in , , ,

Ligi Kuu England yaanza

Pazia la Ligi Kuu ya England (EPL) linafunguliwa Jumamosi hii, huku timu kadhaa zikiwa zimesuka upya vikosi vyao, na ushindani ukionekana kuwa mkubwa zaidi.

Hata hivyo, kwa wengi, utabiri wa ubingwa ni miongoni mwa timu nne au tano, Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City na labda Manchester United nikizipanga kwa alfabeti wala si kwa yupi ni imara zaidi.
 
LOUIS VAN GAAL ANAKARIBISHWA OLD TRAFFORD
 
Mechi ya kwanza itakuwa baina ya Manchester United na Swansea, ambapo kocha mpya wa Man U, Louis van Gaal anaanza na mechi kadhaa zinazoonekana kuwa rahisi, Mdachi huyo akiwa na kazi ya kufuta uchafu ulioachwa na mtangulizi wake, David Moyes.

hapa Uingereza, mechi za muda huo wa mchana kama watakayoanza nayo United zinaitwa za ‘lunch time’ kwani kwa hapa itakuwa saa 6:45 wakati nyumbani Afrika Mashariki ni kwenye saa 8:45 kipindi hiki cha kiangazi.

Swansea lazima watakuwa na wakati mgumu kwa sababu maelfu ya washabiki wa Man U watalifungua paa la Old Trafford kumkaribisha rasmi kocha wao huyo, Van Gaal, lakini pia shinikizo lipo kwa United, maana wasiposhinda hawataeleweka.

Watapenda warekebishe mambo tangu mapema, kuondokana na hali ya msimu uliopita, ambapo walimaliza katika nafasi ya saba na kukosa nafasi ya kushiriki mashindano yoyote ya kimataifa msimu huu, wakaishia kumfukuza kocha kabla hajamaliza hata mwaka hapo.

Robin van Persie na Wayne Rooney (nahodha) wanatarajiwa kupangwa pamoja mbele ili kuhakikisha wanazifumania nyavu mara nyingi kadiri wawezavyo. Swansea na kocha wao, Gary Monk wanasubiriwa kuona watakuja na mfumo gani dhidi ya United.
 
LEICESTER WANAWAKAMIA EVERTON
 
kuna mechi tano zinazochezwa saa 9:00 ya hapa, ikimaanisha saa 11:00 jioni ya huko nyumbani. Leicester waliojiwekea lengo la kumaliza juu ya timu sita za chini kwenye msimamo wa ligi, wanawakaribisha Everton.

Wamesajili wachezaji kadhaa, akiwamo mpachika mabao wa Argentina, Leonardo Ulloa, lakini pia wanao Jamie Vardy  na David Nugent, na pia wameamua kubaki na wachezaji wao wengi waliosaidia kupanda daraja.

Everton swanaofundishwa na Roberto Martinez wanajivunia kufanikiwa kumsajili moja kwa moja mshambuliaji aliyekuwa Chelsea,  Romelu Lukaku aliyewafungia mabao 15 kati ya 30 ya msimu uliopita.
 
QPR YA REDKNAPP, RIO FERDINAND VS HULL

 
Queen Park Rangers (QPR) waliorejea ligi kuu kwa msimu huu baada ya kushuka ule wa 2012/13 chini ya kocha Harry Redknapp, watakuwa na mkongwe Rio Ferdinand kwenye beki ya kati, wa nachuana na Hull ya kocha Steve Bruce ambao walifika fainali ya Kombe la FA na kufungwa na Arsenal 3-2 msimu uliopita.

QPR pia watakuwa na mwalimu wa kikosi cha kwanza, Glenn Hoddle aliyepata kuwa kocha wa Timu ya Taifa ya England, huku mshambuliaji Loic Remy akisubiri iwapo timu iliyofuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) itamchukua. Uhamisho wake kwenda Liverpool umekwama kwa madai ya vipimo vya afya kuwa na utata.
 
