Sekta ya michezo ni eneo lingine la biashara,utalii na chanzo kikubwa cha mapato ya serikali mbaliimbali duniani. Kodi hukusanywa kupitia wachezaji,makocha,haki za televisheni na maeneo mengine.
Michezo ya aina mbalimbali kwenye mashindano huwa chachu ya kuinua hali ya maisha ya wachezaji, walimu,wadau na watalaamu. Kusema hivyo ndiyo maana baadhi ya nchi zimekuwa zikiwekeza kwa kiwango kikubwa.
Mashindano kama Olimpiki, riadha ya Diamond League, IAAF, Ligi za soka, mbio za magari na mengineyo yamekuwa chachu ya kiuchumi kwa nchi tofauti. Hii ndiyo maana baadhi ya serikali zinaingia gharama kuhakikisha zinawezesha upatikanaji wa huduma fulani ama baadhi ya raia kupewa kipaumbele kupiia michezo na kadhalika.
Ndiyo sababu serikali ya awamu ya nne nchini iliamua kulipa mishahara ya makocha wa timu ya taifa, Taifa Stars wakati huo Marcio Maximo. Hata hivyo juhudi za kuboresha sekta ya michezo zimekuwa hafifu na inaelekea haijatiliwa mkazo ili kuleta matokeo chanya.
Tanzania inao wachezaji wengi katika ngazi tofauti wanaocheza michezo mbalimbali kuanzia soka, riadha, floor ball na mingine mingi lakini wanashindwa kuiwakilisha Tanzania kwa vile hakuna ruhusa ya uraia pacha. Kizazi chenye asili ya Tanzania hakijapewa nafasi kurudi na kuimarisha sekta ya michezo.
Kwa mfano, wapo raia wa Tanzania ambao wanaishi nchi za Ulaya, Asia na Amerika, ambao wana watoto wenye vipaji vya michezo mbalimbali. kizazi hicho ambacho kingeweza kutumika kuleta mafanikio kwa nchi yetu kimejikuta kikiwa nje ya mfumo wa sekta ya michezo kutokana nan chi yetu kushindwa kutengeneza utaratibu wa kuwatumia.
Wapo wanasoka ambao wamezaliwa kwa wazazi kutoka Tanzania katika nchi za Ulaya na wamekuwa wakichagua mataifa kuwakilisha mataifa kama vile Denmark, Sweden Finland, Uswisi, Ujerumani, Uingereza kwenye michezo badala ya
Tanzania. kukosekana utaratibu huo ndio sababu inayoleta swali ni kwa namna gani Tanzania inaweza kujifunza kwa jirani zao Burundi?
Utaratibu wa sekta ya michezo nchini Burundi ni kuhakikisha kocha wao wa timu ya taifa anakuwa na rasilimali zote iwenye timu hiyo ili kuleta mafanikio katika kandanda. Kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka Burundi amepewa fursa ya kutekeleza mipango ya soka nchini humo kwa kuzunguka nchi za Ulaya na nje ya Ulaya akitafuta watoto wenye asili ya Burundi waje kusaidia timu ya taifa ya Burundi.
Kocha wa Burundi amefanikiwa kuwashawishi mastaa kama Saido Berahino na Gael Bigirimana ambao wote walikuwa wameshachezea timu za taifa za Uingereza katika ngazi tofauti.
Kocha wa Burundi amefanikiwa pia kumleta Marco Waymans ambaye alikuwa ameshachezea timu ya taifa ya Ubelgiji ya Vijana, naye kama walivyo mastaa wengine akakubali kuichezea timu ya taifa ya Burundi.
Aidha, kocha huyo amezidi kutanua mipango kwa kufanikiwa kumleta Thilo Kehrer anayekipiga katika klabu ya PSG ya Ufaransa kwenda kuchezea timu ya taifa ya Burundi, bahati mbaya kabla ya kuanza utekelezaji wa zoezi hilo serikali ya Ujerumani ikamshawishi kijana huyo achezee nchi yao, naye akageuza mawazo na kuiacha Burundi. Ingawa jaribio la kumpata Thilo halijafanikiwa lakini Burundi wameonesha wazi mikakati yao kwenye michezo na kwamba wanataka kuleta mafanikio ndani ya kipindi cha miaka 10 ijayo.
Hivi karibuni kocha huyo pia amefanikiwa kumleta kijana mwingine Mike Tresor Ndayishimiye ambaye amewahi kuchezea timu ya taifa ya vijana ya Ubelgiji, naye tayari ameshakubali kusaidia Burundi nchi walikotoka wazazi wake.
Shirikisho la soka la Burundi wana mipango ya kuwaita vijana wote wenye vipaji vya soka wenye asili ya nchi hiyo kuchezea timu ya taifa. Vijana wote wanaocheza vilabu vya Ulaya wanatakiwa kuwekwa kambini ili wachague wachezaji wazuri waingizwe kwenye timu ya taifa. Malengo ya Burundi ni kuhakikisha wanacheza fainali za Kombe la dunia mwaka 2026 na wameanza kuandaa vijana.
Unapoona mikakati ya namna hiyo maana yake imebarikiwa na serikali. Kwamba serikali imeamua kwa kauli moja na utashi kuwa ni wakati wa kuwarudisha kizazi chenye asili ya Burundi kuleta manafaniko.
Nikitazama nchi yetu namna tunavyoendesha soka letu, sioni dalili za kuchukua mkondo kama huu kuhakikisha wachezaji wenye vipaji ambao wanataokana na kizazi cha watanzania wanaoishi nje ya nchi. Sioni mipango ya kuwafuatilia ama kuwa na mpango wa kuwachukua vijana wenye vipaji ili waje kutumikia Taifa Stars.
Sioni hayo, lakini taifa dogo la Burundi ambalo tumewazidi mambo mengi kisoka, kiuchumi,ulinzi na kadhalika wanachukua hatua madhubuti na kutekeleza mipango yao. Ni lini serikali ya Tanzania itakuwa na utashi kuhakikisha inaweka utaratibu ambao unawezesha kuwachukua vijana wenye vipaji kuchezea timu zetu za taifa?
Ni lini shirikisho la soka TFF litakuwa na mpango wa kuhakikisha linajikita kuwaibua na kuwachukua wachezaji wenye asili ya Tanzania kuchezea nchi ya wazazi wao ama wao wenyewe?
Comments
Loading…