HAKI ni suala la msingi kwa kila timu inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania. Haki hiyo inahusisha pia mashabiki  wa soka ambao wanatoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali kimapato mbali ya mapato wanayopata kwenye haki za televisheni, wafadhili na wadhamini wao. Timu zote za Ligi Kuu Tanzania zina haki sawa. haki hiyo inawahusu wadau, viongozi wa timu na shirikisho la michezo pamoja na vyama vya soka kote nchini. Tunapozungumzia haki ya kila timu tuna maana kuwa utaratibu wa kisheria na kikanuni unaoendesha Ligi Kuu unapaswa kuheshimiwa. Waendeshaji wa Ligi Kuu wanapaswa kuwaheshimu wadau wa soka. 

Waendeshaji wa Ligi Kuu wanapaswa kuheshimu nafasi ya timu na kanuni zake. Kwa mfano, hivi karibuni limetokea tukio la kuahirishwa mechi ya Ligi Kuu kati ya Yanga na Simba. Mechi hiyo ilipaswa kuchezwa Machi 8 mwaka huu ambapo sababu za kuahirishwa ni malalamiko ya Simba kutoruhusiwa kufanya mazoezi kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa. Simba walikuwa wageni wa Yanga, hivyo walikuwa na haki zote za kupewa uwanja huo kufanya mazoezi siku moja kabla ya mchezo husika kwa mujibu wa kanuni ya 17 (45) ya uendeshaji wa Ligi Kuu. 

Katika kanuni hiyo imebainisha kuwa Simba walipaswa kuwasiliana na timu mwenyeji, uongozi wa uwanja, maofisa wa mchezo husika ili kukamilisha haki yao ya kukabidhiwa uwanja. Hali kadhalika baada ya kukamilisha taarifa kwa timu mwenyeji,msimamizi  wa uwanja na maofisa wa mchezo, Simba wangekuwa na haki zote za kutumia uwanja wa Benjamin Mkapa. Pamoja na mambo mengine uongozi wa uwanja ulipaswa kuwasiliana na timu mwenyeji na maofisa wa mchezo kuhakiki taarifa ya ujio wa Simba. 

Aidha, kumekuwa na malalamiko kuwepo kwa Makomandoo wa klabu ya Yanga ambao walisimama kidete kuzuia Simba kuingia uwanjani hapo kwa ajili ya maandalizi ya kiufundi. Mazonge menngi yaliyotawala sakata lenyewe, hayajengi wala kuimarisha Ligi Kuu Tanzania. Kama nilivyosema mwanzoni, Simba wanayo haki yao, lakini walipaswa kutekeleza taratibu katika haki hizo. Yanga wanayo haki yao, lakini walipaswa kuhakikisha mgeni wao Simba anapata nafasi ya kufanya mazoezi. 

Vilevile uongozi wa uwanja si lazima upigiwe simu pekee au kuandikiwa baruapepe, bali hata wao walipaswa kuwasiliana na wahusika walipo kwenye kanuni (Yanga na Maofisa wa mchezo). Kwa maana hiyo kanuni zilizotungwa kuendesha Ligi Kuu zinapaswa kuzingatiwa kwa kila mdau, kila timu na kila kiongozi. Heshima ya Ligi kuu yetu lazima itunzwe. 

TANZANIASPORTS inafahamu kuwa wapo mashabiki waliotoka Tunduma, mji ambao upo mpakani na Zambia, huku baadhi yao wakiwa raia wa Zambia waliotamani kulitazama pambano hilo kwa macho yao. pia wapo mashabiki kutoka nchini Kenya ambao mara nyingi huwa wanakuja Tanzania katika mechi kama hiyo ya watani. Ni mechi ambayo huwavutia wageni na wenyeji. Wageni kama watalii ambao wanakuwa nchini, wanasafiri kutoka sehemu walizokwenda kutalii hadi Dar Es Salaam kulitazama pambano hili. Kwahiyo pambano la Simba na Yanga ni miongoni mwa vivutio vya utalii ambavyovinapaswa kutunzwa. Wingi wa mashabiki kutoka nje ya nchi, mikoani na baadhi ya wadau barani Afrika wanatazama mechi hiyo kupima gumzo na ufundi wa Ligi Kuu Tanzania. Katika mechi kama hiyo huwa kivutio kwa makocha na viongozi wa vilabu vya nje ambao wanatarajia kujifunza au kuangalia uwezekano wa kuwasajili wachezaji kadhaa kwenye Ligi Kuu. 

