Hivi karibuni klabu ya Singida Fountain Gate ilihamishia makazi yake kwenda katika jiji la mwanza na hazikupita siku nyingi wakatangaza kwamba wameamua kuachana na benchi lao la ufundi amalo pia lilijumuisha moja ya wachezaji magwiji nchini Tanzania ambaye aliwahi kucheza soka katika klabu kubwa ya Vancouver whitecaps aitwaye Nizar Khalfan. Kabla watu hawajakaa sawa klabu hiyo ilitangaza kwamba imeamua kumchukua kocha Jamhuri “Julio” Kihwelo Kama kocha wa mda ambaye atamalizia mechi zilisalia mpaka msimu utakapomalizika. Kabla watu hawajakaa sawa Zaidi idara ya habari na mawasiliano ya klabu hiyo ikatangaza kwamba wanakuja na kampeni inayofahamika kama Ajenda kumi za Julio.
Tukianza kumuangalia wasifu wa Kocha Jamhuri “Julio” KIhwelo tunaona kuwa ni mojawapo ya magwiji nchini Tanzania kwani ana uzoefu wa mda mrefu na ni katika makocha wachache nchini Tanzania ambao wanasifika kuwa walikuwa wachezaji mashuhuri na wakafanikiwa kuwa ni mojawapo ya makocha ambao wamejitengenezea jina katika kiwanda cha soka nchini Tanzania.
Julio ametokea katika familia mashuhuri ya soka ambayo imezalisha wanasoka kadhaa ikiwemo Musa Kihwelo aliyechezea Simba, Mwanamtwa Kihwelo aliyechezea Simba yanga pamoja na Reli morogoro, Mhehe Kihwelo aliyechezea Pilsner na Mwisho ni yeye Jamhuri Kihwelo aliyechezea Pilsner na Simba. Katika uwanda wa ukocha amefundisha vilabu kadhaa vya ndani na nje ya nchi. Vilabu vya ndani ya nchi ambavyo amewahi kuvifundisha ni ikiwemo na Mwadui ya Shinyanga, Simba Sports club, Namungo, Coastal Union. Nje ya nchi amewahi kufundisha soka katika nchi za Qatar, Yemen na Dubai. kiwasifu ni kocha ambaye huwa anajiamini sana na huwa anajua kunogesha mechi za timu ambazo huwa anazifundisha kwani huwa ana ufundi wa kutoa maneno ambayo huwafurahisha mashabiki na pia kwa namna moja ama nyingine huogopesha timu pinzani.
Katika ufundishaji wake amekuwa ni mpinzani mkubwa wa klabu ya wanajangwani ya Yanga na kila anapokuwa ana mechi na yanga amekuwa kabla ya mechi huwa ana kawaida ya kutoa kauli za kejeli ambazo huwa zinaendeleza utani wa jadi licha ya kwamba yeye sio mtumishi wa Simba. Mfano katika miaka ya nyuma aliwahi kuwatania wanayanga kwamba klabu yao ni kama Pombe ya ngomani kwama kila mtu anaweza kuinywa pombe hiyo ambapo alikuwa anamaanisha kwamba Yanga inaweza kufungwa na timu yoyote ile na kwama haimtishi wala kidogo. Licha ya kwamba amekuwa ana matokeo mazuti pindi anapokuwa anafundisha ila kuna mda matokeo yanapokuwa sio mazuri amekuwa anatoa kauli ambazo kwa mda mwingine mfano mzuri ni pale Oktoba 2 mwaka 2016 alitangaza hadharani kwamba anajiuzulu kufundisha soka la Tanzania kufuatia kutoridhishwa na maamuzi yanayofanywa na marefa na hiyo ilikuwa baada ya kupata kufungwa kipigo cha goli 1 kwa sifuri kutoka kwa wababe wa mbeya ama Mbeya City katika uwanja wa Sokoine.
