Man City mdomoni mwa Barca
*Arsenal vs Monaco, Chelsea vs PSG
Ratiba ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imetoka, ambapo mabingwa wa England, Manchester City wamepangwa kucheza na Barcelona kwenye mechi mbili za mtoano, ikiwa ni msimu wa pili mfululizo wanapangwa hivyo.
Katika hatua hii ya 16 bora, Chelsea watamenyana na Paris Saint-Germain wa Ufaransa wakati Arsenal wamepangiwa kucheza na Monaco wa Ufaransa pia. Mabingwa watetezi watapepetana na Schalke ya Ujerumani wakati Atletico Madrid watavaana na Bayer Leverkusen.
Droo hiyo inaonesha kwamba Bayern Munich watakabiliana na Shakhtar Donetsk, Juventus wao ni Borussia Dortmund, huku Basel wakipimana nguvu Porto kwenye mechi zitakazochezwa Februari na Machi mwakani.
Katika mechi za msimu uliopita hatua kama hii, Barca waliwapiga City 4-1 kwa wastani, ambapo mechi ya kwanza iliyopigwa Etihad walishinda 2-0 na ile ya pili wakapiga 2-1 kwao Nou Camp.
Chelsea nao wanakutana na PSG kwa mwaka wa pili mfululizo, ambapo msimu uliopita katika mazingira ya aina yake waliwashinda Wafaransa hao na kusonga mbele kwenye robo fainali. Kivutio kwa mechi hiyo ni kwamba mchezaji wa zamani wa Chelsea aliyeonwa na kocha Jose Mourinho hafai atakuwa kwenye kikosi cha PSG. Aliuzwa huko kwa pauni milioni 40.
Arsenal watacheza dhidi ya Monaco, timu ambayo kocha Arsene Wenger aliwafundisha kuanzia 1987 hadi 1994. Katika mechi zao zote, Monaco walifunga mabao manne tu, lakini bado wakaibuka nafasi ya kwanza.
Ofisa wa Arsenal, David Miles amesema kwamba katika miaka michache iliyopita Arsenal wamekuwa wakikumbana na timu kubwa zaidi Ulaya tofauti na sasa, lakini akasema kwamba hawawabezi Monaco, kwa sababu walistahili kufika hatua ya 16 bora.
Akizungumzia juu ya kupangwa dhidi ya Barcelona, Mkurugenzi wa Soka wa Man City,Txiki Begiristain aliyepata kuchezea Barca alisema kwamba kila mchezo kwenye droo hiyo ni sawa na kwamba wanasubiri kwa hamu kuwavaa Barcelona.
“Tunajiamini sana kutokana na jinsi tulivyofuzu kwa kuwafunga Bayern Munich nyumbani kwao na kisha kuwachakaza Roma ugenini,” akasema.
Mtendaji wa Chelsea, David Barnard anasema kupangwa dhidi ya PSG ni vyema, kwa maana ya aina ya timu lakini pia kwa ajili ya washabiki wao.
Comments
Loading…