STOKE WAWAKARIBISHA ASTON VILLA
 
Stoke ni wenyeji wa Aston Villa, wenyeji chini ya kocha Mark Hughes wakionekana wazuri baada ya kufanya usajili wa mshambuliaji Bojan Krkic kutoka Barcelona. Villa wanaofundishwa na Paul Lambert na msaidizi wake Roy Keane bado wanajiuliza lini mshambuliaji wao mahiri, Christian Benteke atapona.
 
 
WEST BROM VS SUNDERLAND

West Bromwich Albion wa bosi Alan Irvine wanawakaribisha Sunderland wa Gus Poyet. Albion, au Baggies wanaangalia iwapo beki wao mpya wa kati kutoka Manchester City, Joleon Lescott atakuwa fiti. wamemsajili Mnigeria, Brown Ideye kwa pauni milioni 10 na watatarajia kuvuna kwake kadiri kwa wingi.

Sunderland wanaingia wakiwa na kiungo mpya kutoka City, Jack Rodwell lakini pia wanategemea kwamba dili la kumchukua moja kwa moja Fabio Borini litakamilika, kwani amekuwa akiwafungia mabao muhimu.
 
SPURS NA WA MJINI WENZAO WEST HAM
 
Tottenham Hotspur walio chini ya kocha mpya, Mauricio Pochettino wana safari kutoka kaskazini mwa London kwenda  mashariki mwa jiji kuwakanili West Ham wanaofunzwa na Sam Allardyce ‘Big Sam’ ambaye ameambiwa na mmiliki wa klabu kwamba wanataka kuona soka maridadi zaidi ya msimu uliopita.

Mchezaji wao mahiri, Andy Carroll ameumia tena, na hilo linawafanya kutofaidi mamilioni ya pauni walizomnunua nazo kutoka Liverpool. Spurs wamejiwekea lengo la kumaliza katika nafasi sita za juu kwenye msimamo wa ligi na wanao wachezaji wengi.
 
ARSENAL NA CRYSTAL PALACE

epl

Mechi ya mwisho kwa Jumamosi hii ni baina ya Arsenal na Crystal Palace, Arsene Wenge akiikaribisha timu isiyokuwa na kocha kwenye dimba la Emirates, baada ya Tony Pulis kushindwana na wamiliki wa klabu hiyo ya London.

Mechi hii inachezwa saa 11:30 kwa saa za hapa Uingereza, ambazo ni saa 1:30 kwa saa za nyumbani Afrika Mashariki. Kutokana na ukubwa na ukali wa kikosi chao, hakuna sababu kwa nini Arsenal wasiwe kati ya timu zinazoukimbilia ubingwa msimu huu.

Nyongeza ya wachezaji muhimu na wakubwa kama Alexis Sanchez kutoka Barcelona, kipa David Ospina kutoka Nice, beki wa kati Calum Chambers (19) kutoka Southampton, beki wa kimataifa wa Ufaransa, Mathieu Debuchy kutoka Newcastle na kurejea kwa mshambuliaji Joel Campbell kutoka mkoponi Olympiacos, kunawapa nguvu kubwa Arsenal.

Wakiwapanga vyema Sanchez, Alex Oxlade-Chamberlain na Theo Walcott anayekaribia kupona, huku Olivier Giroud au Yaya Sanogo akiwa namba tisa, wanaweza kupenya ngome yoyote ile, mradi wote wawe fiti kwa kila hali.

Lakini wakikumbuka siku ya kwanza msimu uliopita, ambapo walifungwa 3-1 na Aston Villa, wanaweza kupata ufufutende, japokuwa si kawaida yao wala ya kocha wao. Wachezaji wa Palace watakuwa bado na mbinu walizofunzwa na Pulis, hata kama ameshaondoka, kwa hiyo wanaweza kujaribu kuwazuia Arsenal wasicheke wa kwanza.

Hii ni mechi ambayo kila mahali pameandikwa kuwa ‘wenyeji watashinda’, hivyo shinikizo lipo kwa Arsenal, wasiposhinda kitanuka.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Tony Pulis aondoka Crystal Palace

Manchester United wapigwa nyumbani