Kwenye mchezo wa soka hakuna mchezaji ambaye hana ndoto za kuchezea Real Madrid. Inawezekana mchezaji asijiunge nayo ama akachezea timu fulani hadi mwisho wa maisha yake, lakini linapofika suala la kusajiliwa na Real Madrid wengi wao hujutia baada ya kustaafu.
Tumeyaona hayo kwa Andre Pirlo aliyestaafia Juventus, Francesco Totti aliyestaafia AS Roma na wengine ambao hawakupata nafasi ya kuchezea miamba hiyo ya Hispania.
Eden Hazard ni nyota ambaye amebahatika kujiunga na timu ya ndoto yake. Kuhama kutoka Lille ya Ufaransa kwenda Chelsea ya England ilikuwa hatua ya kukua kisoka wakati ambao Real Madrid haikuonesha nia ya kumsajili. Lakini sasa Hazard ni mchezaji wa Real Madrid akiwa amejiunga msimu uliopita.
Msimu wake wa kwanza 2019/2020 amefanikiwa kutwaa taji la La Liga chini ya kocha ambaye anamhusudu tangu akiwa mchezaji Zinedine Zidane. Real Madrid walilipa dau la pauni milioni 143 ili kupata huduma ya Eden Hazard.
Jambo kubwa zaidi linaloeleweka ni kwamba Real Madrid ilikuwa na matarajio makubwa kutoka kwa nyota huyo wa zamani wa Chelsea, ambaye alipata fursa ya kucheza chini ya kocha anayempenda zaidi.
Hata hivyo Hazard hadi leo hajafanikiwa kuonesha kile kiwango kilichosababisha pesa nyingi zitolewe katika usajili wake. Sasa ana miaka 29, amefunga mabao matatu katika mechi 29.
Kasi yake ya mchezo imekumbwa na majeraha ya mara kwa mara. Anaweza kucheza mechi tatu mfululizo kisha zinazofuata akawa hospitalini kupatiwa matibabu. Tatizo hili limekuwa kubwa sasa, Hazard haonekani kuwa na mchango mkubwa kama ule wa Lucas Vazquez wala thamani yake aliyonunuliwa.
Katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Inter Milan, ilionekana kama Hazard angeweza kuinuka zaidi na kucheza kwa kiwango cha juu. Alianza mchezo taratibu na alionesha namna anavyoweza kutoa mchango.
Kifundi na uzoefu Hazard ni mzuri kuliko Vinicius Junior,Rodrygo Goes,Martin Odegaard, Lucas Vazquez, Mariano Diaz na hata Luka Jovic. Ufundi wake wa kusoma mchezo, uwezo wa kutengeneza mabao, kuifungua safu ya ulinzi ya timu pinzani pamoja na kucheza kitimu ni mambo yanayompa sifa Hazard.
Timu inapokosa maarifa ya kuipasua safu ya ulinzi ya timu pinzani, mara nyingi Hazard ndiye amekuwa akitumika kufanya kazi hiyo. Yeye hutengeneza mianya ya kufunga na kuipa ushindi timu yake.
Hizo ndizo sifa alizokuwa nazo Lille hata kumvutia Zidane ambaye kwa miaka mingi alibainisha umuhimu wa kusajiliwa nyota huyo alipokuwa kinda. Hata hivyo Hazard akasajiliwa na Chelsea na akaonesha ubora wake kwa kipindi kirefu.
Uwezo alionao ndio chachu ya kusajiliwa Real Madrid. Na kwahiyo matarajio yaliyokuwepo ilikuwa lazima yatokee. Madrid kama klabu ilitambua kuwa mauzo ya jezi yangekuwa makubwa. Ilitambua mchango wake kiufundi utaongeza maarifa ndani ya kikosi cha Real Madrid. Vilevile ungesaidia kunyambulisha maagizo ya kiufundi ya kocha Zidane.
Lakini Hazard ni nyota ambaye amekuwa akisua sua msimu wa pili sasa. Alinunuliwa akiwa na miaka 28, mzoefu wa kutosha na ambaye amejijengea heshima inayompa nafasi ya kutamba kikosi chochote. Lakini mambo yamekuwa magumu kwake. Real Madrid haijapata mchango wake. Madrid wameishia kumtibu majeraha mengi huku kukiwa na maswali juu ya mustakabali wake.
