in , ,

Cape Verde waweka rekodi AFCON

Bafana Bafana nje AFCON

*Wenyeji Bafana Bafana nao wavuka

Nchi ndogo zaidi kuwahi kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), Cape Verde wameingia robo fainali.

Papa hao wa Bluu wamefanya kazi ya ziada Jumapili hii, wakitoka nyuma baada ya kufungwa na Angola, kurejesha bao na kushinda kwa mabao 2-1.

Cape Verde sasa wametinga kwenye timu nane bora, wakiwashangaza wadau walioshuhudia au kufuatilia pambano hilo katika mji wa Port Elizabeth.

Angola walipata bao dakika ya 33, baada ya beki wa Cape Verde, Fernando ‘Nando’ Maria Neves kujifunga.

Bao hilo halikuwakatisha tamaa, kwani waliongeza jitihada na kusawazisha zikiwa zimebaki dakika tisa, pale beki mwingine, Fernando Varela alipofunga bao safi kwa kichwa.

Mchezaji Heldon Ramos aliyeingia uwanjani dakika ya 46, alipachika bao katika dakika ya 90 ya mchezo, na kuacha washabiki wa taifa hilo wakilipuka kwa furaha.

Kisiwa cha Cape Verde kilianza kuvuta hisia za watu wengi kwenye mechi za kufuzu kushiriki fainali hizi, kutokana na kufanya kwake vizuri dhidi ya vigogo.

Bado wengi wanaikumbuka Oktoba 14 mwaka jana, kwani Papa hao walifuzu kwa fainali hizi walipowafungisha virago Simba Wasiofugika wa Cameroon.

Waliwatoa Cameroon kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya kufungwa mabao 2-1 katika mechi ya marudiano Stade Ahmadou Ahidjo jijini Yaoundé, Cameroon, wakitangulia kwa ushindi wa mabao 2-0 nyumbani.

Cape Verde ilicheza mechi yake ya kwanza na timu ya nje ya Afrika kwa kukipiga na Luxembourg Novemba 2, 2002 na kutoka suluhu.

Wenyeji Afrika Kusini nao wamefuzu kwa robo fainali, baada ya kujikita nafasi ya kwanza ya kundi lao, kwa kutoka sare ya mabao 2-2 na Morocco.

Hata hivyo, Bafana Bafana walikuwa na wakati mgumu, kwani walimaliza kipindi cha kwanza wakiwa nyuma kwa bao moja.

Pamoja na kuwa na washabiki wengi uwanjani, wachezaji walishindwa kujijenga kimchezo, kuyumbisha kiungo na kuipita beki ya Morocco ipasavyo.

Ilibidi wasubiri hadi dakika ya 86 kujihakikishia sare.

Walianza kupelekeshwa tangu mwanzo wa mchezo, ambapo dakika ya 10 tu Issam El Adoua aliwapatia Morocco bao la kwanza.

May Mahlangu wa Bafana Bafana waliwarejeshea matumaini washabiki kwa kupachika bao la kusawazisha, lakini hawakuongeza shinikizo baada ya hapo.

Wakati washabiki waliojaa uwanjani walidhani walishaokoka kichapo, Mehdi Namli alifunga bao katika dakika ya 82 na kukatisha kwa muda chereko chereko.

Kocha wa Afrika Kusini, Gordon Igesund, katika shati lake jeupe lililokuwa liking’aa kwenye Jua la Durban alibadilika sura na kuwataka wachezaji wake waamke.

Alikuwa Siyabonga Sangweni aliyewakata maini Wamorocco kwa kusawazisha bao dakika chache kabla ya mechi kumalizika, na kuwafungisha virago wapinzani hao wa kaskazini mwa Afrika.

Sare ya Bafana Bafana, hata hivyo, imeonekana kama ya bahati zaidi, kwa sababu ya mazingira yote ya mchezo, na jinsi Morocco walivyotawala idara mbalimbali.

Hatua kubwa zaidi waliyopata kufika Bafana Bafana ni katika soka ni kutwaa kombe hili mwaka 1996 walipoliandaa kwa mara ya kwanza.

Katika fainali ya Kombe la Dunia la FIFA mwaka 2010 iliyofanyika Afrika Kusini, Bafana Bafana hawakuvuka raundi ya kwanza, hivyo wana kazi kubwa robo fainali.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Ivory Coast robo fainali

Ghana na Mali wavuka