Manchester City kwa mara ya kwanza kwenye historia yao wamefuzu kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya. Shukrani kwa bao la Kevin De Bruyne kwenye mchezo wa jana dhidi ya PSG.
Bao hilo alilofunga kwa ufundi nje ya eneo la hatari mnamo dakika ya 76 lilimaanisha kuwa PSG walihitaji mabao mawili au zaidi kwenye dakika zilizokuwa zimesalia ili waweze kusonga mbele. Maajabu ya De Bruyne yalishawaua PSG.
Mchezo wa jana ni mmoja kati ya michezo ambayo De Bruyne amedhihirisha kiwango chake cha hali ya juu. Ukiacha bao safi alilofunga, yeye ndiye mchezaji aliyetengeneza nafasi nyingi zaidi kwenye mchezo huo. Alitengeneza nafasi nne.
Ukiacha mchezo huo wa jana wa marudiano, De Bruyne aling’ara pia kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Paris ndani ya dimba la Parc des Princes wiki iliyopita. Aliifungia City bao safi la kuongoza akimalizia kazi ya Fernandinho.
Uwezo wake wa kukokota mpira, kupiga pasi, kutengeneza nafasi, kupiga mashuti ya mbali na kumalizia nafasi za kufunga unamfanya awe mmoja kati ya viungo washambuliaji hatari kwa sasa Ulaya.
Hata takwimu zake kwenye Ligi Kuu ya England msimu huu zinaonesha wazi namna alivyo kwenye kiwango cha juu. Akiwa ameanza kwenye michezo 18 pekee amefunga mabao 6 na kutengeneza 9.
Nyota huyo wa miaka 24, raia wa Ubelgiji kwa sasa yupo kwenye kiwango ambacho kinaweza kumfanya kocha wa klabu yoyote kubwa ya Ulaya kutamani kuwa naye kwenye kikosi chake.
Amezua maswali mengi hivi karibuni kutokana na kiwango anachoonesha. Washabiki, waandishi na wachambuzi wa soka wanajiuliza ilikuwaje kocha mahiri kama Jose Mourinho akashindwa kutambua uwezo alio nao na kuamua kumuuza.
Kiasi cha paundi milioni 18 pekee kilimng’oa kutoka kwenye Chelsea ya Mourinho na akajiunga na Wolfsburg Januari 2014. Wolfsburg walikuwa wamelamba dume.
Walifaidika mno na kiwango cha ajabu alichokionesha De Bruyne akiwa nao kwenye msimu uliopita wa Bundesliga. Mchango wa De Bruyne uliwarejesha kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kukosekana kwa misimu mitano.
De Bruyne alimaliza msimu wake huo wa Bundesliga akiwa na mabao 10. Alitengeneza mengine 21 na kuweka rekodi kwa kuwa hakuna aliyewahi kupika idadi hiyo ya mabao kwenye msimu mmoja wa Bundesliga.
Alikamata nafasi ya pili kwenye orodha ya wachezaji waliotengeneza nafasi nyingi zaidi ndani ya ligi tano kubwa za Ulaya kwenye msimu wa 2014/15. Alitengeneza nafasi 112 nyuma ya Dimitri Payet aliyetengeneza nafasi 135 akiwa na Marseille.
Kiwango chake kikawavutia Manchester City ambao Agosti 30 mwaka jana walitangaza kumsajiili kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 55. Hizo ni sawa na takribani shilingi bilioni 171 za Tanzania.
Dau hilo likamuweka kwenye nafasi ya pili kwenye orodha ya wachezaji walisajiliwa kwa pesa nyingi zaidi na klabu za England akiwa nyuma ya Angel Di Maria aliyesajiliwa na Manchester United kwa paundi milioni 59.7 Agosti 2014.
Bilioni 171 walizotoa Manchester City kumsajili De Bruyne zimezaa matunda. Kiungo huyo ametoa mchango mkubwa kuipeleka Manchester City kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu huu.
Akibaki kwenye kiwango hiki alicho nacho sasa, bila shaka Manchester City watakuwa moja kati ya timu tishio za Ulaya hivi karibuni. Kevin De Bruyne ni wa thamani ya ile shilingi bilioni 171.