Inatarajiwa Hazard awe mchezaji wa kutumainiwa kuliko chipukizi niliowataja hapo juu. Inatarajiwa Hazard awe kiongozi wa pili baada ya Karim Benzema katika safu ya ushambuliaji. Lakini kwa sasa inawategemea chipukizi ambao hawawezi kubeba mizigo mizito ya ushindi wa timu hiyo.
Martin Odegaard anazidi kuimarika akiwa na miaka 21. Vinicius na Rodrgyo bado ni vijana walio chini ya miaka 20 ambao wanategemewa kwa miaka mitano ijayo. Marco Asensio bado hajarudi katika kiwango chake, lakini naye ni miongoni mwa wachezaji waandamizi wanaohitajika kubeba majukumu ya timu.
Pembeni ya Hazard jina linalokaribia ni Asensio na Lucas Vazquez. Ni Vazquez pekee amekuwa akitumika nafasi tofauti na kutoa mchango mkubwa kuliko wengine waliotajwa hapo juu. Nafasi ya winga ambayo Hazard hucheza akiumia inabaki kwa chipukizi. Isco naye hajawa katika kiwango bora na ndio maana amebaki kucheza benchi tu.
Huyu Hazard wa sasa anayecheza mechi 29 na kupachika mabao matatu anasikitisha mno. Haonekani kuwa timamu kimwili kwa sababu amekuwa akiumia mara kwa mara.
Je, inawezekana tatizo ni matibabu hafifu? Tatizo ni benchi la ufindi kwenye kitengo cha viungo? Je, ni kitu gani kinachokumba nyota huyo ambaye alitarajiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia?
Kwa hakika jambo hilo litakuwa linamuumiza kichwa Zidane kwa vile amekuwa akiamini Hazard ni mmoja wa nyota waliotakiwa kutikisa dunia mapema na alitakiwa kuchezea Real Madrid. Klabu imemsajili akiwa na miaka 28, huwezi kusema ni umri mkubwa kusajili na kwamba labda amefika kilele cha mafanikio.
Zidane mwenyewe alisajiliwa akiwa na miaka 29 akitokea Juventus Turin ya Italia, lakini alifanya mambo makubwa klabu hapo.
Mashabiki wa Real Madrid hawaambiliki kuhusu Zidane. Hawajali kuwa alisajiliwa akiwa na miaka 29 yaani kuelekea mwishoni mwa uwezo wake lakini kazi aliyoifanya kwa kipindi chote alichocheza Real Madrid inamfanya awe na heshima kubwa.
Kwa wakati huu itakuwa ni kujidanganya Hazard kupewa heshima na mashabiki wa Real Madrid huku wakitambua mchango wake mdogo. Vilevile ni vigumu kutegemea kuwa labda ataweza kurejesha kiwango Real Madrid kama kile alichokionesha akiwa Chelsea.
Majeraha ya mara kwa mara yanarudisha nyuma uwezo wa mchezaji. Tumeona mastaa kadhaa wakishindwa kuendelea na kandanda tangu walipopata majeraha. Real Madrid ilishuhudia kiwango bora cha chipukizi wake Jesse Rodriguez lakini tangu alipoumizwa mguu hakuwahi kurejesha kiwnago chake cha awali.
Ni kama majeraha hayo yalizika kabisa uwezo wake. Jesse alijiunga na miamba ya Ufaransa PSG, lakini hakufanya maajabu na mwisho wakamtoa kwa mkopo kabla ya kumuuza kabisa.
Hazard anafikirisha mno kila anapokuwa uwanjani. Uchezaji wake umepunguza kasi yake ingawa muono na maarifa yake yanaonekana kwenda vizuri. Mchezo pekee ambao ulivutia kumtazama Hazard akicheza ni dhidi ya Inter Milan nchini Italia. Alijaribu kutuonesha juu ya kile akilichomfanya asajiliwe Real Madrid. Lakini bila mafanikio hakufikia hata robo ya uwezo alioonesha Chelesa. Sijui ni nini kilichotokea kwake.
Muda utaongea.
Comments
Loading…