Hapana shaka jana Arsenal walianza na pumzi mpya ndani ya maisha mapya ya bila Arsene Wenger.

Kocha ambaye kadumu kwa miaka ishirini na mbili (22). Miaka mingi sana na alifanikiwa kukaa pale kwa sababu ya alama kubwa aliyoiweka Arsenal kuanzia nje na ndani ya uwanja.

Alijijengea heshima kubwa sana na mpaka anaondoka Arsenal aliondoka akiwa ni mtu mwenye heshima kubwa sana.

Vitabu vya historia vitamtambua Arsene Wenger kama mtu muhimu katika klabu ya Arsenal.

Ndiyo maana hata kuondoka kwake kulikuwa kwa kushtusha, hakuna aliyetegemea. Kila jicho liliongezeka ukubwa kwa mshangao wa habari ile, ngoma za masikio zilihisi zinapokea habari za uongo, kwa mara ya kwanza viungo vya miili yetu vilijua vinajidanganya vyenyewe.

Lakini huo ndiyo ulibaki kuwa ukweli, hakuna kilichobadilika, sikio lilivyosikia ndivyo ukweli ulivyokuwa umebaki kuwa Arsene Wenger alikuwa ameondoka Arsenal rasmi.

Wana Arsenal wakabaki kusubiri kuishi maisha ya bila na Arsene Wenger kitu ambacho wengi wao walikuwa wameshajiandaa nacho kabisa.

Walikuwa wamechoka kuishi maisha chini ya Arsene Wenger, walitaka mtu mpya mwenye mawazo mapya. Bahati hii ilimshukia Unai Emery.

Mshindi wa UEFA EUROPA CUP mara tatu mfululizo akiwa na Sevilla. Kuna watu waliotegemea makubwa na wengine hawakutegemea kubwa lolote kutoka kwa Unai Emery.

Tulitegemea mabadiliko mengi kutoka kwake, ndicho kitu ambacho kilitokea jana.

Arsene Wenger aliwapa uhuru wachezaji wake, hakutaka kuwalazimisha sana wacheze atakavyo, alihakikisha wachezaji wake wako huru uwanjani kucheza mchezo unaowafurahisha.

Hii imekuwa tofauti sana na kwa Unai Emery, Unai Emery amekuwa kocha ambaye anataka wachezaji wake wacheze kulingana na mbinu zake.

Ndilo soka la kisasa, soka lenye mapinduzi mengi ya mbinu, mapinduzi ambayo Unai Emery ameyawekeza katika kikosi cha Arsenal.

Ndiyo maana kwangu mimi halikuwa jambo la kushangaza Mkhitaryan na Ozil wakicheza pembeni ya uwanja na Ramsey akisogezwa kama namba 10.

Tumeshazoea kumuona Ramsey akicheza kama kiungo anayekuja mpaka chini kuchukua mipira na kupanda nayo mpaka mbele (Box to box midfielder).

Kwa Unai Emery kumchezesha kama namba kumi ilikuwa nafasi nzuri kwa timu kuazia kukabia juu, kitu ambacho kilikuwa kigumu kwa sababu muda mwingi Ramsey alionekana yupo katikati ya uwanja na kuwa ngumu kwake kuanzia kukabia juu.

Mkhutaryan na Ozil kucheza pembeni Unai Emery alikuwa anataka kuwafanya Ozil na Mkhitaryan wawe wanatokea pembeni kuingia katikati ya uwanja ili kuwafanya mabeki wa pembeni wa Manchester City (Mendy na Walker) wawe wanawafuata katikati ya uwanja ili kutengeneza uwazi eneo la pembeni ili kuwapa nafasi Bellerin na Mait-Niles kushambulia kwa kutumia uwazi utakaokuwa unatengenezwa pembeni, lakini ikawa tofauti kabisa na mategemeo ya Unai kwani Mendy na Walker walikuwa wanabaki pembeni na kushambulia kwa pembeni hali iliyowafanya kina Mkhitaryan na Ozil wabaki pembeni kukaba hali iliyosababisha Aubameyang kutopata mipira mingi kwa kiasi kikubwa.

Hapa ndipo mbinu za Unai Emery zilianza kuonekana zinapelea mbele ya mbinu za Pep Guardiola. Pep Guariola alimuonesha Unai ana safari ndefu kutoa “U”- Wenger ndani ya kikosi cha Arsenal.

Miaka 22 kwenye kikosi kile kile, ni ngumu kufanikiwa kwa muda mfupi, inahitaji muda kuweza kuweka tamaduni yake anayoiona inafaa kumpa matokeo ndani ya kikosi cha Arsenal.

Muda bado unampa nafasi ya kutengeneza nyumba anayotaka kuishi lakini binadamu hawana uvumilivu na muda, kwao wao hutamani kuona mtoto akitembea wiki moja baada ya kuzaliwa.

Kwao wao kwenye matamanio yao kila kitu kinawezekana, kitu ambacho hakiendani na ƴuhalisia wa maisha, maendeleo huja kwa kuzipanda ngazi na siyo kutegemea lifti huo ndiyo ƴuhalisia wa maisha.

Kwenye mpira hakuna anayeamini kupitia kupanda ngazi kama njia bora ya kufikia mafanikio imara

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

JORGINHO, SIGARA YA ZIADA YA SARRI

Tanzania Sports

NABY KEITA NA UKAMILISHO WA TORATI YA LIVERPOOL