*Ni mamilioni ya dola yaliyotolewa na Hammam
*Maofisa wa Afrika walilamba dola milioni tano
*Makamu wa rais ataka kura ya 2022 irudiwe
Fukuto kubwa linatikisa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kuhusiana na kashfa ya kutolewa mamilioni ya dola kwa wajumbe ili waunge mkono Qatar kuwa mwenyeji wa fainali za soka 2022.
Baada ya wakuu wa Fifa kudhani kashfa hiyo imeisha, takwimu na nyaraka mpya zimepatikana zikitoa ushahidi wa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Fifa na raia wa Qatar, Mohamed Bin Hammam alitoa dola milioni tano kwa maofisa wa Fifa kutoka Afrika.
Qatar wamekuwa wakikanusha kuhusishwa na kashfa za rushwa na kwamba wajumbe walipiga kura kidemokrasia bila shinikizo lolote kutoka kwa ofisa wake.
Vielelezo vipya vinaonesha kwamba Hammam alipiga kampeni waziwazi mwaka mmoja kabla, akiwafuata wajumbe kutoka mabara tofauti ili kuhakikisha Qatar wanapewa nafasi hiyo.
Fifa wamejikuta katika kashfa kwa sababu ilikuwa kana kwamba walifunga macho na masikio kiasi cha kupanga michezo hiyo ifanyike majira ya joto wakati nchini Qatar joto litakuwa la juu sana kiasi kwamba hata mitaani watu hukaa kwa shida.
Hilo ni tatizo kubwa, hasa kwa wachezaji, na kwa namna ya pekee wachezaji wanaotoka nchi zenye baridi kama Ulaya na Amerika, kwani hata sasa wameshakuwa na wasiwasi kutokana na joto linalotarajiwa kuwa katika baadhi ya miji nchini Brazil baadaye mwezi huu.
Bin Hammam (65) anadaiwa pia kutoa pauni 250,000 kugharimia kesi ya mjumbe wa kamati ya utendaji ya Ffa kutoka Oceania, Reynald Temarii ili aweze kupiga kura kwa ajili ya kuichagua Qatar na kuhakikisha Australia hawapati.
Bin Hammam pia anadaiwa kumlipa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Fifa, Jack Warner na familia yake pauni milioni moja muda mfupi tu baada ya Qatar kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa fainali hizo.
Bin Hammam alitoa fedha ili Temarii anayetoka Tahiti agharimie shauri lake la rufaa baada ya Fifa kumzuia kupiga kura kutokana na kunaswa akiwahonga maofisa wa Amerika ili waichague Qatar.
Lengo pia lilikuwa kumzuia naibu wake, David Chung kupiga kura kwenye kikao hicho. Chung anadaiwa kwamba kama angepiga kura angeichagua Australia, hivyo Bin Hammam alifanikiwa kumzuia kwa kumwaga fedha zinazodhaniwa zilitolewa na matajiri wa kampuni za mafuta na mashirika ya ndege nchini Qatar.
Tuhuma hizi zinaonesha uozo wa hali ya juu katika mchakato mzima wa kuwapa Qatar nafasi hiyo na sasa Makamu wa Rais wa Fifa, Jim Boyce anasema anapendekeza mchakato huo urudiwe kwa kupigwa kura upya.
Mpelelezi mkuu wa Fifa, Michael Garcia ameshaanza kuendesha upelelezi juu ya suala hilo na Boyce anasema ikiwa itagundulika ni kweli, hawana budi kurudia kura hiyo.
Comments
Loading…