in

Kulikoni kila msimu wanaanza upya

Yanga Vs Simba

ORODHA ya wachezaji wanaoingia na kusajiliwa katika timu za soka za Tanzania imeongezeka. Mabingwa wa soka nchini Simba wamesajili. Mshindi wa pili Yanga nao wamesajili. Biashara United inayojiwinda na mashindano ya kimataifa nao wanasajili.

Hali kadhalika mabwanyenye wa Azam Complex, Azam FC nao wanasajili idadi kubwa sio kidogo. Hizo ni timu ambazo zinatarajiwa kuwakilisha mashindano ya kimataifa msimu ujao unaoanz Septemba 25 mwaka huu.

Wastani wa wachezaji wanaosajilia katika klabu za Ligi Kuu Tanzania ni juu ya 5. Kwamba timu zote za Ligi Kuu zinasajilimwachezaji zaidi ya watano kwa msimu mmoja. Baadhi ya timu zinasajili wachezaji zaidi ya 10 kila msimu.

Polisi Tanzania imeachana na wachezaji takribani 10, hapo hapo wanatarajiwa kusajili wachezaji zaidi ya 10. Hii ina maana kwa msimu ujao Polisi Tanzania itakuwa na wachezai wapya kikosini zaidi ya 10.

Yanga wamesajili wachezaji sita wa kigeni; Djigui Diarra (Mali),Khalid Aucho (Uganda),Djuma Shaban (DRC), Yannick Bangala Litombo (DRC), Fiston Mayele (DRC) na Heritier Makambo (DRC). Upo uwezekano Simba wakasajili wachezaji wapya zaidi ya watano katika kikosi chao.

Kimsingi mwenendo wa timu nyingi za Ligi Kuu Tanzania bara umekuwa wa kuanza upya kila msimu. Msimu unapomalizika vituko vya usajili huwa ni vingi sana, kiasi kwamba inaleta maswali mengi.

Ni lini timu zetu zitakuwa na uhakika wa kujenga kikosi imara angalau cha miaka miwili au mitatu? Ni Simba pekee wanaweza kujibu hoja hii kuwa wao kwa miaka minne wamekaa na nyota wao na wametwaa mataji yote ya Ligi Kuu huku wakiwa na maingizio machache kila msimu. Hata hivyo nao wametajwa kuwa na mpango wa kusajili wachezaji wapya 8 kwaajili ya msimu ujao.

Usajili wa wachezaji wengi ni ule ambao unavunja hata uti wa mgongo wa timu. Kwa mfano msimu wa 2019/2020 Yanga iliwatema takribani wachezaji 15 katika kikosi chake ambapo baadhi walikuwa kutoka nje ya nchi.

Kwa maana hiyo ili kuingia msimu mpya wa 2020/2021 Yanga walisajili wachezaji 15 wapya kujaza kikosi chao. Lakini sasa wamesajili wachezaji sita na inawezekana wakafikia 10 kadiri ya taarifa wanavyozidi kutambulisha nyota wao.

Usajili wa wachezaji wengi huenda si tatizo, lakini tatizo linakuja kila msimu timu zinaanza upya. Kuanza upya maana yake ni kusahihisha makosa ya msimu uliomalizika.

Sasa kila msimu timu zinasajili, ina maana usajili huo umekuwa wa ubabaishaji,kubahatisha na kukosa malengo ya nini kinatakiwa kufanywa. Wachezaji wanapoachwa kwa kutoonesha viwnago ni muhimu kuwatathimini changamoto wanazotoa kwa wale wa kikosi cha kwanza.

Kwa mfano mchezaji anatemwa wakati inajulikana licha ya kipaji chake bado hakupata nafasi ya kucheza chini ya kocha ambaye anakuwa na falsafa na mbinu ambazo zinaweza kumweka benchi mchezaji fulani na mwingine akawa chaguo la kwanza.

Lakini mabadiliko ya makocha yanapofanyika unaweza kuona kocha mpya anamchezesha zaidi mchezaji aliyekuwa anadhaniwa kupoteza mwelekeo, wakati yule aliyekuwa anapangwa na kocha mwingine anawekwa benchi.

Kitendawili hiki kinatokana na Kamati za usajili kushindwa kuelewa kwanini wachezaji hupindua na kupinduliwa kwenye kikosi cha kwanza wakiwa na makocha tofauti.

Kila kocha anakuwa na mbinu zake na anatumia wachezaji wanaomfaa kwenye mchezo husika. Unaweza kuona mchezaji mwingine hafai kwa mbinu za kocha fulani lakini akaja mwingine akaona ndiye mchezaji anayweza kucheza kwa mbinu zake.

Katika mazingira hayo benchi la ufundi ndilo linatakiwa kuwasaidia kuendeleza moto wa kutoa changamoto pamoja na kuwaambia viongozi wapunguze kutema idadi kubwa ya wachezaji kwa sababu inabomoa timu zao.

Timu nyingi za Ligi Kuu zinasajili wachezaji 25 hadi 30. Kwa maana hiyo unapoona timu inaachana na wachezaji takribani 10 hadi 15 maana yake makosa ya usajili yaliyofanyika yanaangukia kwa wachezaji ambao wanaonekana kuathiriwa na uamuzi huo hivyo kushusha kabisa viwango vyao.

Kama timu zingekuwa zinasajili kimahesabu na kulinda uti wa mgongo wa timu yao bila shaka zisingekuwa zinaanza upya. Kuanza upya kila msimu maana yake hakuna mipango kwa timu husika wala viongozi hawafikirii jingine zaidi ya mechi inayofuata kisha matokeo yakiwa mabaya wanaanza kulalamika kuwa wachezaji wamehujumu kwa kucheza chini ya kiwango.

Kwa soka la Tanzania inaelekea suala la kuzidiwa mchezo halipo bali kuna kuhujumu timu na kucbheza chini ya kiwango ndiyo sababu inayotumiwa na viongozi wetu kuwaadhibu wachezaji.

Katika mazingira hayo hakuna anayekumbuka namna kamati za usajili vinavyopaswa kuadhibiwa kwa makosa ya usajili mbaya hivyo kuipa timu hasara zaidi. kila msimu mabilioni ya fedha yanatumika kusajili lakini hakuna matunda makubwa yanayopatikana.

Kwa mfano Yanga wameukosa ubingwa kwa misimu minne, lakini katikati ya misimu hiyo hawajengi timu yoyote badala yake wanaanza upya kila msimu.

Kwao kila msimu wanaanza uya, na ukimalizika maana yake hakuna mipango ya miaka angalau mitatu ya kulinda kikosi chao ambacho wanaamini kinaweza kufanya mambo makubwa.

Kwa namna hiyo soka letu na timu zetu zimekuwa zikiburuza mikia na kubaki nyuma hata kama baadhi ya watu watasema Ligi yetu inakua kwa kasi lakini wasisahau inakua bila mipango.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

73 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Premier League 2021-22

EPL ina mechi kali za ufunguzi

Yanga Vs Simba

Ligi yetu inapanda thamani