in , ,

DERBY YA INTERMILAN NA MILAN IMEBAKI KWENYE VITABU

Vitabu vya historia vinaniambia uwanja wa San Siro pale katika mji wa
Milan ushawahi kutumiwa na bado unatumiwa na vigogo viwili nchini
Italy yani Intermilan na Ac Milan.

Vigogo ambavyo vinahistoria kubwa katika soka la Italy pamoja na
duniani kwa ujumla.

Vigogo ambavyo ndivyo vina mafanikio makubwa katika soka la Italy,
vikiwa vimechukua Seria A mara 18 kila mmoja.

Historia hiyo hiyo inaniambia Ac Milan ndiyo timu ya nne kwa mafanikio
makubwa duniani. Ikiwa ndiyo timu pekee ya Italy yenye mafanikio
makubwa katika michuano ya kimataifa.

Intermilan ikiwa imechukua UEFA 3 na Ac Milan ikiwa imechukua UEFA 5.

Hayo yote yalitokea kipindi cha nyuma, kipindi ambacho hizi timu
zilikuwa katika kiwango bora.

Kiwango ambacho kiliifanya mechi ya Intermilan na Ac Milan kuwa derby
inayofuatiliwa zaidi duniani.

Mambo mengi yamebadirika, tena yamebadirika kutokana na upepo mbaya
kupita katika timu hizi.

Ukame wa makombe umeingia katika nyumba hizi mbili za Kifalme nchini Italy.

Hakuna tena kombe kubwa ambalo linaingia kwenye uwanja wa San Siro
tangu msimu wa mwaka 2009/2010 ambapo Intermilan ilifanikiwa kuleta
makombe mawili makubwa katika uwanja wa San Siro ( Seria A na UEFA).

Hii ndiyo ilikuwa mara ya mwisho uwanja huu wa San Siro ukishuhudia
unapokea kombe kubwa.

Anguko kubwa la uchumi katika kuanzia miaka 2010 ndilo ambalo lilikuja
kuangusha kila kitu.

Ufalme wa Intermilan na Ac Milan ulianguka vibaya baada ya uchumi wa
Italy kuanguka na kufanya timu nyingi zipoteze dira.

Wakati wa kumiliki wachezaji wakubwa ukawa umeishia pale.

Mvuto wa derby hii ukaanza kuporomoka kwa kasi kuanzia ndani ya uwanja
mpaka nje ya uwanja.

Hakukuwa na mechi ya ushindani tena ndani ya uwanja kati ya Intermilan
na Ac Milan.

Vikosi vya timu zote vilikuwa vyepesi, kiasi ambacho vilikuwa haviwezi
kutoa upinzani wa kweli kama kipindi cha nyuma.

Kipindi ambacho kila mtu alikuwa radhi kuacha usingizi wake kwenda
kuwashuhudia kina Paolo Maldini.

Kipindi ambacho lazima ujutie kama ulikosa kuangalia mechi hii, roho
ilikuwa inauma kama ulikosa kushuhudia Ronaldo De Lima akisumbuana na
mabeki wa Ac Milan.

Chozi lazima likutoke kama ulishindwa kumwangalia Nesta katika mechi
hii, ilikuwa furaha kushuhudia beki wa kiwango cha dunia akitoa jasho
la damu kuhakikisha Intermilan hapati ushindi.

Wakati unashuhudia Nesta akiwakaba kwa ustadi washambuliaji wa
Intermilan ndiyo wakati ambalo unamuona Inzanghi akiwa anaibia na
kufunga goli ambalo linaamsha dunia nzima kwa kushangilia.

Wakati huo pia watu wakimsubiri Vieri afunge goli ambalo litawaacha
midomo wazi na kubaki kujiuliza huyu katokea sayari gani?

Kuna mabeki visiki ambao walikuwa wamekamirika kila idara. Utaanzaje
kumpita Materazzi kiwepesi na yeye akuchekee?

Utaanzaje kutofurahia kiwango cha Laurent Blanc huku Ac Milan wakiwa
na Seedorf katikati akipika kila aina ya chakula kitamu .

Ubabe ,ukorofi na uwezo wa kukaba ulikuwa unavutia sana pindi
unapomuona Gattuso.

Mtu ambaye alikuwa mfupi, lakini alikuwa na uwezo wa kupambana na mtu
yoyote haijalishi alikuwa anamzidi urefu, kwake yeye aliona wanaendana
na ikizingatia alikuwa ameshiba kweli kweli kama Zlatan Ibrahimovich.

Mshambuliaji mwenye jeuri, kejeli na uwezo mkubwa uwanjani.
Mshambuliaji ambaye kila kocha alijivunia kuwa naye.

Mshambuliajia ambaye alikuwa akiweka ufalme sehemu yoyote ile ambayo
alikuwa anaenda.

Ndiyo maana ni mfalme wa San Siro kwa sababu ashawahi kucheza vilabu
vyote hivi viwili kwa mafanikio makubwa yani (Intermilan na Ac Milan)

Kipindi hicho kila mchezaji alikuwa anajua thamani ya jezi ya
Intermilan na Ac Milan

Ndiyo maana walicheza kwa kujituma kuipigania jezi za vilabu hivi.

Hali tayari imeshabadirika ambapo timu zote zinapitia katika vipindi vya mpito.

Vipindi ambavyo hakuna klabu inafanya vizuri katika ligi ya ndani au
ligi ya nje.

Mafanikio yao yameporomoka kwa kiasi kikubwa sana.

Kitu ambacho kila zikikutana sasa hivi hakuna msisimko tena kama kipindi kile.

Mtu hawezi kuumia tena kuikosa mechi ya Intermilan na Ac Milan kama
kipindi kile.

Kwa sababu ufundi umepungua, ushindani umepungua, burudani pia
imepungua kila kitu kinaganyika katika hali ya ukawaida.

Namba ya watazamaji wa hii mechi duniani imepungua kwa kiasi kikubwa sana.

Ule msisimko wa hii derby umebaki kwenye vitabu vya historia tu na
siyo uwanjani tena.

Martin Kiyumbi

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

UCHAMBUZI WA BAADHI YA MECHI ZA LIGI KUU YA ENGLAND

Tanzania Sports

LIGI KUU BARA (VPL) USHINDANI KILA KONA