in

Chelsea ni wasafi, Man City ni mtu wa ziada

Chelsea Na Man City

FAINALI UEFA

VILABU viwili vya Uingereza vitakutana kwenye mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mnamo Meim29 mwaka huu. Ni Chelsea inayonolewa na Thomas Tuchel na Man City inayonolewa na Pep Guardiola. Timu hizo zimekutana katika mchezo wa Ligi Kuu Uingereza siku chache zilizopita, ambapo Chelsea waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Pengine mchezo huo haukuwa muhimu sana kwa Pep Guardiola kwa sababu aliuwa anaongoza Ligi kwa tofauti ya pointi 10 dhidi ya washindani wake Manchester United. Lakini ulikuwa mchezo wa kupimana ubavu wa kimbinu baina ya makocha hao.

CHELSEA WASAFI

Unapowatazama Chelsea wakimiliki mpira hakika wanafurahisha. Siri yao ni kwamba, kwanza wanacheza kwa uangalifu na wana makosa machache sana. Ni timu inayocheza bila kufanya makosa, lakini hilo halina maana hawawezi kufanya.

Katika mechi mbili za nusu fainali dhidi ya Real Madrid walicheza kwa umakini na uangalifu mkubwa pasipo kufanya makosa binafsi au kitimu. Nhata hivyo wamekuja kufanya makosa kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Arsenal, hivyo ndivyo soka lilivyo mchezo wa makosa na kuambulia kipigo cha 1-0.

Pili, Chelsea wanacheza katika njia ya kocha wao Thomas Tuchel, kwamba ili waweze kucheza vizuri kwa mbinu zake wanahitaji wachezaji wenye kasi,wabunifu na wenye uwezo wa kuibeba  timu inaposhambuliwa.

Wachezaji wake kama Kai Hudson-Odoi, Pulisic, ni aina ya wale wanaocheza kibunifu zaidi. Kasi yao dhidi ya wapinzani ni tishio tosha. Wao Chelsea wanaweza kucheza mashambulizi ya kushtukiza kwa kasi,kumiliki mpira na kuliacha eneo la ushambuliaji (nambari 9) likiwa tupu kwa maana wanagawana namna ya kusimama katika eneo hilo.

Michezo yao dhidi ya Real Madrid walitumia mbinu hiyo, na kuwafanya wachezaji wao kulikaribia lango bila kutegemea mmaliziaji (namba tisa). Mfumo  wa 4-4-2 unawafanya wacheze katika ‘highline’ ambako mipira mingi hupitia pembeni kulia na kushoto kuingia katikati na kutoka kwenda pembeni tena.

Mbio za Ngolo Kante na Mount mara nyingi zinakuwa pembeni kulia na kushoto wakijaribu kuingia katikati, lakini mabao yao huwa yanapata mfungaji ambaye anatokea pembeni kufuata mpira (kupokea pasi ya kufunga akitokea nje ya eneo la hatari).

Tanzania Sports
Chelsea Na Man City

Faida waliyonayo ni kwamba eneo lao la kiungo wa ulinzi linachezwa na watu wawili wenye majukumu tofauti. Jorginho huwa anashughulika kuzima mipango ya timu pinzani, wakati Kante anakuwa mtu wa kuwasukuma wapinzani kurudi lango mwao kujilinda huku akiwa na kazi nyingine ya kupika pasi za mabao kwenda pembeni au kulia.

Katika eneo la nambari hawashughuliki nalo. Unapokuwa na winga mwenye kasi kama Hudson-Odoi au Mason Mount maana yake watakuwa wanafanya kazi ya kuwarudisha mabeki wa pemheni wa timu pinzani ili kuhami lango lao.

Tatizo la Chelsea ni kwamba hawana mabeki wa pembeni wenye ufundi kama ule wenzao wa Man City wa Zinchenko au Kyler Walker ambao ni silaha zao za kwanza katika kutengeneza ushindi.

Changamoto nyingine ni namna gani Chelsea wanaweza kuhimili kishindo cha timu ambayo inaweza kuwasambaratisha eneo la kiungo na kuwabakiza viungo wao nyuma tu. Pili namna gani wanaweza kuhimili presha ya mawinga wakali ambao watawabakiza nyumba mabeki wa pembeni kulia na kushoto.

Tanzania Sports
Estadio do Dragao

Ni namna gani wanamudu kukabiliana na nambari tisa mwenye kasi,nguvu na maarifa kama walivyokuwa zama za Didier Grogba. Chelsea hii kama pakipatikana mshambuliaji mwenye mabavu na kuwashughulisha mabeki wao wa kati Thiago Silva na Antonio Rudiger, nini kitatokea? Je watakuwa na uhuru uleule kama ulivyozoeleka? Vipi kasi za  Bernardo Silva na Riaz Mahrez watamudu kweli?

Kwenye mchezo dhidi ya Man City nimemwona Pep Guardiola akijaribu kutumia mbinu za mabeki watano kisha akawaelekeza washambuliaji wake wawe wanakaba kwa 1-3.

Nambari 9 alikuwa anaongoza kusimama nje ya 18 ya lango la Chelsea, huku nyuma yake akisaidiwa na wachezaji watatu. Nao wachezaji watatu hao walikuwa wakilindwa na Ikaly Gundogan, yaani kiungo mshambuliaji.

Tatizo la Man City hakuna mshambuliaji tishio mwenye mabavu. Sioni kitisho cha nambari 9 wa Man City wa sasa sababu Gabriel Jesus na Sergio Aguero hawana kile ambacho washambuliaji kamili wa kati wanatakiwa kuwa navyo.

Pep Guardiola na Thomas Tuchel hawana mshambuliaji mwenye mabavu kama Richarlson wa Everton au wa aina yake ambaye anatakiwa kuwashughulisha mabeki dakika zote za mchezo, yaani ni kama wasemavyo mashabiki wa soka “mshambuliaji wa kukichafua”

MTU WA ZIADA

Fainali ya UEFA inahitaji zaidi ya kucheza kitimu. Fainali inahitaji aina ya wachezaji ambao wanakupa kitu bora zaidi ya timu. Chukulia mfano bao la Karim Benzema dhidi ya Liverpool, miaka kadhaa iliyopita. Chukulia mabao ya Gareth Bale dhidi ya Liverpool.

Chukulia ushindi wa Liverpool dhidi ya Tottenham Hotspurs, ambapo Liverpool walipata penalti ambayo iliwapa bao la ushindi lakini ukiangalia uchezaji wa kitimu Spurs walikuwa bora uwanjani, lakini walikosa wachezaji wanaoamua mechi. Liverpool walikuwa na mtu wa ziada Divock Origi alikichafua dhidi ya Barcelona misimu kadhaa iliyopita.

Watazame Bayern Munich walikuwa wanatamba kwa kufunga mabao mengi lakini siku ya fainali ya UEFA msimu uliopita walipata bao moja tu, ikiwa na maana uamuzi wa kushinda mchezo ulihitaji akili ya mchezaji mmoja au aina ya wachezaji ambao wanakupa kitu cha ziada yaani juu ya uchezaji wa kitimu.

Tuchel ana Olivier Giroud, halafu Pep ana Gabriel Jesus, hawa hawawezi kuwapa kitu cha ziada nje ya uchezaji wa kitimu. Ni washambuliaji kwa asili lakini si wale ambao wana kaliba ya “kukichafua uwanjani”.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Mbappe

Nini kitatokea kwa Kylian Mbappe?

Baadhi ya wachambuzi wa Michezo

MALIPO :UCHAMBUZI WA MICHEZO NI WAJIBU