in , ,

Zambia wavuliwa ubingwa Afrika

*Burkina Faso, Nigeria robo fainali

Mabingwa wa Afrika, Zambia wameaga mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa aibu.

Chipolopolo waliotwaa kombe hilo mwaka jana, wametupwa nje baada ya kutoka sare mechi zote tatu na kushindwa kuingia kwenye nane bora.

Walikuwa ni Burkina Faso waliowatibulia Zambia ndoto za kutetea ubingwa, baada ya kuwabana muda wote wa mchezo na kutoka suluhu.

Farasi Wasiohasiwa, kama wanavyoitwa Burkina Faso, wenyewe wameweka historia ya kuvuka, kwani wamekuwa na kawaida ya kutolewa kwenye hatua za awali.

Kumbukumbu pekee ya karibu zaidi ya kufanya vizuri kwa Burkina Faso ni 1998 walipoishia nafasi ya nne, michuano ilipofanyika kwao Afrika Magharibi.

Kwa suluhu hiyo na Nigeria kuwafunga Ethiopia, Burkina Faso wameshika nafasi ya kwanza kwenye kundi C, wakifuatiwa na Nigeria.

Kwa msingi huo, Zambia imeungana na Ethiopia kufunga safari tofauti za kurejea makwao, wakiacha walioonesha soka zuri kuingia hatua za mtoano.

Farasi hao waligangamala kwenye ngome kiasi cha kuwanyima washambuliaji wa Zambia nafasi ya kufurukuta, japokuwa kwa ujumla Chipolopolo hawakuonesha makali yoyote.

Zambia wanakuwa mabingwa watetezi wa kwanza kutupwa nje ya mashindano katika hatua ya mwanzo, tangu Algeria walipoaga kwa mtindo huo mwaka 1992.

Burkina Faso ambao wamekuwa wakichukuliwa kwamba ni wageni, sasa wameonesha dhamira ya kufanya kweli, kama walivyosisitizwa na Rais wao Blaisie Compaore.

Hata hivyo, Farasi hao walipata pigo dakika ya 11, baada ya mchezaji wao tegemeo na mfungaji bora wa mashindano hadi sasa, Ali Traore kutolewa nje na machela baada ya kuumia goti.

“Tuliamini kwamba tulikuwa na nafasi ya kusonga mbele kwenye mashindano haya…kichocheo kikubwa kwetu kilikuwa kusogea karibu na kufuzu na kucheza dhidi ya mabingwa,” anasema kocha wa Burkina Faso, Paul Putt.

Victor Moses anayekipiga Chelsea alikuwa shujaa wa Nigeria kwa upande mwingine, kwa jinsi alivyokoleza mashambulizi, akapata penati mbili na kuzifunga.

Ufungaji wake ulikuwa mwiba kwa Ethiopia, lakini pia kwa Zambia, kwani iwapo Nigeria na Ethiopia wangetoka sare, Zambia wangevuka na Burkina Faso.

Wakijua kwamba walihitaji ushindi tu, pia wakiwa kwenye shinikizo kutoka nyumbani kwamba hawakuwa na kisingizio cha kutoshinda, Nigeria walifurahia ushindi huo.

Hata hivyo hawakuupata kwa staili ya aina yake, kwa sababu walibanwa muda mwingi wa mchezo, hadi kipindi cha pili walipofanikiwa kupata matuta hayo dakika za 79 na 90.

Hapakuwa na matukio ya kuvutia sana katika muda mwingi wa mchezo, zaidi ya golikipa Alula Girma kumwangusha Moses na kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Kituko kilikuwa mchezaji wa kati, Addis Hintsa kuingia golini, kwa vile Wahabeshi walishamaliza idadi ya wachezaji wanaotakiwa kubadilisha.

Hata hivyo, iliwachukua Swala hao wa Ethiopia karibu dakika tano kukamilisha matakwa ya mchezaji huyo wa kati kuingia golini.

Mwamuzi alimzuia kwa sababu namba za fulana hazikufanana na za kaptula yake, hivyo akasaidiwa na wana timu wenzake kuzibadilisha kwa kutumia gundi ya karatasi, ambapo hapakuwa na uwiano wenye kiwango cha kufaa.

Jumatano inashuhudia Ivory Coast watacheza na Algeria, huku Togo wakiumana na Tunisia katika mchezo wa mwisho wa mtoano wa mashindano haya yanayoendelea nchini Afrika Kusini.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Ghana na Mali wavuka

Dua la Togo lafika