Manchester United wameshindwa kupata ushindi kwenye mechi yake ya tatu katika Ligi Kuu ya England (EPL), tofauti na utabiri wa kocha Louis van Gaal kwamba wangeanza kushinda Jumamosi hii.
Wakiwachezesha Angel Di Maria, Robin van Persie, Juan Mata na Ashley Young mbele dhidi ya Bunrley waliopanda daraja msimu huu, Mashetani Wekundu wameambulia sare tasa, na hadi sasa wamejikusanyia pointi mbili tu.
Walitoshana nguvu na Sunderland kwenye mechi iliyopita wakati ileya funga dimba katika Uwanja wa Old Trafford walifungwa 2-1 na Swansea, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya Swansea kuwafunga United kwenye EPL.
Burnley waliwabana Man U na nyota wao Di Maria aliyesajiliwa kwa pauni milioni 59.7 na kuvunja rekodi ya Uingereza, na mechi ilikuwa ya kuvutia kwenye dimba la Turf Moor. Van Gaal amesema anahitaji muda zaidi kwa sababu anajenga timu mpya, ila asichojua ni iwapo atapewa muda huo.
Di Maria alicheza kwa dakika 70 kabla ya kubadilishwa na Anderson, lakini pia Van Persie naye alitolewa dakika ya 73 na nafasi yake kuchukuliwa na Danny Wellbeck anayetarajiwa ama kuuzwa au kutolewa kwa mkopo. Juan Mata aliumia na kwenda nje, nafasi yake ikichukuliwa na chipukizi Adnan Januzaj.
Nusura Burnley wawaadhiri United, ambapo mpira wa David Jones uligonga mtambaa wa panya. Hii ni pointi ya kwanza kwa Burnley, kwani katika mechi zake za awali walifungwa na Swansea na Chelsea.
Comments
Loading…