in , , ,

JORGINHO, SIGARA YA ZIADA YA SARRI

Rafael Benitez hakuwahi kuona miguu yake, macho yake yalimuonesha udongo kwenye dhahabu iliyokuwa inapatikana katika miguu ya Jorginho.

Hakuwahi kuiamini kabisa, kwake yeye alikuwa tayari kumwamini Maria de Montserrat mwanamke wa maisha yake kumiliki dimba la katikati la Napoli.

Hakuwa na hofu kwenye hilo, hakuumizwa na hali ya kumkalisha benchi Jorginho. Aliona mbao ndiyo zinazostahili maisha ya Jorginho kuliko nyasi.

Maisha yaliendelea kwa Rafael Benitez kuendelea kuamini kuwa Jorginho alikuja Napoli kwa ajili ya kutumia makalio yake kwenye mbao kuliko miguu yake kwenye nyasi.

Ilikuwa dhambi kubwa sana, dhambi ambayo mpaka sasa inamuumiza na kumliza Rafael Benitez.

Hakujua kama anatenda dhambi mpaka pale Maurizio Sarri alipokuja kuudhihirishia ulimwengu kuwa muda ndiyo hakimu mzuri.

Hajawahi kutoa hukumu isiyompendeza mtu, hukumu zake huwa za haki na ikizingatia kuwa dunia imetawaliwa na mchezo wa nafasi ndipo hapo muda huchukua nafasi ya kusema ukweli ambao huwa unafichwa kutokana na ufinyu wa nafasi.

Kama ilivyokuwa kwa midomo yake alivyoipa nafasi kubwa ya kuingiza vipisi vya sigara na pua zake kutoa moshi wa sigara ndivyo hivo aliamini katika kutoa nafasi katika miguu ya Jorginho.

Hakutaka kuendelea kushuhudia miguu yake ikiozea kwenye benchi wakati ilikuwa fito imara ya kutengeneza utawala wa soka la Maurizio Sarri.

Utawala ambao mhimili na uti wa mgongo wa mbinu za Maurizio Sarri alikuwa Jorginho.

Huyu ndiye aliyepiga pasi nyingi kuzidi mchezaji yoyote kwenye ligi tano bora ulaya katika msimu uliopita.

Lilikuwa jambo kubwa ambalo lilifanya watu wengi kumwangalia kwa jicho la ndani, hatukutaka kuruhusu jicho letu la nyama kuliruhusu kumtazama Jorginho kwa sababu alitupa sababu zote za kwanini yeye Maurizio Sarri.

Kwa kifupi akili za Maurizio Sarri ziliwekwa kwenye miguu ya Jorginho, akawa anatakiwa kubeba maono ya mfumo wa Maurizio Sarri.

Hakumwangusha, alifanya kila jambo kwa ufasaha na haikuwa ajabu hata ilipotangazwa kuwa Jorginho amevunja rekodi ya Andrea Pirlo ya kupiga pasi nyingi katika mechi moja.

Thamani yake ilikuwa kubwa sana msimu uliopita kama thamani ya mapigo ya moyo wa mwanadamu.

Mapigo ya moyo wa Maurizio Sarri yalikuwa katika miguu ya Jorginho. Miguu yake ilitawanya pasi kila upande wa uwanja.

Akili zake ziliweza kusoma mchezo ndani ya dakika tisini na kuamua ni namna gani timu inatakiwa kucheza kipindi hiki.

Hata alipohitajika kuwalinda mabeki wake wanne alifanya hivo kwa umahiri wenye kuhitaji akili kubwa kuliko nguvu nyingi.

Mwili wake umetawaliwa na akili kubwa ndiyo maana ana maono makubwa ndani ya uwanja anajua ni kipindi gani inatakiwa ishambulie na kujizuia.

Anajua ni sehemu gani sahihi kwake kupitisha mipira wakati timu inaposhambulia, kwa kifupi Jorginho ubongo wake nusu uliumbwa Brazil na nusu yake ikaja kumaliziwa Italy, miguu yake ilitengenezwa na udongo wa kibrazil na moyo wake ukatengenezwa kwa nyama za Kiitaliano.

Hakati tamaa kwenye ufundi wake wa kujenga timu yenye kuvutia inapotazamwa, ndiyo maana Maurizio Sarri alipokuja Chelsea aliamua kuja naye kwa sababu huyu ni sigara yake ya ziada.

Ndiye anayeiamsha anayewakilisha kwa vitendo kila anachofikiria Maurizio Sarri. Leo hii yupo darajani, daraja ambalo Eden Hazard amekuwa mhimili mkubwa kwa muda mrefu.

Timu bora inahitaji wachezaji bora wengi, huwezi kuubeza ubora wa Eden Hazard katika kikosi cha Chelsea lakini ukweli ubaki kuwa uchi kuwa Jorginho ndiye mchezaji muhimu katika falsafa za Maurizio Sarri.

Hatofunga magoli mengi, hatotoa pasi nyingi za magoli lakini ataiamrisha Chelsea icheze kama atakavyo Maurizio Sarri, huyu ndiye mchora ramani wa kwanza wa nyumba iliyopo katika ubongo wa Maurizio Sarri.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Pazia EPL linafunguliwa

Tanzania Sports

UNAI EMERY…