CAF wametoka kukifungia kiwanja chetu nchini ambacho kimejenga taswira bora zaidi barani Afrika huku baadhi ya mashabiki wakiibuka na msemo wa ‘machinjio”. Uwanja wa Benjamin Mkapa uliwakarahisha maafisa wa CAF ambao waliwasilisha ripoti kuwa uwanja huo katika eneo la kuchezea limepoteza ubora wake. CAF iliagiza kufanyika marekebisho ya haraka ili kuwa tayari kwa mashindano yay a Kimataifa ya CHAN mwaka huu. Mashindano ya CHAN yanahusisha timu za Taifa za Afrika zinazoundwa na wachezaji wa Ligi za ndani. Kwa upande wa serikali ya Tanzania kupitia msemaji wake Gerson Msigwa alitoa msimamo wa serikali kuwa uwnaja huo utakuwa na ubora wake uleule na kwamba CAF wanakaribishwa tena kwa ukaguzi. Aidha, msemaji wa serikali alibainisha kuwa mchezo wa kwanza wa robo fainali wa mashindano ya Kombe la Shirikisho utafanyika uwanjani hapo. Serikali imejitetea kuwa hakuna tatizo lolote na kwamba wana uhakika wa uwanja wa Benjamin Mkapa kuwa katika mazingira mazuri.
Katika mazingira hayo
TANZANIASPORTS kwa kuzingatia umuhimu wa mashindano ya CHAN ambayo yanaandaliwa kwa ushirikiano wa Kenya, Tanzania na Uganda inasisitiza kuwa suala la viwanja vya soka linatakiw akutiliwa mkazo. Wakati hilo likijitokeza, nalo Shirikisho la Soka nchini TFF limevifungia viwanja mbalimbali kutokana na kutokidhi vigezo vya kikanuni zinazoainisha ubora wa uwanja wa kutumika kwenye Ligi Kuu. Mathalani wikiendi iliyopita tumeshuhudia TFF ikiufungia uwanja wa Ali Hassan Mwinyi uliopo mkoani Tabora kwa madai kuwa umekosa vigezo vya kutumika kwenye Ligi Kuu.
“Uwanja uliofungiwa kutokana na miundombinu yake kutofaa kutumika kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya Kanuni ya Leseni za klabu umekaguliwa na kukidhi vigezo vya kikanuni baada ya marekebisho yaliyoelekezwa kufanyika. TFF inaendelea kuzikumbusha klabu kuendelea kuboresha na kutunza miundombinu ya viwanja vyao vya nyumbani kwa kushirikiana na wamiliki (kwa klabu ambazo hazimiliki viwanja) ili michezo ya Ligi ichezwe kwenye viwanja bora vinavyosaidia kuongeza ushindani na thamani ya Ligi,” inasema sehemu ya taarifa ya TFF kwa umma kuhusu kufungia uwanja wa Ali Hassan Mwinyi iliyotolewa jumapili ya Machi 16, 2025.
Hata hivyo suala la viwanja ni jambo ambalo linazidi kulitia aibu taifa letu. Ligi yetu imeingia kwenye 10 bora barani Afrika, ni muhimu kuhakikisha viwanja vyake vinakuwa kwenye ubora. Ifahamike ubora wa Ligi yetu utavutia watendaji na wataalamu wengine lakini muhimu kuwa na vitendea kazi bora ikiwemo viwanja.
Kwa maana hiyo viwanja hivi vinakaguliwa na Kamati maalumu ya Bodi ya Ligi ambapo pamoja na mambo menbgine inahakikisha vigezo vya kikanuni vinatimizwa na wenyeji. Katika suala la ukaguzi wa viwanja si jambo la kuficha kwa sababu vinakwenda kuonekana kwenye Televisheni ya kiwango cha juu. kwahiyo wahusika wa viwanja, kwa maana ya wamiliki, wanaokodi, na wasimamizi wa Ligi Kuu wanatakiwa kuelewa kuweka muda wa matumizi ya viwanja vyenye mashaka ni jambo muhimu. kwamba wamiliki wanatakiwa kufahamu uwanja wao utakuwa imara kwa miaka mingapi na ukarabati au matengenezo ya kawaida yafanyike muda gani. Hili suala la kufungiwa viwanja linaitia aibu soka letu.
Ni vyema kufahamu kuwa ubaya wa viwnaja unakosesha timu nyingi kufaidi matunda ya usajili wao. Kwa sababu baadhi ya wachezaji wanashindwa kabisa kuonesha umahiri wao kwenye viwanja vibaya na hivyo kusubiri wanapofika uwanja wa Benjamin Mkapa, Azam Complex, KMC Complex au uwanja wa Uhuru ili kuonesha makali yao.
Kufungiwa viwanja pia kunasababisha usumbufu na gharama kubwa kwa klabu kutokana na kulazimika kutumia viwanja vya mbali. Kwa mfano kufungiwa uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kutailazimisha klabu ya Tabora United kutafuta uwanja mwingine wa haraka ili kucheza mechi zake za nyumbani. Kwa ramani ya Tabora, timu hiyo itakuwa na uchaguzi wa viwanja viwili vya haraka, CCM Kirumba au Jamhuri Dodoma.
Wakati uamuzi wa kufungiwa viwanja unafanyika ni muhimu pia kuelewa ni namna gani wakaguzi wanaweza kuchukuliwa hatua kwa sababu wao wanayo dhamana katika hili. Kinyume na hapo Bodi ya Ligi inatakiwa kueleza umma katika ukaguzi wao kwa kushirikiana na TFF wanatumia sifa gani nyingine nje ya kuangalia mazingira ya uwanja? Ifike wakati jukumu hili liwe linafanyika kwa uangalifu mara baada ya Ligi kumalizika na kuwakumbusha wadau juu ya msimu unaofuata. Kufungia pekee hakutosha nadhani inafaa pia klabu kupigwa faini kwa makosa ya kuendelea kutumia uwanja mbovu.
Comments
Loading…