Tukirudi katika Ajenda 10 za Julio taafsiri ambayo inapatikana kwa haraka ni kwamba ana mechi kumi ambazo ni za kumalizia msimu. Mechi hizo ni pamoja na Dhidi ya vilabu vifuatavyo: 1. Namungo(nyumbani), 2. Yanga(Nyumbani) 3.Ihefu(ugenini), 4.Mashujaa(nyumbani) 5.Dodoma jiji(nyumbani), 6. Coastal union (ugenini) 7.JKT Tanzania (ugenini), 8.KMC ( ugenini) , 9.Geita Gold(nyumbani) na 10.Kagera Sugar(Nyumbani)
Mechi yake ya kwanza dhidi ya Namungo ambayo ameichezea uwanja wa nyumbani ameianza vizuri kwani amemfunga ushindi mdogo wa goli moja kwa sifuri. Huo umekuwa ni mwanzo mzuri kwake na kama akijipanga vizuri anaweza kuimaliza timu katika nafasi nzuri kama waswahili wasemavyo “…… mchezo kwao hutunzwa”. Katika ajenda zake ana jumla ya mechi 6 kati ya 10 alizobakiza atacheza nyumbani kwa hiyo kama atakuwa amejipanga vizuri anaweza akaondoka na pointi 18 ambazo zitakuwa zimemuweka katika hatua nzuri katika ligi. Kama Singida fountain Gate watamtumia vizuri kocha Julio pia katika mechi za nyumani wanaweza kujikuta wakaongeza hamasa katika mechi zao kwani ni kocha ambaye anayeweza kutengeneza maneno yenye kutia hamasa na kuwafanya mashabiki wengi wakaifuatilia klabu hiyo hususani katika mechi za nyumbani.
Changamoto atakazokutana nazo kocha Julio ni kwanza kwamba mzunguko wa pili huwa sio mrahisi kwani kila klabu huwa inatafuta matokeo kwa nguvu kubwa ili iweze kuwa kwenye nafasi nzuri katika kumalizia ligi pili na mechi yake ya pili itakuwa dhidi ya bingwa mtetezi wa ligi kuu bara ambaye ni klabu ya Yanga ambayo kwa namna moja ama nyingine iko katika hali ya hasira baada ya kupoteza mchezo wake dhidi ya klabu ya matajiri wa Chamanzi Azam FC. Mchezo huo utakuwa sio mwepesi sana kwani klabu hiyo itajipanga sana kuhakikisha inaondoka na alama tatu dhidi yao kwani ikifanya hivyo itakuwa imejiweka kwenye hali nzuri kutetea ubingwa wao wa ligi. Kama kocha Julio atafanikiwa kuifunga Yanga basi atakuwa amekiweka kikosi chake katika morali nzuri watakuwa na ari ya kujiamini kwa hali ya juu na watatisha vilabu vingine ambavyo wamebakiza navyo mechi.
Changamoto ya pili ni kujenga mahusiano mazuri Zaidi na uongozi wa klau hiyo na kama hatakuwa na matokeo mazuri basi ni ngumu kuwa na mahusiano hayo kwani akifungwa inawezekana asimalize hata hizo mechi. Tumeshuhudia klau ya Singida Fountain Gate ilifukuza kocha wake mholanzi Hans van Der Pluijm mnamo Agosti 30 mwaka 2023 na halikadhalika disemba 28 mwaka 2023 aliyekuwa kocha wa timu hiyo baada ya kufukuzwa Pluijm naye alitangaza kuachia ngazi kwa hiari yake na aliondoka nchini na kurudi kwao kwa kusema kwamba hakuwa na mahusiano mazuri ya kikazi na uongozi wa timu hiyo. Hiyo ilikuwa mda mchache kabla ya kwenda kwenye Mapinduzi Cup.
Fursa aliyonayo kwa sasa ana timu ambayo ina wachezaji wa ushindani ambao wanaweza kumletea matokeo mazuri na kama akifanikiwa kushinda mechi zote basi atakuwa kwenye nafasi ya kutengeneza historia yake mpya. Rai yangu kwa viongozi wa Singida Fountain Gate kama kocha Julio atawapa matokeo ya kuwafanya wafuzu kushiriki mashindano ya kimataifa basi wakae naye na wampe nafasi ya kuendelea kukinoa kikosi hicho pindi wakiwa wanashiriki mashindano ya kimataifa.
Comments
Loading…