KAMA ingekuwa lawama za uzalendo bila shaka kocha wa PSG, Luis Enrique angelaumiwa kwa kusababisha kipaji cha Marco Asensio kuyumba klabuni hapo. Lakini ni Luis Enrique huyo huyo amewahi kueleza umma wa Hispania kuwa ni vizuri Marco Asensio akatafuta timu ambayo ingempa nafasi ya kucheza kuliko alivyokuwa anasugua benchi pale Real Madrid. Hata hivyo Luis Enrique akaenda kuwa kocha wa PSG baada ya kutemana na kibarua cha kuinoa timu ya Taifa ya Hispania.
Akiwa PSG hakumtumia ipasavyo Marco Asensio ambaye alikuwa akimtamani kila mara kwenye kikosi cha timu ya Taifa. Asensio kuona hivyo alilazimika kutoendelea kuichezea Real Madrid kwa sababu hakupata namba katika kikosi cha kwanza. Hali hiyo ilimfanya ashuke kiwango na ari ya kandanda. Kwenda kwake PSG ilikuwa njia ya kunusuru kipaji chake, lakini hali ya mambo sasa imekuwa tofauti. Marco Asensio yule winga na namba kumi ambaye alisifiwa na Zinedine Zidane kuwa ana mguu bora zaidi wa kushoto kando ya Lionel Messi. Kwa Zidane alimwona Marco Asensio kama mchezaji mwneye kipaji kizuri na amekuwa na matumizi bora ya mguu wa kushoto.
Wakati dirisha dogo la usajili la Januari likiwa limefika ukingoni, Marco Asensio ni miongoni mwa nyota waliolazimika kuvihama vilabu vyao. Asensio amejiunga na klabu ya Aston Villa, mabingwa wa zamani wa Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa sambamba na Marcus Rashfod aliyetokea Man United. Kikosi cha Unai Emry kinaundwa na washambuliaji vijana Marco Asensio, Marcus Rashford, na Ollie Watkins ambao wanatarajiwa kuimarisha Aston Villa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Aston Villa walikuwa wanahaha kuongeza wachezaji katika kikosi chao ili kuimarisha safu ya ushambuliaji hivyo majina hayo mawili ya Asensio na Rashford yameingia klabu hapokwa mkopo. Ikumbukwe Aston Villa wamempoteza mshambuliaji wao Jhon Duran ambaye amejiunga na Al Nassr miamba ya Saudi Arabia kwa ada ya pauni miloioni 65. Aston Villa walilazimika kuingia sokoni kupata angalau wachezaji wa mkopo ili kukimbizana na makataa ya dirisha la usajili.
Marco Asensio ana umri wa miaka 29 kwa sasa akiwa chini ya mkataba na PSG hadi Juni 2026. Alijiunga na PSG mapema Julai mwaka 2023 wakati akitokea Real Madrid. Asensio amefunga mabao 7 katika mechi 47 alizocheza akiwa PSG. Idadi hiyo ni ndogo kulinganisha na kile alichokifanya akiwa Real Madrid ambako alifunga mabao 61 katika michezo 286.
Hata hivyo amekuwa mchezaji anayesugua benchi kwa muda mrefu chini ya Luis Enrique na katika mechi tatu zilizopita hakutumika kwenye kikosi cha kwanza. Aston Villa wamekuwa kwenye hekaheka za kukiongezea nguvu kikosi chao, huku wakishuhudia kuyumba kwao katika mechi kadhaa za EPL. Mfano katika mchezo wao wa Ligi Kuu jumamosi iliyopita waliambulia kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Wolves, na Unai Emery alisisitiza kuwa klabu yake hiyo ilihitaji kuongeza wachezaji wenye uzoefu na mashindano makubwa yakiwemo Ligi ya Mabingwa pamoja na EPL. Hivyo ujio wa Marcus Rashford na Marco Asensio ni sehemu ya kukiimarisha kikosi chake.
“Tulihitaji wachezaji wapya ili kuziba mapengo ya wale walioondoka. Timu hii inahitaji nguvu ya ziada ili kuwapa wepesi wachezaji waliopo. Nafikiri tunawapata wachezaji tunaowahitaji na kuingia kwenye hatua ya 16 mtoano ya Ligi ya Mabingwa. Katika hatua hii lazima uwe na wachezaji wenye uzoefu kupata matokeo na pointi kwenye EPL ambako tutajaribu kukusanya pointi zetu na kushika nafasi ya nane, saba, sita hadi tano,” alisema Unai Emery alipozungumza na vyombo vya habari kuhusu usajili mpya.
Marco Asensio amekuwa akihangaika kuimarisha uwezo wake pamoja na kumshawishi kocha Luis Enrique ili kupata nafasi katika kikosi cha kwanza. Ujio wa Asensio na Rashford unatarajiwa kuipandisha Aston Villa ambayo inafanya jitihada kuhakikisha wanacheza kwa mafanikio msimu huu kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Asensio ni mchezaji mwenye uzoefu wa mashindano ya UEFA akiwa ametwaa mataji akdhaa chini ya kocha Zinedine Zidane na Real Madrid.
Kama unahitaji winga anayefahamu vyema upachikaji wa mabao basi Asensio ni miongoni mwa nyota hao. Uwezo wake wa kucheza winga wa kulia, namba kumi na kushoto vinampa nafasi yakutumika popote kadiri anavyotaji kocha. Kwenye kikosi cha Aston Villa kwa sasa washambuliaji watatu wanaoweza kuongoza jihazi hilo. Rashford, Asensio na Watkins na bila shaka Joao Felix atakuwa miongoni mwa wachezaji wao muhimu kwenye mashindnao ya Ligi ya Mabingwa pamoja na Ligi Kuu England. Huu ni wakati ambao Asensio anatakiwa kurudisha makali na kuokoa kipaji chake cha soka chini ya Unai Emery huku umri wake nao ukielekea ukingoni.
Comments
Loading…