmoja wa nyota wa Liverpool walioachwa pale Bernabeu ningejihisi vibaya kuachwa dhidi ya mabingwa wa Ulaya,” akasema Lineker.

Kocha Rodgers alimjibu hivi: “Nadhani uchezaji wao unazungumza zaidi kuliko maneno yetu. Gary (Lineker) ni mtu ninayemheshimu sana na alikuwa mchezaji wa hadhi ya juu lakini hajapata kuwa kocha, kwa hiyo hajapata kiukweli kuelewa inakuwaje wakati wa kuchagua wachezaji.

“Naheshimu mawazo yake lakini nadhani maneno yalijidhihirisha wazi kwa timu ilivyocheza. Ufanisi wao hauendani kabisa na suala la kukata tama. Hadi mwisho wa mchezo wachezaji wangu walicheza vizuri kulandana na umaarufu wa Liverpool.

Hilo lingekuwa jibu langu.”
Ripoti za kabla ya mechi zilisema Rodgers angemwacha nje Gerrard ili awe timamua kabisa kwa ajili ya mechi ya Jumamosi hii, ambapo Chelsea wanakwenda Anfield kukumbana nao kwenye Ligi Kuu. Liverpool wameanza vibaya msimu huu, tofauti kabisa na uliopita.

“Sikupumzisha wachezaji kwa ajili ya Jumamosi. Nilichagua timu niliyodhani ingeweza kunipa ushindi. Wachezaji walikuwa wazuri uwanjani na ilikuwa bahati mbaya kwamba hatukushinda,” Rodgers akamalizika.

Kusikia hivyo, Lineker naye akajibu: “Rodgers kujibu akionesha kwamba wengi wa wachezaji wake waliachwa kwa sababu ya walivyokuwa hovyo walipocheza na Newcastle na si kwamba wamepumzishwa kwa ajili ya Jumamosi (kucheza na Chelsea) kama ni kweli ni sawa kabisa.”

Msimu uliopita Liverpool hawakuwa kwenye mashindano yoyote ya Ulaya, na kutolewa kwao mapema kwenye mashindano mengine ya nyumbani kulimaanisha kwamba waliweza kuchezesha kikosi karibu kile kile kila mechi.
Msimu huu wana mechi nyingi na pia wapo wachezaji wengi wapya wanaotakiwa kuzoeshwa kikosini ili waendane na mfumo wake wa kucheza. Kati ya walioanza Bernabeu ni Kolo Toure ambaye hakuwa amecheza kwenye ligi, kiungo Lucas Leiva anayechezea timu kwa mara ya tano tu.

Kanuni za Shirikisho la Sola Ulaya (Uefa) zinataka klabu kupanga timu imara katika hatua zote za mashindano hayo, lakini chombo kinachosimamia mashindano hayo hakitachukua hatua yoyote dhidi ya Liverpool.

Rodgers aliacha wachezaji saba nje na mchambuzi wa soka kwenye Televisheni ya Hispania ambaye ni mchezaji wa zamani wa Liverpool, Michael Robinson alisema ni ajabu timu ilivyopangwa, akisema kupumzisha wachezaji ni kitu kimoja na kuheshimu mashindano ni kingine.

“Nadhani Rodgers amefanya makosa, maelfu ya washabiki wa Liverpool wamesafiri kuja hadi Bernaneu kutazama mechi na sasa wanashuhudia wachezaji muhimu wakiwa benchi. Rodgers amenyoosha bendera nyeupe ya kuachia ngazi hata kabla mchezo haujaanza,” akasema Robinson.

Henry Winter wa Daily Telegraph anasema kwamba Liverpool waliondoka Madrid wakiwa wameshuka kiwango zaidi lakini watu kama Kolo Toure na Alberto Moreno walicheza vyema. Kwenye mechi ya mwanzo ambayo Liverpool walichezesha nyota wake, walifungwa 3-0.

Mwandishi wa Daily Express, Paul Joyce anasema watu wanaweza kusema ni uamuzi wa hovyo aliochukua Rodgers lakini unaamsha tafakuri kubwa, hasa wakati ambapo mambo hayaendi vyema, kwamba ametuma ujumbe, amefanya maamuzi mengi ambayo ama ataishi nayo au kufa nayo.

Mtangazaji wa Canal Plus & Cuatro, Julio Maldonado anasema: “Ni vigumu kuamini kwamba line-up ya Liverpool haina Gerrard wala Sterling ambao ni wazima. Bila kujali matokeo, nadhani klabu kubw akama Liverpool kwenye mashindano makubwa zaidi hawatakiwi kufanya hivyo.”

Delfin Melero wa Marca, moja ya magazeti maarufu zaidi Hispania anasema: “Siamini hali hii. Ufafanuzi pekee ni kwamba Rodgers ameamua wapoteze mechi hii na kuamua kuacha nyota wake wawe timamua kwa ajili ya mechi dhidi ya Chelsea. Hawakuja wakijiamini kwamba wataambulia chochote hapa Bernabeu. Uchaguzi wa Rodgers unapeleka ujumbe wa wazi.”

Naye Marcos Lopez wa Marca pia anasema, Liverpool wakicheza bila mchezaji yeyote Mwingereza walikosa nguvu na kasi inayotakiwa na kwamba kwa uchaguzi wa timu wameharibu hadhi yao, mechi ikawa kama ya kirafiki wakati wa safari za Amerika za kabla ya msimu.
Je, Rodgers alifanya makosa kuipanga timu kama alivyoamua? Linabaki kuwa swali, lakini wametoka na matokeo mazuri kuliko vigogo waliyompa nyumbani Anfield. Tusubiri tuone nani watacheza Jumamosi dhidi ya Chelsea.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Arsenal wajivuruga UCL

Man City majanga, Chelsea doro