Chelsea wamemteua Guus Hiddink kuwa kocha mkuu wa Chelsea, nafasi
atakayoshika hadi mwisho wa msimu huu.
Taarifa ya Chelsea imesema kwamba mmiliki wa klabu, Roman Abramovich
na Bodi ya Wakurugenzi wanamkaribisha tena kocha mwenye utajiri wa
uzoefu wa soka ya ngazi za juu na mafanikio, ikiwa ni pamoja na
alipofanya nao kazi 2009 na kutwaa Kombe la FA.
“Abramovich na Bodi wanaamini kwamba Guus ana kile kinachotakiwa kwa
ajili ya kuwezesha kikosi chetu chenye vipaji vingi kufanikiwa,”
imesema taarifa hiyo.
Kocha huyo anayechukua nafasi ya Jose Mourinho aliyefukuzwa kazi baada
ya kushindwa mechi tisa kati ya 16 za mwanzo msimu huu, ameeleza
kufurahishwa kurejea Stamford Bridge, lakini lazima ajue ana mzigo
mzito wa kuvusha.
“Nafurahi kurudi Stamford Bridge. Chelsea ni moja ya klabu kubwa zaidi
duniani lakini ipo eneo (la msimamo wa ligi) ambalo haitakiwi kuwa kwa
sasa. Hata hivyo, nina uhakika tunaweza kubadilisha mambo msimu huu.
“Nasubiri kwa hamu kuchapa kazi na wachezaji pamoja na wafanyakazi
wenzangu kwenye klabu hii kubwa, hasa kuhuisha uhusiano wangu na
washabiki wa Chelsea,” akasema Hiddink aliyekuwa kocha wa Timu ya
Taifa ya Uholanzi kabla ya kujiuzulu majuzi.
Hasimamii mechi ya leo nyumbani dhidi ya Sunderland, badala yake ipo
chini ya kocha msaidizi, Steve Holland na Eddie Newton pamoja na
masuala yote ya soka hadi hapo Hiddink atakapoanza kazi rasmi.
Hiddink ndiye alishika hatamu za Chelsea kuanzia Februari 2009,
akapoteza mechi moja tu wakati Chelsea wakijikusanya baada ya kufanya
vibaya hadi nusu msimu kisha wakamaliza katika nafasi ya tatu katika
Ligi Kuu na kuwahakikishia ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Aliondoka vyema pia kwa kuwaachia Kombe la FA walipowafunga Everton
2-1 katika uwanja wa Wembley. Alifanya kazi hiyo sambamba na kuwa
kocha wa Urusi, moja ya nafasi sita alizopata kushika katika soka ya
kimataifa kwenye kipindi chake katika kazi hiyo cha miaka 30 hivi.
Alianzia kazi PSV Eindhoven, klabu aliyochezea pia. Akiwa kocha,
Hiddink alitwaa nao mataji matatu ya ligi pamoja na Kombe la Ulaya
1988. Alinyakua mengine matatu aliporejea hapo na kukaa kuanzia 2002
hadi 2006.
Amesafiri na kufundisha nchini Uturuki na Hispania pamoja na timu za
taifa za Uholanzi, Korea Kusini na Australia. Aliwafikisha Urusi
kwenye nusu fainali za Euro 2008 kabla ya kuingia Chelsea baada ya
kufukuzwa Luis Felipe Scolari.
Hiddink akiwa Anzhi Makhachkala nchini Urusi, alimsajili Willian
kutoka Shakhtar Donetsk na sasa anamkuta Chelsea, akiwa mmoja wa
wachezaji walio kwenye kiwango kizuri kwa sasa.