in , , ,

Mourinho hakuna kulala

Kocha wa Chelsea aliyefukuzwa kazi jana, Jose Mourinho, amesema
hatakwenda mapumziko kwa sababu hajachoka wala hahitaji likizo,
ikimaanisha kwamba yupo tayari kwa kazi wakati wowote.

Mourinho alifukuzwa kazi na mmiliki wa klabu, bilionea wa Urusi Roman
Abramovich, ikiwa ni mara ya pili, lakini safari hii ni kutokana na
timu kufanya vibaya kuliko ilivyopata kutokea kwenye historia ya
wawili hao kufanya kazi pamoja.

Chelsea wapo nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi, ikiwa ni pointi moja
tu juu ya eneo la kushuka daraja, hivyo bodi ya wakurugenzi ilipokaa
na kujadili suala hilo, iliona haja ya hatua kuchukuliwa, ndipo
Abramovich ‘akainua shoka’ na kumaliza kazi.

Taarifa ya wakala anayemwakilisha kocha huyo mwenye umri wa miaka 52
ilieleza kwamba atabaki London, na kwamba Chelsea ndio walioamua
aondoke, tofauti na ilivyokuwa kwenye klabu nyingine na kwamba
hatahudhuria mechi kubwa. Taarifa ilisema:

“Hatakwenda (Mourinho) mapumzikoni, hajachoka, hayahitaji. Yupo vizuri
kabisa na tayari kusonga mbele. Jose Mourinho anafurahi kwamba alirudi
Chelsea kwa sababu aliweza kuwapa washabiki taji jingine la ubingwa wa
Ligi Kuu ya England.

“Anaona fahari sana juu ya mataji yake nane Chelsea na anawashukuru
washabiki kwa kumuunga mkono kwao kwa hali ya juu katika vipindi vyote
viwili klabuni. Tangu aanze kazi, kuna wakati Jose aliamua kuondoka
katika klabu fulani, lakini ni Chelsea tu ambako ni klabu iliamua
kumwondoa.

“Hatahudhuria mechi kubwa kwa sababu anataka kutuliza aina yoyote ya
uvumi unaoweza kuzuka juu ya hatima yake. Jose ataendelea kuishi
London na anatumaini kwamba yeye na familia yake watapewa fursa ya
kufanya hivyo kwa faragha.”

Mazungumzo yamekuwa yakiendelea kwa muda sasa na kocha aliyeachia
ngazi Timu ya Taifa ya England, Guus Hiddink aliyepata kushika nafasi
hiyo Stamford Bridge katika kipindi cha mpito na wakikubaliana
ataibeba mikoba ya Mourinho.

Wakuu wa Chelsea walianza mazungumzo na Mholanzi huyo tangu akiwa kwao
kisha yakashika kasi alipoingia London lakini inaelekea kuna mambo
alitaka kuhakikishiwa kwanza pamoja na kujua mazingira ya sasa klabuni
yakoje.

Mourinho amekuwa akihusishwa na kujiunga na Manchester United, nafasi
anayodaiwa aliitaka tangu 2013 Sir Alex Ferguson alipong’atuka lakini
pia anahusishwa na Bayern Munich ambako kocha wao, Pep Guardiola
anamaliza mkataba na huenda akaondoka.

Kwingine ni Real Madrid ambako Rafa Benitez hafanyi vizuri sana,
lakini Rais Florentino Perez aliyeachana na Mourinho miaka michache
iliyopita huko Madrid, amesema klabu hiyo haina mpango wa haraka wa
kumrejesha huko.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Guus Hiddink asubiriwa

Tanzania Sports

Hiddink atua Chelsea