Endapo klabu kama Wydad Casablanca Morocco imemsajili Seleman Mwalimu kutoka Fountain Gate (aliyekuwa kwa mkopo kutoka Singida Black Stars) maana yake matarajio yao kuangalia mechi kama Yanga na Simba ni kuchota ufundi wa wachezaji ambao wanaweza kusajiliwa. Lakini pia Yanga na Simba zenyewe zinaonesha thamani na hadhi ya taasisi zao pamoja na kuzitangaza. Kwamba kila klabu ya Ligi Kuu Tanzania inapotaka kuheshimiwa lazima ijiheshimu kwanza. Simba wakitaka heshima na hadhi yao ilindwe ni lazima wajiheshimu kwanza ili wadau wengine wafuate. 

Tanzania Sports
Hizi ndiyo timu mbili maarufu kwenye ligi ya NBC

Yanga nao wakitaka hadhi yao ilindwe na kuheshimiwa ni lazima wenyewe wajiheshimu kwanza na kulinda hadhi na thamani yao. kwa maana hiyo heshima ya klabu ni hatua ya pili baada ya kujiheshimu katika hatua ya kwanza. Kama klabu inataka kujionesha inafanya mambo kienyeji na uswahili swahili mwingi isitarajie heshima yoyote. Klabu hizo mbili zinasajili wachezaji kwa mamilioni ya Dola halafu zinategemea kuendesha mambo kienyeji namna hii kisha kutaka watu waziheshimu. Hakuna heshima inayopatikana kw aklabu ambazo hazijiheshimu zenyewe.

Kwa upande wa Shirikisho la soka, TFF na Bodi ya Ligi Kuu ili ziheshimiwe kama taasisi lazima zijiheshimu zenyewe. Hakuna taasisi au mtu binafsi anayeweza kuipa heshima TFF endapo yenyewe haijiheshimu. Hakuna taasisi au mtu binafsi ambaye anaweza kuipa heshima Bodi ya Ligi endapo yenyewe haijieshimu. Kwahiyo kufutwa kwa mchezo wa Machi 8 kunachafua heshima ya Ligi Kuu, heshima ya soka letu, heshma ya TFF, heshima ya Bodi ya Ligi, heshima ya klabu zote mbili zilizotarajiwa kushiriki mchezo huo.

Wadhamini pia watakuwa wanashangaa namna taasisi za soka zinavyofanya mambo kienyeji. Wadhamini wa Ligi Kuu watakuwa wavumilivu kwa sasa na baadaye lakini upo wakati watalazimika kuachana na udhamini wao ikiwa taasisi zinazohusika na mchezo wa soka hazijiheshimu wala kuheshimu taratibu walizojiwekea. Hali kadhalika watu wa Azam Media watakuwa wameingia gharama kubwa yamuda na fedha lakini hakuna heshima wlaiyopewa. Kwa maana hakuna taasisi ambayo itakubali kuvunjiwa heshima zake kwa sababu za rejareja. Hilo litakuwa na maana kwamba Ligi Kuu inavunjiwa heshima yake.  Tafadhalini TFF, Bodi ya Ligi, Yanga na Simba Ligi Kuu IHESHIMIWE. Ni brand yetu muhimu sana, maana hofu yangu itafika wakati tutakuwa kama mashabiki wa Kenya waliosusia kwenda viwanjani kuangalia timu zao. Tutaanza kuwabembeleza tena kurudi viwanjani kwa gharama kubwa ambayop inatokana na uzembe wa watawala wetu wa Ligi Kuu.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Man United kwenye mstari wa kushuka daraja

Tanzania Sports

Wakaguzi wa viwanja vya Ligi Kuu wazomewe kwa uzembe