in

Nini kitatokea kwa Kylian Mbappe?

Mbappe

NDOTO za mwanasoka chipukizi mahiri Kylian Mbappe kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya zimeyuka msimu huu. Hili ni jaribio la pili kwa ngazi ya juu ya mashindano ya ngazi ya klabu. Awali PSG haikufua dafu kwenye mashindano hayo, hali ambayo ilizua minong’ono kuwa nyota huyo angeondoka klabuni hapo.

Hata hivyo msimu uliopita  2019/2020 Mbappe alifanikiwa kuifikisha PSG hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Katika mchezo wa fainali walichapwa bao 1-0 na Bayern Munich. Kipindi hicho PSG walikuwa chini ya kocha Thomas Tuchel, ambaye desemba mwaka 2020 alifutwa kazi baada ya kutofautiana na mkurugenzi wake Leonardo raia wa Brazil.

Ilidhaniwa kuwa Mbappe angeondoka klabuni hapo kuelekea kwa miamba ya Hispania, Real Madrid, Barelona au Liverpool ya Uingereza. Mbappe alihusishwa na vilabu mbalimbalo barani Ulaya, lakini aliamua kubaki PSG ikiwa ni njia ya kutaka kutimiza ndoto za ktwaa taji la Ligi ya Mabingwa akiwa jijini Paris nchini Ufaransa.

Ili kutimiza ndoto hiyo, Mbappe alianza kulalamikia majukumu hafifu anayopewa katika kikosi cha PSG. Kwamba angependa kuongoza safu ya mshambulizi ambayo ilikuwa chini ya Edinson Cavani na Mauro Icardi. Hata hivyo PSG ikaamua kutemana na Cavani ili kumwezesha Mbappe kubeba majukumu makubwa kikosini.

Msimu wa 2020/2021 PSG imekuwa na kiwango bora, huku ikukumbukwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya miamba ya Hispania Barcelona ndani ya dimba la Camp Nou. Ushindi wa PSG ndani ya Camp Nou ulikuwa muhimu kuelekea ndoto za kinda huyo, huku Wacatalunya hao wakimtazama kama mbadala wa Lionel Messi.

Nguvu na akili zilizoelekezwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu huu ziliishia miguuni mwa Manchester City ya Pep Guardiola. PSG ikiwa imeongoza kwa bao 1-0 kwa muda mrefu kwenye uwanja wa nyumbani ilijikuta ikiruhusu mabao mawili ya haraka yaliyofungwa na Man City hivyo kumaliza dakika 90 kwa kunyukwa mabao 2-1. Katika mchezo wa marudiano jijini Manchester miamba hiyo ya Ufaransa ilinyukwa mabao 2-0.

Hapo ndipo safari ya ndoto za Mbappe iliishia. Minong;ono ilianza tena huku akihusishwa na klabu zilezile. Hata hivyo Real Madrid wanaonekana kupewa kipaumbele zaidi kumnyakua staa huyo wa Kifaransa ingawa gharama za usajili zinatajwa kuwa kubwa na huenda zikawa kikwazo cha Madrid kumsajili.

Wiki hii imeibuka habari nyingine ambayo imeibua minong’ono juu ya hatima ya Mbappe ndani ya PSG. Nyota mwenzake raia wa Brazil Neymar Junior amesaini mkataba mpya utakaomweka klabuni hapo hadi mwaka 2025.

Mkataba wa Neymar una maana kubwa kwa Mbappe, kwamba anatakiwa kufanya uamuzi juu ya mustakabali wake kubaki kikosini PSG au kuondoka.

Neymar amemaliza minong’ono kuhusu hatima yake ya baadaye ambapo naye alidaiwa kuwa angelihama timu hiyo baada ya kushindwa kuipatia taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kulikuwa na habari nyingi zilizomhusisha Neymar kurejea Barcelona lakini sasa imedhihirika kuwa hatoondoka PSG.

Sasa habari zinageuka kwenda kwa Mbappe ambaye ni nyota mwenzake kikosini PSG na wameifanya timu hiyo kuwa kivutio kikubwa kwenye kandanda. Mkataba wa Mbappe unamalizika Juni 2022, huku mkurugenzi ake Leonardo na uongozi wa klabu ya PSG wameweka mezani ofay a kumbakiza nyota huyo, lakini Mbappe anaonekana kuwa mtulivu kwa kutopaparikia mkataba mpya.

Mbappe hapendi kuzungumzia suala la mkataba mpya na uamuzi alionao, ingawa ameshindwa kuzuia habari zinazomhusisha kujiunga Real Madrid ambako angejiunga mara baada ya kutoka Monaco. Hakuna siri kwamba Los Blancos wanatamani kumsajili nyota huyo, lakini itategemea zaidi iwapo Zinedine Zidane ataendelea kukinoa kikosi cha Real Madrid au la.

Hadi sasa sababu kadhaa za Mbappe kubaki PSG zimeelezwa, kwamba anatamani kuona mipango ya timu hiyo kabla ya kuchukua uamuzi wa kubaki au kuondoka. Mbappe ana kiu kubwa ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa kuliko kitu kingine chochote, na anaamini litakuwa jambo zuri ikiwa atachukua akiwa PSG.

Hatua ya real Madrid kuwa mwanzilishi wa European Super League ni dalili ya namna hali ya fedha ilivyo klabuni hapo, kwahiyo huenda ikamfanya asubiri hadi kumalizika mkataba wake PSG ndipo aondoka akiwa mchezaji huru kwani dau la usajili huenda likawa kikwazo kwenda Santiago Bernabeu.

Baada ya kutawala soka la Ufaransa ambalo halina nafasi kubwa Ulaya, PSG imeamua kusaka ubabe katika Ligi ya Mabingwa, ambapo klabu hiyo imefika wakati sasa inahofiwa na wapinzani wao. Real Madrid imekuwa timu isiyoogopwa kwa sasa, na inaonekana inajijenga upya kwa kusajil damu change baada ya kikosi cha dhahabu kufikia ukomo wa uwezo.

Uamuzi wa Neymar kubaki PSG huenda ukatoa mchango mkubwa katika mkataba wa Mbappe kumshawishi kuendelea kukipiga klabuni hapo kwa lengo la kufanya jaribio lingine la kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa katika jiji alilokulia la Paris. Nini kitatokea? Hilo ndilo linalosubiriwa sasa na baadaye.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Simba vs Yanga

Maswali magumu kuahirishwa mechi Simba vs Yanga

Chelsea Na Man City

Chelsea ni wasafi, Man City ni mtu wa ziada