in , ,

Tuzidi kumfukuza Ndemla kwa kelele zetu

Kila mguu wake unapokanyaga nyasi za uwanja wa taifa kuna kipya hutokea. Hii ni kwa sababu udongo mwingi wa kutengenezea vipaji ulitumika katika miguu yake.

Mwili wake ni mdogo sana!, udogo wa umbo lake ulisababishwa na MUNGU kutumia wingi wa udongo kuumba miguu ya Said Khamis Ndemla.

Hili ndilo eneo ambalo alitumia muda mwingi sana wakati anamuumba Said Khamis Ndemla. Alitaka kumtengeneza mchezaji mahiri, mwenye kipaji na fundi wa mpira. Na alifanikiwa kwenye hilo.

Akamwacha Said Ndemla ajiendeshe mwenyewe baada ya kupewa mtaji wa kipaji katika miguu yake. Yeye ndiye aliyeachiwa jukumu la kukifanya kipaji chake kinafika mbali kwa kukitumikia ipasavyo.

Kwenye suala la kutumikia kipaji hatumwiitaji tena mwenyezi MUNGU aje kutusaidia kutumikia vipaji vyetu. Hubaki kuwa ni wajibu wetu.

Hapa ndipo neno “Juhudi” linapotumika kuelezea mafanikio ya mtu husika. Wote tumezaliwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa kwa sababu MUNGU aliweka kitu kikubwa ndani ya kila mwanadamu, kinachokuja kututofautisha ni juhudi kati yetu.

Ndiyo mchezaji bora na mfungaji mahiri kuwahi kutokea duniani Cristiano Ronaldo aliwahi kusema ƙkipaji bila kukifanyia kazi kwa juhudi hakina maana yoyote.

Maana ya kipaji huja pale unapoongeza juhudi ndani ya kipaji chako. Faida ya kipaji haiji kwa kukaa chini na kujisifia kuwa una kipaji kikubwa. Hiki kitu hakipo kabisa.

Hakuna anayenufaika na kipaji chake kwa kukaa tu. Hakuna!, na hajawahi kutokea duniani. Tena kwenye hili ambayo hatuna mkataba na muda.

Hatuna mkataba na jua, jua likichomoza Mashariki haliwezi kutusubiri tuanze safari ya pamoja kuelekea magharibi. Kinachotokea ni sisi kwenda sambamba na jua ili likifika magharibi tuwe na uhakika wa kupata machache mazuri kulingana na juhudi zetu.

Hakuna jasho linalomwagika bure kwenye ardhi hii. Nahisi ndicho kitu ambacho Said Khamis Ndemla ameshindwa kukielewa zaidi tangu aanze safari yake ya mpira wa miguu.

Anatumia muda mwingi sana kukaa kivulini. Hataki kabisa kuhangaika juani ili kutengeneza mazingira mazuri ya kulia kivulini. Hapo ndipo anapopingana na ukweli wa mafanikio.

Ukweli ambao aliwahi kuusema Cristiano Ronaldo kuwa kipaji bila juhudi ni sawa na bure!, Said Ndemla anaonekana yuko tayari kupata bure kwa muda mrefu. Kakaa sana kivulini, sijui kakata tamaa au amepumzika ?.

Ameshindwa kuelewa kuwa hakuna ambaye aliwahi kuwa na urafiki na muda mpaka akafanikiwa hata kuukopa sekunde!

Ameanguka sana, tena mara nyingi na ameshindwa kwa muda mrefu kuamka kisha akajikung’uta mavumbi na kuanza kukimbia tena.

Wengi hukosea sana kwenye safari ya maisha hakuna ambaye asiye mkamilifu. Ukamilifu wetu huletwa na makosa ambayo sisi huyafanya mara kwa mara.

Tatizo moja tu ambalo huwa tunalisahau nalo ni kutumia muda mwingi tukiwa tumelala tulipoangukia huku tukiwa tunajutia makosa ambayo tumeyafanya.

Inawezekana muda uliumbwa kwa umbo la samaki!, hauwezi kurudi nyuma hata siku. Na ndicho kitu ambacho sisi hukitamani kila tunapofanya makosa. Hatamani sana muda urudi nyuma ili tu tusirudie makosa yetu na kusahau kuwa kusimama na kujifuta vumbi kisha tukaendelea na safari ndicho kitu ambacho tunatakiwa kukifanya.

Najua kuna vingi ambavyo Said Ndemla alivifanya na anavijutia kama mwanadamu, kitu ambacho anatakiwa kukifanya ni kusahau yote na kuanza kukimbia.

Akimbie haswaaa, akimbie sana kama ambavyo alivyokuwa anakimbia kwenye mechi dhidi ya Stand United. Mbio za aina hiyo ndiyo mbio sahihi kwake yeye kufika sehemu ambayo anaitamani, sehemu ambayo hata sisi tunatamani afike. Sitaki kumuona hapa nchini, macho yangu yashakataa ƙkabisa kuwa miguu ya Said Ndemla inafaa kumalizia soka kwenye ligi yetu hii , ndiyo maana huwa nafurahi sana kipindi ambacho mashabiki wanapompigia kelele za kuondoka Tanzania. SAID NDEMLA ONDOKA TANZANIA!

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Zahera anakubaliana na mimi kuwa Ajib ni mchezaji wa mechi ndogo?

Tanzania Sports

Simba yenye NDEMLA ni hatari zaidi kuliko Simba yenye MKUDE