in

Mzuka wa ‘Kazelona’ wa Yanga ulivyozimwa

cedric kaze

Cedric Kaze ameondolewa katika benchi la ufundi la vinara wa Ligi Kuu Tanzania, Yanga. Mabingwa hao wa kihistoria wameshindwa kuvumilia matokeo mechi mbili za mwishoni. Michezo ambayo imehitimisha kibarua cha Cedric Kaze ni dhidi ya Coastal Union ya Tanga ambako Yanga walilazwa mabao 2-1, pamoja na sare ya 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania.

Tanzaniasports inafahamu kuwa kabla ya kuondolewa kocha huyo kulikuwa na kikao kizito ndani ya uongozi wa Yanga ambako inadaiwa hoja ya mwenendo wa timu na nafasi ya kocha Cedric Kaze zilijadiliwa kwa kina. Aidha baadhi ya taarifa zinaeleza kuwa kulikuwa na mechi maalumu zimetengwa ili kutoa tathmini kama waendelee naye au mkataba uvunjwe. Makala haya yaelezea mambo kadhaa ya kusisimua ya Cedric Kaze.

‘KAZELONA’

Hili ni jina la utani ambalo limekuwa likitumiwa na mashabiki wa soka nchini Tanzania wakiwa na maana kuwa kocha huyo angeleta soko la kusisimua kama la Barcelona ya Hispania. Barcelona wanafahamika kuwa na vijana mahiri katika akademi yao. Kaze ni mwalimu wa soka aliyenoa tiu mbalimbali nchini Burundi pamoja na vijana wa Barcelona huko nchini Canada. Yanga waliahidiwa kucheza soka kama la Barcelona na ndipo linaibuka jina la Kazelona.

‘HAKUTAKA UBINGWA’

Tanzania Sports
Usajili mzuri wa Yanga

Tangu siku ya kwanza aliyopewa jukumu la kuinoa Yanga, Cedric Kaze alikataa kuahidi kuwa atatwaa ubingwa msimu huu. Kaze aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano wake wa kwanza na kusisitiza kuwa anataka kuona Yanga ikicheza soka safi kama Barcelona. Kwa Kaze suala la burudani kwa mashabiki kilikuwa kitu cha kwanza na muhimu zaidi kuelekea ushindi wa timu yake. 

AMEINYANYASA SIMBA

Kaze katika kipindi chake cha ukocha Yanga amekutana na watani wa jadi wa timu hiyo Simba mara mbili. Katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kazealiwaongoza vijana wake dhidi ya Simba na kupata bao la mapema. Lakini mabingwa watetezi Simba walisawazisha hivyo mchezo kumalizika kwa 1-1. Katka mchezo huo Simba walitawaliwa kwa kiasi kikubwa. 

Kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, Cedric Kaze aliwafunga Simba kwa njia ya matuta na kuipa ubingwa vijana wa Jangwani na Twiga. Kwahiyo Kaze hajawahi kufungwa na Simba bali ameinyanyasa Simba katika michezo mwili aliyokutana nayo.

TAKWIMU

Kuanzia Desemba 31 mwaka 2019 takwimu za Cedric Kaze zinajieleza bayana, ambako alipambana na Tanzania Prisons mkoani Rukwa na kutoka sare 1-1. Febryari 13 aliwaongoza Yanga kukutana na Mbeya City ambako walitoka sare 1-1 mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine. 

Februari 17 Cedric Kaze aliwaongoza vijana wake kupambana na Kagera Sugar ya mkoani Kagera kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa na kutoka sare 3-3. Februari 20 Yanga walikutana na Mtibwa Sugar jijini Dar es salaam ambako waliibugiza miamba hiyo ya Turiani 1-0 lililofungwa na Calinhos.

Machi 4 mwaka huu Kaze aliwaongoza vijana wake kwenye uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga ambako walifungwa mabao 2-1 na Coastal Union.

Polisi Tanzania waliwaalika Yanga mnamo Machi 7 mwaka huu jijini Arusha ambako matokeo yalikuwa 1-1. Baada ya mchezo huo ndipo uongozi wa Yanga ulitangaza kumfuta kazi Cedric Kaze na benchi lote la ufundi.

KAZE WA KILELENI

Cedric Kaze anakuwa kocha wa pili kufukuzwa Yanga baada ya kuondolewa Zlatko Krompotic ambaye alikuja kuchukua nafasi ya Luc Aymael. Makocha wazawa waliokaimu nafasi hizo ni Charles Mkwassa na Juma Mwambusi. Kaze anaondoka Yanga akiiacha ikiwa kileleni mwa Ligi Kuu tanzania Bara. Ameondolewa huku timu ikiwa imepata pointi 50 na kufungwa mchezo mmoja pekee kati ya mechi 23 walizocheza. 

Amecheza mechi 18 za Ligi Kuu. Ameshinda michezo 10, ametoka sare michezo 7 na kufungwa mchezo mmoja.

MIEZI 6,WACHEZAJI WAWILI

Kaze katika kibarua chake amedumu kwa miezi 6 Yanga na kusajili wacheaji wawili Saido Ntibazonkiza na Fiston Abdul Razack wote raia wa Burundi. Hata hivyo Yanga ni timu ya ajabu ambayo ilisajili wachezaji zaidi ya 20 kwa msimu mmoja. Hii ni sawa na kusema Cedric Kaze ametumia wachezaji ambao hakuwaasajili.

ALIKATAA OFA YA SIMBA

Kaze amewahi kuwa na mazungumzo na klabu ya Simba wakati ikinolewa na kocha Dylan Kerry mwaka 2015. Simba walitaka Cedric Kaze awe kocha msaidizi wa Dylan Kerry lakini kwa maneno yake mwenyewe Kaze alisema hakutaka kuwa msaidizi wa yeyote. inaelezwa huo ndio ulikuwa wakati ambao Simba waliamua kumchukua Jackson Mayanja kuwa kocha msaidizi wa Kerry. Pia mwaka 2017 wakati Simba walipomfukuza Patrick Aussems kulikuwa na mazungumzo kati ya Simba na Kaze, lakini hayakuwa na mafanikio.

DHAHABU YA BURUNDI

Kaze anakuwa miongoni mwa makocha wa Burundi ambao wametokea kuwa lulu nchini. Kwa miaka hivi karibuni kumekuwa na wimbi la makocha kutoka Burundi, Ettiene Ndayiragije (Mbao FC,KMC, Azam FC na Taifa Stars).

Masoud Djuma Irambonaimana (Simba), Hitimana Theiry (Stand United,KMC,Namungo F.C na Mtibwa Sugar. Haruna Harerimana yeye alikuwa kocha wa Mwadui FC na baadaye Lipuli F.C. Ramadhani Swazurimo (Mbeya City na Singida United). 

Bahati Vivier (Kocha msaidizi wa Azam). Aliyekuwa kocha wa makipa wa Yanga, Vladimir  Niyonkuru ni raia wa Burundi. Kaze amewakilisha kizazi cha dhahabu cha Burundi kwenye ukocha.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
SIMBA SC

Simba wanatangaza ‘utamu’ wa Ligi Kuu Tanzania

Marco Rose

Borussia Dortmund mikononi mwa Marco Rose