in , , ,

FIFA yasogeza msimu

FIFA HQ

Hatimaye Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limetangaza kusogeza msimu wa soka wa 2019/2020 kwa muda usiojulikana.

Kadhalika, shirikisho hilo limetangaza kuongeza muda wa mikataba katika dakika ya mwisho kwa kwa wachezaji ambao mikataba yao inamalizika Juni 30 mwaka huu.

Tafsiri ya uamuzi huo ni kwamba kila nchi itaamua lini na kwa vipi watamaliza msimu huu uliozongwa na janga la virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu na tayari maelfu ya watu wamefariki dunia katika nchi mbalimbali.

Hatua inayofuata ni kubadilisha tarehe za usajili, ambapo pia klabu za Ligi Kuu ya England (EPL) zinataka kumalizwa kwa mechi zilizosalia ili kwanza bingwa apatikane kihalali, wa kupanda na kushuka daraja na pia wasipokonywe mamilioni ya pauni kutoka kwenye haki za matangazo ya televisheni.

FIFA watathibitisha uamuzi huo na kutoa mamlaka kwa kila nchi kuamua jinsi ya kumaliza msimu na pia namna ya kuanza msimu mpya wa 2020/2021 ambao kwa kawaida huanza Agosti.

Mpango huo unatarajiwa kuwekwa hadharani ndani ya siku mbili tatu hizi, ambapo itamaanisha ile nadharia ya kubatilisha msimu huu wote kutotumika, kwa sababu hata Bodi ya Ligi Kuu ya England (EPL) itapata hasara kwa sababu itakosa fedha za udhamini.

Msimu huu wa EPL unatakiwa kwenda na mechi zilizobaki zichezwe, vinginevyo klabu zitakazimika kurejesha pauni milioni 762 za matangazo ya televisheni, ikimaanisha kwamba zitatumbukia kwenye madeni makubwa kwa sababu tayari baadhi wamezitumia.

Tarehe kamili za kukamilika kwa msimu huo hazikujadiliwa kwenye kikao baina ya klabu za EPL – watu wa Uingereza kwa sasa wamelazimika kujifungia ndani na hakuna kwenda kwenye kazi zisizo za lazima wala kukusanyika, kwa sababu ya virusi vya corona.

Hata hivyo, mipango ya FIFA, kwa kiasi fulani, imetuliza hali na mataifa yatakuwa na uhuru wa kujiamulia namna ya kusonga mbele kutoka kwenye mkwamo. Uwezekano wa kumaliza msimu ni pamoja na kutangaza mwisho sasa hivi na kuwapa ubingwa wanaoongoza na kuwashusha watatu walio chini; kurefusha msimu hadi janga litakapomalizika au kupima wachezaji na kucheza bila watazamaji.

Katika mkutano huo wa Ijumaa, klabu za EPL zilisema kwamba zinafikiria kuwakata wachezaji wao asilimia 30 ya mapato. Hata hivyo, wachezaji wamehoji hatua hiyo, wakisema wanageuzwa mbuzi wa kafara na hakuna uhakika iwapo fedha hizo zitafanya linalotakiwa.

Klabu nyingi zinapenda mechi ziendelee bila watazamaji na kuoneshwa kwenye seti za televisheni ili mambo yaishe salama na wajipange kuanza msimu mpya kwa wakati bila kuwachosha sana wachezaji.

Hata hivyo, kuna klabu chache zinataka kuona soka ikirejea wakati ambapo watazamaji wataruhusiwa, ikimaanisha baada ya janga la corona kumalizika, serikali kuondoa marufuku ya kukusanyika na wakuu wa afya kuridhia kwamba hakuna hatari tena kiafya.

FIFA wanazingatia kwamba kusambaa kwa virusi vya corona kumekuwa tofauti kutoka nchi moja hadi nyingine, hivyo kila moja inatakiwa kupewa uhuru wa kutazama hali yake na kuamua. Wiki iliyopita, Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) lilieleza dhamira yake ya kutaka kuona ligi za ndani ya nchi, Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) na Ligi ya Europa zikimalizika vyema.

Ama kuhusu dirisha la usajili kwa msimu wa kiangazi hapa England ni kuanzia Juni 10 hadi Septemba mosi mwaka huu, lakini hili sasa inaonekana litabadilika kwa sababu si ajabu msimu ukasonga hadi Julai.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Ubingwa Ulaya sintofahamu

Tanzania Sports

Liverpool wapiga ‘abautani’