Liverpool wamebadili ghafla uamuzi wao wa awali wa kuwapeleka wafanyakazi wao wasiokuwa wachezaji katika likizo za lazima.
Mabingwa hao watarajiwa walichukua uamuzi huo mwishoni mwa wiki iliyopita, sababu ikiwa ni kuenea kwa virusi vya corona na hivyo mechi kutofanyika kwa muda usiojulikana na kusababisha mapato kupungua.
Hatua yao ya awali ilisababisha manung’uniko kutoka kwa wadau wengi, walioona kwamba wamiliki wa klabu hiyo hawakutumia busara kuufikia, na baada yua tafakari wamebadilisha na kusema hawakuwa wametafakari na kufikia hilo vyema.
Liverpool badala yake sasa wameomba radhi. Walichukua hatua hiyo baada ya kuwa michezo na mikusanyiko imezuiwa na serikali na watu kutakiwa kuwa ndani. Haijulikani lini soka itarejea uwanjani kwa hali ilivyo, ambapo watu wengi wameambukizwa na idadi ya vifo inaongezeka.
Liverpool walikuwa wamefikiria kujitua mzigo wa wafanyakazi wake wasiokuwa wachezaji na kuitegea serikali iwalipe asilimia fulani. Hayo yanakuja wakati klabu zikitaka kuwakata wachezaji asilimia 30 ya mapato yao kwa ajili ya kusaidia kwenye janga hilo la COVID-19.
Uamuzi wa Liverpool unajulikana kwamba umekuwa na athari kwa watu kwenye 200 hivi iliowaajiri. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Liverpool, Peter Moore alikiri kwamba hawakuchakata vyema suala hilo.
“Tulikosea kwenye mchakato. Tulikuja kufanya mawasiliano na wadau mbalimbali katika mchakato uliolenga kufikia mwisho mwema kwa wote wanaohusika,” barua yake ilieleza.
Mtendaji huyo akasema kwamba lengo lao lilikuwa, na badi ni kuhakikisha kwamba wafanyakazi wote wanalindwa kwa kadiri inavyowezekana dhidi ya kupoteza kazi, kukosa mapato katika kipindi hiki kigumu lakini pia kuona kwamba hawaambukizwi maradhi ya COVID-19.
Wamiliki wa Liverpool ni Wamarekani – Fenway Sports Group. Liverpool walikuwa klabu ya tano miongoni mwa zile za Ligi Kuu ya England (EPL) kufikiria kuwaweka kwenye likizo ya lazima wafanyakazi hao
Abautani ya Liverpool inatia shinikizo kwa Newcastle United, Tottenham Hotspur, Bournemouth na Norwich ambao wamefikia uamuzi kama huo wa awali wa Liverpool dhidi ya wafanyakazi ambao si wachezaji.