in , , ,

Ghana na Mali wavuka

*Wakongomani waishia kulia uwanjani

Timu za Afrika Magharibi za Ghana na Mali zimefuzu kuingia robo fainali ya Kombe la Mabingwa Afrika (AFCON) kutoka kundi B.

Ghana walijihakikishia nafasi kiulaini baada ya kuwacharaza Niger mabao 3-0 na kushika usukani wa kundi lao baada ya kumaliza mechi tatu kila moja.

Mali walifanya kazi ngumu hadi kufuzu, kwani walitangulia kufungwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa penati, kabla ya kujipanga upya na kusawazisha.

Sare pekee ilitosha kuwavusha, huku Kongo wakihitaji ushindi wa aina yoyote ili wasifunge virago kurudi Kinshasa.

Hata hivyo, baada ya mchezo kumalizika, ilikuwa ni vilio kutoka kwa wachezaji na washabiki Wakongomani, lakini wale wa Niger waliona ni kawaida, kutokana na udhaifu wa tangu mechi za mwanzo.

Nahodha wa Ghana, Asamoah Gyan alikuwa kichocheo cha ushindi wa Jumatatu hii, na ndiye aliyefunga bao la kwanza, kwa kuunganisha majalo ya Albert Adomah.

Alikuwa ni Gyan tena, aliyemtengea pande mfungaji wa bao la pili, Christian Atsu, aliyeweka gambani kabla ya kuusindikiza wavuni.

Ghana walifunga kitabu cha mabao pale Gyan alipopiga kichwa maridadi, kikapanguliwa kidogo na golikipa Douda Kassaly kabla ya John Boye kuutia mpira kimiani.

Ghana walionesha mchezo mzuri na kutoka na ushindi mkubwa, licha ya kuingia uwanjani wakijua walichohitaji ili kufuzu ilikuwa suluhu au sare tu.

Yawezekana kiu ya kombe ndiyo inayowasukuma wachezaji kujituma zaidi, kwani tangu mwaka 1982 hawajatwaa kombe hilo, na nahodha Gyan aliapa kwamba watajitahidi kuwafurahisha wananchi wao safari hii.

Ama kwa upande wa Mali, walijikuta wakitunguliwa bao baada ya kiungo Dieumerci Mbokani kuwanyanyua vitini washabiki wengi wa Kongo waliohudhuria katika dakika ya tatu tu ya mchezo.

Hata hivyo, Mali walisawazisha bao hilo dakika ya 11 baada ya Mahamadou Samassa kupokea pasi safi ya Adama Tamboura.

Tangu wakati huo ilibaki kuwa mtafutano, kila timu ikitaka kupata bao la ushindi, lakini shinikizo likiwa kwa Wakongomani, ambao kocha wao Claude LeRoy alikuwa akihangaika kuwaelekeza wachezaji wake bila mafanikio.

Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Mali kufuzu hatua hiyo, ambapo mwaka jana walifika hadi nusu fainali, na kuishia kuwa washindi wa tatu kwenye fainali zilizogfanyika Gabon na Guinea ya Ikweta.

Jumanne hii kundi C linatafuta timu mbili za kuingia robo fainali, ambapo Burkina Faso wanaoneshana kazi na Zambia, huku Nigeria wakiwakabili Ethiopia.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Cape Verde waweka rekodi AFCON

Zambia wavuliwa ubingwa Afrika