in

Ligi yetu inapanda thamani

Yanga Vs Simba

LIGI Kuu Tanzania Bara imeanza mbio za kuteka soko la mauzo ya wachezaji barani Afrika baada ya vipaji mbalimbali kuwavutia makocha wan je katika ligi nyinginezo barani Afrika kama vile Morocco,Algeria,Guinea,Tunisia,Afrika kusini na Misri kwa kuzitaja chache.

Dalili za kunyemelea soko la mauzo ya wachezaji zilianza kukita mizizi mara baada ya michuano ya AFCON iliyopita, ambapo mshambuliaji mahiri wa Uganda maarufu kama The Cranes, Emmanuel Okwi alikuwa kwenye orodha ya wachezaji ambao walitia fora katika upachikaji wa mabao.

TANZANIASPORTS katika tathmini yake inaonesha kitendo cha Okwi kuwa mmoja wa washambuliaji mwiba kilikuwa ni kufungua mlango zaidi ulioegeshwa kwa wachezaji wanaokipiga katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwamba wachambuzi,wadau wa soka,a,makocha,wachezaji na viongozi waliona huenda Ligi ya Tanzania imehifadhi wachezaji wenye vipaji vizuri ambavyo vinaweza si kuwasaidia vigogo wengine wa soka bali hata kuwauza kwa timu zingine kwa fedha nyingi.

Hali kadhalika, katika vikosi vya Kenya,Tanzania na Uganda kulikuwa na baadhi ya nyota wanaocheza Ligi Kuu Tanzania. baada ya michuano ya AFCON ikafuatiwa na CHAN 2020, ambako Tanzania ikiwa chini ya kocha wake Ettiene Ndayiragije ilionesha namna vipaji vilivyopo.

Kwenye AFCON kulikuwa na wachezaji wa Tanzania wanaotumikia klabu za Ligi ya Misri,Uturuki,Morocco na kwingineko. Wachezaji waliokwenda huko hakupelekwa kwa majaribio badala yake waliuzwa moja kwa moja tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Ujio wa mabingwa wa soka Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika nayo umetoa mchango mkubwa katika kuwaendelea nyota mbalimbali. samba iliishia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa baada ya kutolewa na Kaizer Chifes ya Afrika kusini kwa jumla ya mabao 4-3.

Simba ikiwa na nyota wake iliztetemesha timu mbalimbali kama vile Al Ahly ya Misri, El Marreikh ya Sudan, AS Vita ya DRC. Na zaidi Simba ilikuwa ilifanikiwa kuzifunga timu zote zilizocheza kwenye uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Mafanikio hayo yameibeba Ligi ya Tanzania ambapo sasa vigogo wa soka barani Afrika wameanza kugawana wachezaji waliopo katika kikosi cha Simba. Luis Miquissone anatajwa kuuzwa kwa mabingwa soka wa Afrika Al Ahly. Cletous Chama anatajwa kuuzwa kwa vigogo wa soka wa Morocco FAR Rabat, wakati Tuisila Kisinda naye anaelekea kucheza soka nje ya Tanzania.

Hii ina maana Ligi ya Tanzania imeanza kutoa wachezaji wenye vipaji vinavyowindwa kote Afrika. Uthibitisho wa hilo ni kuzagaa kwa nyota wengine waliocheza ligi yetu,  Simon Msuva,Nickson Kibabage,Rashid Chilunda, Himid Mao na Yahya Zaid nao waliuzwa moja kwa moja Uarabuni bila kupewa majaribio.

Hivi karibuni mshambuliaji mwingine Adam Adam alikwenda kujiunga na klabu moja nchini Libya kucheza soka la kulipwa, licha ya kurejea kwa sababu za usalama wa nchi hiyo kuwa mdogo.

Hii inamaanisha Ligi yetu inapiga hatua ya kukua na soko la wachezaji kwenye Ligi yetu linazidi kupanda chati kila siku. Hivyo ni wakati mwafaka sasa timu za Tanzania kuwekeza kwenye vijana kwa sababu sasa wanaweza kuwaza kwenda timu zingine za nje kama Afrika kusini,Algeria,Morocco,Tunisia,Misri na ng’ambo ya bara la Afrika kama Kelvin John Pius aliyekwenda KRC Genk ya Ubelgiji.

Hata hivyo, wakati klabu zikiwauza wachezaji nyota wan je waliopo nchini, ni vema kuwekeza pia kwa wachezaji wetu wazawa. Pia wachezaji wazawa wanatakiwa kutambua kuwa fursa hii ni muhimu kwa maendeleo yao binafsi na klabu zao kwa ujumla.

Njia ya kwanza ya kutumia fursa hizo ni kwa timu zinazoshiriki mashindano ya Kimataifa ya Afrika, kwamba katika vikosi vyao wanao wachezaji wazawa, nao watafutowe soko la kimataifa ili wauzwe badala ya kuuza wachezaji wa kigeni.

Tanzania inawakilishwa na timu nne katika mashindano ya kimataifa ambazo ni Yanga,Simba,Biashara United na Azam. Fursa hiyo ya michuano inakuza vipaji vya wacheaji wetu pamoja na ushirikiano na vilabu vingine.

Fursa hiyo inawasaidia wachezaji kuonekana sehemu mbalimbali, hivyo kuwawezesha wataalamu wa kufuatilia vipaji kutolazimisha mchezaji afanyiwe majaribio wakati ameonwa kwenye michuano akishiriki.

Kizazi cha sasa kinafaidishwa na matumizi ya mitandao ya intaneti kama YouTubu ambako video za wachezaji mbalimbali zinapopatikana inawawia rahisi wataalamu hao kumnunua mchezaji bila kuhangaikia majaribio kama ilivyokuwa zamani.

Mafanikio ya klabu zinazoshiriki mashindano ya CAF msimu ujao angalau kufika hatua ya makundi itawezesha wachezaji na viongozi wao kupata faida zaidi kwenye mchezo huo. Wanaotazama vipaji na kutafuta ni wengi kiasi kwamba wachezaji wanatakiwa kuona wanaposhiriki ni kama bidhaa sokoni ambayo ili inunuliwe lazima ionekane ina ubora na thamani.

Nihitimishe kwa kusema, Ligi yetu inapanda thamani, na itaongezeka zaidi kwa kuzalisha vipaji maridhawa vya soka. Wachezaji na makocha wa kigeni watapenda kutumia Ligi yetu ili kupanua wigo na thamani zao katika mchezo wa soka. tunapowavutia wachezaji wa kigeni,makawala na makocha maana yake tunapandisha thamani lakini lazima viongozi na wachezaji wafahamu kuwa wenye pesa zao watatumbukiza kwetu ili kuvinyakua vipaji vilivyoko. La muhimu ni kujijengea thamani.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Yanga Vs Simba

Kulikoni kila msimu wanaanza upya

Azamfc

Kaeni chonjo, CAF yawataja