in , , ,

LIGI YA MABINGWA ULAYA:

Manuel Pellegrini na Kevin De Bruyne

*Man City nusu fainali

*Real Madrid wawapiga Wolfsburg

Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) imefika patamu, baada ya Manchester City
kufanikiwa kuwatupa nje Paris Saint-Germain (PSG) huku Real Madrid
wakiwanyamazisha Wolfsburg na kutinga nusu fainali.

City waliokwenda sare ya 2-2 kwenye mechi ya awali, walifanikiwa
kuingia nusu fainali, ikiwa ni mara yao ya kwanza, na kuelekea
kutimiza ndoto ya wamiliki kutaka kuona waking’aa Ulaya, na hii ni
fahari kubwa kwa kocha anayeondoka, Manuel Pellegrini.

Kiungo aliyetoka kwenye majeraha hivi karibuni, Kevin de Bruyne ndiye
alifunga bao hilo dakika ya 76, ambapo kwa ujumla mechi ilionekana
timu kutoshana nguvu, japokuwa PSG walitawala zaidi mchezo. Manchester
walikosa penati kipindi cha kwanza, ikiwa imepigwa na Sergio Aguero.

Kipa wa wenyeji, City, Joe Hart alicheza vyema na kuokoa mabao matatu
ya wazi yaliyokuwa yatiwe kimiani na mshambuliaji matata, Zlatan
Ibrahimovic. Wakishangiliwa na umati wa washabiki karibu 50,000, City
walijitahidi kupenya ngome ya wapinzani wao lakini bao la De Bruyne
lilikuwa ndio mkwaju pekee uliolenga lango.

City ndio timu pekee ya Uingereza iliyobaki kwenye michuano hiyo na
wanaweza sasa kuota kwenda kwenye fainali zitakazofanyika jijini
Milan, Italia. Pellegrini anayeondoka kumpisha Pep Guardiola hapo
Etihad, alisema anaamini wanaweza kutwaa kombe hilo.

PSG tayari wameshatwaa ubingwa wa Ligue 1 ya Ufaransa, na wameacha
pengo la pointi 28 dhidi ya wapinzani wanaowafuata huko, hivyo sasa
wanasubiri michuano ya UCL mwaka kesho, kwani kwa sasa ni kwa heri.

REAL MADRID WAWATOLEA UVIVU WOLFSBURG

Cristiano Ronaldo celebrates scoring his, and Real Madrid’s third goal
Cristiano Ronaldo celebrates scoring his, and Real Madrid’s third goal

Real Madrid wamefanya kile kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu na
washabiki wao, kwa kuwakandika Wolfsburg 3-0, wakipindua matokeo ya
mechi ya mkondo wa kwanza, ambapo Wajerumani hao waliwachapa 2-0.

Wakicheza nyumbani Santiago Bernabeu, Madrid waliingia wakiwa na lengo
moja, tena baada ya kuwa wameaswa na nyota wao, Cristiano Ronaldo kuwa
makini na kamili ili kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa huo wa
Ulaya.

Alikuwa Ronaldo aliyefunga mabao yote matatu, akianza dakika ya 15, ya
17 na kumalizia hat-trick yake katika dakika ya 77. Wolfsburg
waliwasili katika mji mkuu wa Hispania wakijivunia uongozi wa mabao
hayo mawili, lakini wakajikuta mabao yamesawazishwa katika sekunde 86
tu za kwanza, wakabaki sasa kupigania bao la ushindi.

Ilikuwa faraja kwa kocha Zinedine Zidane ambaye majuzi alifanikiwa
kuwafunga Barcelona kwao Camp Nou, huku akitaka kuendeleza rekodi ya
utwaaji wa kombe hilo, ikizingatiwa kwamba tayari wameshalitwaa mara
10 – La Decima. Zidane alichukua nafasi ya Rafa Benitez na kabla ya
hapo alikuwa msaidizi wake.

Ronaldo sasa amefikisha mabao 93 katika UCL kutokana na mechi 125
alizocheza, akiwa ni kinara na anamzidi hasimu wake, Lionel Messi kwa
mabao 10. Mara mbili nahodha wa Madrid, Sergio Ramos aligonga mtambaa
wa panya wakati Jese aliyeingia kipindi cha pili nusura atikise nyavu
kama si kipa Diego Benaglio kufanya kazi ya ziada.

Real wanaungana na Man City kisha an mshindi baina ya Atletico Madrid
na Barcelona kisha mshindi baina ya Benfica na Bayern Munich katika
droo itakayochezeshwa Ijumaa hii kujua nani atachuana na yupi kwenye
nusu fainali hizo.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Ranieri: Ubingwa Leicester bado

Tanzania Sports

DE BRUYNE ANA THAMANI YA ILE BILIONI 171