*Beki Arsenal hali mbaya

*Walala kwa Spurs kwa mabao yanayozuilika

*Tetesi za klabu kuuzwa £ bil. 1.5 zapingwa

 

Kama kuna kitu kilichowaudhi washabiki wa Arsenal Jumapili hii, ni kuzubaa kwa mabeki wao.

Kutojituma ipasavyo katika baadhi ya vipindi vya dakika 90 za mchezo, ndiko kunakoigharimu timu, na sasa ni wazi wanahitaji ukuta mpya.

Hakuna suluhu nyingine kuhusu ukuta anaouamini Arsene Wenger waliocheza dhidi ya Tottenham Hotspurs na kukubali kufungwa mabao mawili yanayoepukika ndani ya dakika mbili.

Pamoja na Per Mertesacker kusahihisha makosa ya jumla ya beki yao kwa kufunga bao moja zuri la kichwa mbele ya Gareth Bale wa Spurs, bado kuna safari ndefu.

Arsenal crest
Arsenal crest (Photo credit: Wikipedia)

Umekuwa msimu mchungu na mwaka ambao wachezaji wameishia kuvunja rekodi nzuri za waliowatangulia kwa kufungwa hata katika michezo ya kihistoria ambayo Arsenal imekuwa ikisimama dede.

Na sasa shinikizo dhidi ya Wenger litarudia tena, baada ya kuwa limepozwa kwa ushindi mwembamba wa mechi iliyopita dhidi ya Aston Villa.

Athari kubwa za matokeo haya kisaikolojia ni kwamba yanaiweka pabaya Arsenal katika kufuzu kwa mashindano ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.

Pamoja na kwamba wamebaki nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi, wametupwa mbali na wenzao hao.

Wakati Arsenal wana pointi 47, Spurs wamewaacha kwa pointi saba kwani wanazo 54.

Arsenal wanawafuata nyuma Chelsea, lakini napo kuna umbali wa pointi tano, ikimaanisha wanatakiwa kushinda mechi mbili na Chelsea wapoteze zao, ili kurudi kwenye eneo la nne bora walilozoea kwa miaka kadhaa.

Juu zaidi yao ni Manchester City waliofikisha pointi 56 licha ya kucheza mechi moja pungufu yao na wengine wanaohitaji muujiza kuwafikia ni Manchester United wenye pointi 71.

Wakati wakiwa kwenye ukingo wa kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu kwa kufungwa mabao 3-1 Emirates na Bayern Munich, Arsenal wanaelekea kupoteza heshima yao.

Walau ikiwa Ulaya hawatambi, walitarajiwa wang’are England, kwa vile ni timu kubwa yenye mapato mengi, lakini kana kwamba hatoshi kushuka hadhi Ulaya, hata London Kaskazini nako wamepoteza nguvu yao kwa Spurs.

Mjumuisho wa yote hayo ulimwacha kocha wa Spurs, Andre Villas-Boas aliyefukuzwa na Chelsea mwaka jana akichekelea, huku Arsenal wakiomba tetesi zilizokanushwa za matajiri wa Uarabuni kutaka kuinunua klabu kwa pauni bilioni 1.5 ziwe za kweli.

Pamoja na mambo mengine, wanunuzi hao tarajali kutoka Mashariki ya Kati walinukuliwa na gazeti wakisema kwamba ungekuwa mwisho wa wachezaji nyota kuuzwa.

Kwamba kingetolewa kitita kikubwa kwa ajili ya kununua wachezaji wazuri na kupunguza bei ya tiketi za kuingilia mpirani, ambapo zile za Arsenal ni kati ya aghali zaidi kwenye ligi kuu.

Arsenal imetangaza kwamba mwenye hisa nyingi zaidi Arsenal, Mmarekani Stan Kroenke amejizatiti kubaki na klabu hiyo kwa muda mrefu, hana mpango wa kuuza hisa zake, lakini pia hakuna ombi lolote walilopata la kuuza klabu.

Wenger na bodi wamekuwa wakilaumiwa kwa kuachia wachezaji nyota kuondoka bila kununua wengine.

Ilikuwa kama mshangao, pale klabu kama Queen Park Rangers (QPR) ilipotumia mamilioni ya pauni kununua wachezaji wa kimataifa kabla ya msimu huu kuanza, akiwamo golikipa wa kimataifa wa Brazil, Julio Cesar na Januari mwaka huu walimchukua beki mahiri, Christopher Samba.

Washabiki wanajiuliza kulikoni Arsenal imebaki na mabeki wa kuokoteza, wanaojituma uwanjani na mara wanakatika na kuruhusu mabao ya kizembe kama Jumapili hii, hivyo kuwapa shida wachezaji wa kiungo na washambuliaji kusonga mbele.

Arsenal hawajatwaa kombe lolote tangu 2005, lakini wamekuwa wakiachia wachezaji wazuri kuondoka miaka ya karibuni, wakiwamo Cesc Fabregas, Samir Nasri na Robin van Persie.

Pamekuwa na maneno bila vitendo, ya Arsenal kutafuta golikipa mwingine wa kushindanishwa na Wojciech Szczesny ambaye hata hivyo Jumapili hii hakuwa na la kulaumiwa kimchezo.

Wenger amekuwa akisema anakiamini kikosi chake, na nahodha ambaye ni beki, Thomas Vermaelen amekuwa akisisitiza wana nia ya kushinda na hawana tatizo kisaikolojia.

Pamoja na kuachwa nyuma kwenye ligi kuu, Arsenal walichafua hali ya hewa kwa kutolewa kwenye Kombe la Ligi na timu ndogo ya Bradford.

Kadhalika walifungwa na Blackburn Rovers bao 1-0 na kutupwa nje ya michuano ya Kombe la FA, lakini ajabu ni kwamba Blackburn wamekuwa wakifungwa mechi karibu zote kwenye ligi ya chini, na hata baada ya ushindi dhidi ya Arsenal wameendelea kufungwa.

Kipindi kichungu kilihitimishwa kwa kipigo kutoka Bayern Munich, kwa mabao yaliyokuwa pia ya kuepukika, na hakuna matumaini makubwa wanapokwenda Ujerumani Machi 13.

Kroenke aliingia kwenye bodi ya Arsenal 2008 kabla ya kuichukua klabu 2011.

Magoli ya Spurs katika mechi hiyo ya kukata na shoka katika dimba la White Hart Lane yaliwekwa kimiani na Bale aliye kwenye chati na Aaron Lenon.

 

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

WHY HAS TANZANIAN BASKETBALL DROPPED AFTER HASHEEM THABEET’SSUCCESS?

Riadha amkeni, kwa hili serikali haina lawama – Evarist Chahali