in , ,

KUNA SIKU MOJA TU YA MBALAMWEZI, NYOTA NA JUA KUNG’AA KWA PAMOJA

Serengeti boys

Ugumu au uwepesi wa jambo huanzia kwenye akili ya mwanadamu siku zote.
Kupitia hili kuna ukweli mkubwa sana kuwa umasikini au utajiri wa
mwanadamu huanzia katika kufikiria kwake.

Kutenda huja baada ya kufikiria na hapo ndipo tunapokuwa tunafanya
kosa kubwa kipindi tunapoamua kulaumu matendo ya mtu na kuiacha akili
yake ikiwa huru. Mafanikio yapo kichwani na siyo mikononi. Mikono
hutimiza kile ambacho kichwa kimekifikiria na ndiyo maana ni vigumu
kumpata mtu aliyefanikiwa kwa kuanza kutumia mikono kwanza kabla ya
akili.

Akili ndiyo humpeleka mtu sehemu kubwa au ndogo kulingana na yeye
anavyofikiria na ndipo hapa utakapokuja kukubaliana na mimi hakuna
wazo dogo duniani, ukubwa na udogo wa wazo hutegemea na wewe
unavyofikiria.

Ilikuwa na maana kubwa sana kwa Mwenyezi Mungu kuumba jua , nyota na
mbalamwezi na kuzipa muda tofauti wa kuangaza. Haijawahi kutokea hata
siku moja jua, nyota na mbalamwezi kuwaka kwa pamoja ila maandiko
yanatuambia ipo siku zitawaka kwa pamoja ili kutimiza utukufu wa
Mungu.

Mafanikio ni utukufu, na utukufu hutafutwa kila muda, ndiyo maana kuna
wakati ambao Serengeti boys ilipokuwa inapanda ndege kuelekea kambi
nchini Morrocco jicho langu liligeuka kuwaangalia vijana wa timu ya
taifa ya chini ya umri wa miaka 15 waliopo pale Alliance Academy.

Tabasamu lilikuja usoni mwangu baada ya kuzidi kuitazama ndege
iliyowabeba Serengeti boys ikichana mawingu, nafsini mwangu kuna kauli
ilipita ikisema muda wa kujenga utukufu wetu katika soka ndiyo huu.

Hakuna utukufu unaokuja bila maandalizi, na ndipo hapo utakubaliana na
mimi ukitaka kufanikiwa anza kwanza kufanikiwa namna unavyofikiria.

Serengeti boys wanaenda kushiriki michuano ya AFCON ya timu za taifa
zilizochini ya umri wa miaka 17 nchini Gabon. Kama ikifanikiwa kuingia
katika hatua ya nusu fainali basi itakuwa imejitengenezea mazingira
mazuri ya kwenda kushiriki kombe la dunia la vijana waliochini ya umri
wa miaka 17 nchini India .

Hii itakuwa fursa kubwa sana kwa vijana wenyewe kwanza na kwa Taifa kwa ujumla.
Kwa sababu kuanzia Gabon watakuwa na nafasi kubwa ya kujiuza kwa
mawakala wengi ambao watakuwa wamemwagika jukwaani, vivyo hivyo hata
kwenye michuano ya kombe la dunia nchini India.

Fursa hii itawapa nafasi ya vijana kupata timu bora ambazo zitakuwa ni
hakikisho la vipaji vyao kuwa katika mikono salama.

Baada ya Serengeti boys hii itakuwa imebaki timu ya vijana waliochini
ya umri wa miaka 15 ambao wanaandaliwa kwa ajili ya michuano ya Afcon
ya vijana waliochini ya umri wa miaka 17 itakayofanyika hapa nchini,
Tanzania ikiwa mwenyeji.

Kwanza kuwa mwenyeji ni nafasi kubwa sana kwetu sisi kufanya vizuri
kwa sababu siku zote mcheza kwao hutunzwa. Kwa mtaji wa mashabiki na
viwanja vyetu vinatupa hakikishio la sisi kufanya vizuri kwenye
michuano hii.

Vijana hawa walio chini ya umri wa miaka 15 wanapokea matunzo mazuri na
kupata huduma mbalimbali kama elimu, chakula na malazi katika shule ya
Alliance na wanapata nafasi ya kufanya mazoezi kwa pamoja kila jioni
na asubuhi .

Hiki ndicho kitu ambacho nilikuwa nakizungumzia huko juu, maandalizi
ni kitu cha muhimu sana unapotaka kufanya kitu chochote chenye
mafanikio na manufaa kwako. Gharama ya muda au pesa haikwepeki kwenye
mafanikio.

TFF ilitumia muda mwingi na gharama kubwa kuiandaa Serengeti boys na
matunda yake tumeyaona kwa timu yetu kufanikiwa kufuzu michuano ya
Afcon ya vijana.

Kufuzu tu kuna faida kubwa sana kwa sababu vijana watakuwa wanazoea
ile hali ya kushiriki michuano mikubwa wakiwa bado na umri mdogo,
tofauti na siku za nyuma ambapo mchezaji wa Tanzania kuzoea mechi za
kimataifa akiwa timu kubwa ya Taifa, kwa hiyo hawa vijana kwenda
kufikia muda wa kucheza timu ya wakubwa ya Taifa watakuwa wameshazoea
mechi za kimataifa.

Ukichanganya na vijana hawa waliochini ya umri wa miaka 15 kwa sasa,
baada ya michuano ya Afcon ya mwaka 2019 tutakuwa na kikosi imara cha
timu ya vijana ya umri wa miaka 20 na 23 ambacho kitakuwa na vijana
ambao wanajua joto la mashindano makubwa ya kimataifa kwa sababu timu
zote mbili zitakuwa zimeshiriki michuano mikubwa ya kimataifa ya
vijana.

Na hii itatufanya hata kampeni yetu ya kushiriki michuano ya Olympic
kuwa na mafanikio makubwa na mwisho wa siku kuwa na timu ya Taifa
bora, kama ilivyosiku ya mwisho ambapo utukufu wa Jua , nyota na
mbalamwezi kuwaka kwa pamoja na ndipo hapo na sisi utukufu wa soka
letu tutakapoliona.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

NILICHOKIONA KWENYE MECHI ZA UEFA.

Tanzania Sports

TUIPUMZISHE TFF MZIGO , TUINGIE WOTE VITANI