Mashindano ya soka ya afrika ya Afcon yamemalizika salama. Yamemalizika huku mwenyeji timu ya taifa ya Ivory Coast ikiibuka kuwa kidedea wa mashindano hayo kwa kuifunga timu ya taifa ya Nigeria. Hakuna aliyetegemea kwa haraka kwamba taifa hilo ambalo lilianza vibaya kwa kusuasua katika mashindano hayo kwamba ndio lingeibuka kuwa bingwa mwisho wa siku.
Kuna waliodhani labda bingwa angekuwa ni taifa la Moroko kwa namna ambavyo taifa hilo lilifanikiwa katika mashindano ya kombe la dunia na kuna baadhi walidhani kwamba wangefika mbali. Kuna waliodhani labda bingwa mtetezi taifa la Senegal wangeweza kutetea kombe lao na hatimaye wangeibuka mabingwa tena lakini la hasha hawakuweza kubeba ubingwa huo. Lakini timu hizo zote hazikuweza hata kuingia hatua ya nusu fainali na katika hatua ya nusu fainali kulikuwepo timu ambazo hazikutarajiwa kabisa.
Mashindano ya mwaka huu yamefanyika katika nchi ambayo kwa mda mrefu ilikuwa kwenye vita ya wenyewe na wakaweza raia wake kumaliza tofauti baina zao na kurudi kwenye hali za kawaida. Baada ya kurudi kwenye hali ya kawaida taifa hilo liliweza kujipanga vizuri na hatimaye kuweza kushinda mashindano hayo ndani ya mwaka 2015.
Mwaka huu taifa hilo limeandaa mashindano hayo kwa kiwango kikubwa sana. Mashindano hayo ambayo yamechezwa katika jumla ya viwanja 6 vya kisasa ambavyo ni vya hadhi ya kimataifa. Hakika mashindano hayo yamekuwa ni funzo kwa mataifa mengi ya kiafrika ikiwemo nchi ya Tanzania ambayo yatarajia kuwa ni mwenyeji mwenza wa mashindano hayo kwa mwaka 2027.
Katika mambo mengine ambayo mashindano hayo yametufundisha ni kwamba yawezekana mafanikio yakapatikana kupitia makocha wazawa ambao wapo katika nchi husika. Ivory coast kwa mwaka huu imekuwa ni bingwa baada ya kufanya maamuzi magumu ya kuondoa kocha wa kigeni na kukabidhi timu kwa kocha mzawa.
Kocha huyo si mwingine bali ni Emerse Fae ambaye wakati mashindano yanaanza alikuwa ni kocha msaidizi wa timu hiyo ya taifa lakini akajikuta anapewa nafasi hiyo ya kuwa kocha mkuu wa timu hiyo wakati wakiwa wanaelekea mchezo wa tatu wa timu hiyo baada ya timu hiyo kupoteza michezo miwili ya awali katika hatua ya makundi na kujikuta kwenye hatari ya kuaga mashindano hayo ambapo kamati tendaji ya chama cha soka cha nchi hiyo ikalazimika kumtimua kocha mkuu na kukaimisha timu kwa kocha Emerse Fae.
Kabla ya mashindano haya Fae hakuwa kocha mwenye jina barani Afrika kwani hakuwa anafahamika sana nje ya mipaka ya nchi yake lakini baada ya mashindano amekuwa ni maarufu na matumaini kwamba atakabidhiwa timu hiyo ya taifa kijumla kama kocha mkuu.
Afcon iliyotangulia halikadhalika ubingwa ulienda kwa taifa la Senegal ambapo aliyeipa ubingwa alikuwa ni kocha mzawa ajulikanaye kama Aliou Cisse na hiyo ilikuwa mnamo mwaka 2019. Angalau kidogo Aliou Cisse alikuwa anajulikana kutokana na kwamba wakati alipokuwa mchezaji aliongoza Senegal kwa mara ya kwanza kufika katika hatua ya robo fainali ya kombe la dunia la mwaka 2002.
Aliou Cisse hakuwa chaguo la kwanza katika kupewa mikoba ya kufundisha timu hiyo bali alipewa nafasi hiyo kwa kuwabembeleza magwiji wa soka wa taifa hilo kwenda kuongea na raisi wa taifa hilo kubembeleza apewe nafasi hiyo na aliridhia kupewa mshahara mdogo ili mradi apewe jukumu hilo na hakuwaangusha kwani alilibeba kombe hilo.
Makocha wenye rekodi ya kulibeba kombe hilo mara nyingi wote nao halikadhalika ni wazawa. Makocha hao ni Charles Guyufi wa Ghana ambaye alilibeba mara tatu yaani mwaka 1963, 1965 na mwaka 1982. Mwingine ni Hassan Shehata wa misri ambaye alilibeba mara tatu mfululizo yaani mwaka 2006, 2008 na 2010.
Shehata atakumbukwa zaidi kwani alibeba mfululizo katika nyakati ambazo soka la afrika lilikuwa limeanza kuwa lenye ushindani mkubwa sana kwani mataifa ambayo yalikuwa yanashiriki AFCON yalikuwa yamejaa mastaa wa vilabu vikubwa barani Ulaya. Shehata atakumbukwa kikosi chake kilikuwa kimejaa wachezaji ambao asilimia kubwa wanacheza katika ligi ya ndani ya nchi hiyo ya Misri.
Na hiyo sio mara pekee ambapo taifa la Misri ilibeba kombe hilo kwa kutumia kocha mzawa kwani mwaka 1998 walilibeba kupitia mzawa mwingine ambaye ajulikanaye kama Mahmood El Gohary na halikdhalika mwaka huo kikosi chao kilikuwa kimejaa wachezaji wengi ambao walikuwa wanacheza katika ligi ya ndani ya Misri.
Baada ya Shehata katika Afcon iliyofuatia ya mnamo mwaka 2013 taifa la Nigeria lilifanikiwa kuwa bingwa huku likuwa chini ya kocha mzawa Stephen Keshi ambaye naye pia aliwahi kuwa mchezaji mahiri wa taifa hilo kabla ya kutundika daruga na kustaafu kucheza soka.
Mwaka 2019 Algeria ilibeba ubingwa wa Afcon ambao waliupata chini ya kocha mzawa Djamel Belmadi. Kwa hiyo makocha wazawa wamekuwa wanaleta manufaa makubwa barani afrika. Hata katika kombe la dunia lililopita timu ya taifa ya Morokko ilifanikiwa kufika mbali baada ya kumtumia kocha mzawa bwana Walid Regragui ndipo walipoweza kufikia mafanikio hayo.
Naomba nisitafsiriwe vibaya kama ni mbaguzi bali hili ni jambo ambalo linafanyika maeneo tofauti hata na afrika na kuleta mafanikio ukiangalia timu ya taifa ya Brazil mara zote ambazo imeweza kuwa bingwa wa kombe la dunia ilikuwa na kocha wazawa halikadhalika na ujerumani mara zote ilizobeba kombe la dunia ilikuwa na makocha wazawa.
Comments
Loading…