Mshabiki wanashangilia tu. Viongozi wanasajili tu. Wadau wanajadili zaidi. lakini makocha hawalali usingizi linapofika suala la kuamua kikosi cha kucheza kwenye pambano lolote.
Real Madrid kikosi cha kwanza kipo imara kwa sasa kuliko kilivyokuwa msimu uliopita, licha ya mabosi wa timu hiyo kutofanya usajili wa wachezaji wapya angalau hadi sasa.
Wachezaji wakongwe katika kikosi cha Real Madrid walikuwepo katika awamu ya kwanza ya ukocha ya Zinedine Zidane, lakini kuna wachezaji chipukizi wameibuka na kutisha kuchukua nafasi za wazoefu. Chipukizi hao wamekuja katika kikosi wakiwa na mtiririko mzuri kwani wanajigunza mengi kupitia wakongwe waliopo kwenye kikosi hicho.
Chini ya Zidane Real Madrid imekuwa ikiwatumia wachezaji walewale na uti wake wa mgongo umejengwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa klabuni hapo na kwenye mashindano mbalimbali, na ambao walileta mafnikio na kutikisa dunia kutokana na kandanda safi pamoja na kutwaa mataji ya ulaya na dunia.
Kwenye kiungo bado wanategemewa Toni Kroos na Luka Modric tangu mwaka 2014. Wawili hawa wamefanikiwa kuleta ubora wa ufundi wao katika kuongoza safu ya kiungo ya Real Madrid. Toni na Modric ndiyo wanaamua namna Real Madrid inavyotakiwa kucheza.
Wao ndiyo injini ya kulinda mtindo wa kucheza wa klabu hiyo. Toni maarufu kama PhD amekuwa ametajwa kuwa ndiye mpamga njia za mashambulizi ya Real Madrid, huku Modric akiwa mkamilisha kazi inayofanywa na Toni Kroos ili kuwafikia washambuliaji na mawinga.
Sasa, kuibuka kwa wimbi la wachezaji chipukizi kikosini hapo, kiufundi na uimara wa miili yao kumeleta mjadala mkubwa namna gani Zinedine Zidane anaweza kuwatumia vijana na wakongwe. Zidane anaweza kuwa na mnamna au mbinu tofauti za kucheza mechi yoyote, iwe La Laiga au Ligi ya Mabingwa Ulaya. Swali linaloulizwa atacheza namna gani na wachezaji wakongwe pekee au ataongeza chipukizi? Pengine anaweza kuwatumia chipukizi kuwa wengi kuliko wakongwe? Ni mtihani.
MARTIN ODEGAARD
Kwa mfano, Martin Odegaard ni mfano halisi wa wachezaji chipukizi ambao wamejaliwa uwezo mkubwa wa kiufundi na uimara wa mwili wake. Odegaard ana nguvu na uwezo wa kumiliki mpira bila kupokonywa na mchezaji wa timu pinzani. Vitu viwili hivi vinamfanya awe mchezaji anayekaribia kuwa tishio kwa wakongwe ndani ya Real Madrid.
FEDE VALVERDE
Mara kadhaa amechukua namba za Toni Kroos na Luka Modric. Kinda huyo alianza kuibuka taratibu wakati wa Julen Lopetegui, kabla ya kuongeza muda wa kucheza chini ya Santiago Solari. Ni Zinedine Zidane ndiye aliyempa nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza.
Fede Valverde ana nguvu, kasi na uwezo mkubwa wa kupiga mashuti langoni mwa adui. Amekuwa akisaidia kuipandisha timu kushambulia, lakini hana ujuzi kama Modric au Kroos. Uwezo wake unafananishwa na kiungo wa kucheza kiungo cha kushambulia, kukaba na winga kwa wakati mmoja. Makocha wake wanamwona kama silaha ya kuamsha ari, kudhibiti mashambulizi ya adui na mlinzi wa walinzi.
RODRYGO NA VINICIUS JUNIOR
Wawili hawa ni kama washambuliaji, lakini vilevile wanaweza kuchza nafasi za wing azote mbili; kulia na kushoto. Vinicius Junior na Rodrygo Goes wametikisa kikosi cha kwanza cha Real Madrid na kufanikiwa kuwanyima usingizi baadhi ya wakongwe kama Gareth Bale na Lucas Vazquez.
Katika mechi za maandalizi ya msimu huu wamekuwa wakionesha kupevuka kiakili na kiufundi. Na zaidi hawa ni vipaji kutoka nchini Brazil, ambako soka limezalisha vipaji vya kiwnago cha juu wakiwemo makinda hao.
Tofauti zao zipo katika maeneo mawili; kufanya maamuzi wa kiufundi na kasi ya mchezo. Vinicius ana kasi na fundi wa kusambaratisha safu ya ulinzi ya timu pinzani. Amekuwa silaha ya kuwakimbiza mabeki na kusababisha wafanye makosa yanayochangia mabao,penati na kona. Real Madrid imenufaika kwa vyema kutoka kwa kinda huyo.
Rodrygo ni kama mwanahisabati. Anasifika kwa utulivu wa kiakili, ufundi wa hali juu, uwezo wa kukokota mpira, kusoma mchezo na mchezaji mahiri wa kucheza kitimu. Rodrygo hana kasi kama Vinicius lakini kiufundi ndiye amejaliwa kipaji kikubwa kuliko Vini. Makocha wa viungo wanatumia maandalizi ya msimu kuwajenga kimwili. Nia ni kuwafanya wawe na nguvu na misuli ya kutosha kukabiliana na mabeki wenye nguvu kutoka timu pinzani.
“Hawajapoteza uwezo wao wa kukokota mpira na kupiga chenga kwa kasi, lakini wameongezewa nguvu za kimwili kwa sasa,” wanasema makocha binafsi wa viungo wa wachezaji,” Thiago Lobos na Marcel Duarte.
FERLAND MENDY
Ukiwangalia chipukizi hao wanne, beki wa kushoto Ferland Mendy ni mchezaji pekee ambaye anatajwa kuwa na nguvu,kasi kubwa. Yeye ndiye mchezaji wa kwanza kuwa nguvu zaidi kikosini humo. Kama Zidane ataamua kupanga kikosi cha kwanza hadi sasa, kinaweza kuwa hivi; Thibaut Courtois, Dani Carvajal, Raphael Varane, Sergio Ramos, Mendy, Casemiro, Valverde, Odegaard, Rodrygo, Vinicius na Karim Benzema.
Hata hivyo, wachezaji waliotumikia kikosi cha Zidane katika awamu ya kwanza akiwa kocha klabuni hapo wanatarajia kufanya mazungumzo namna ambavyo watatumika msimu ujao.
Kwenye nafasi ya kiungo mkabaji na ushambuliaji, watakuwepo Casemiro, Kroos na Modric. Nafasi zingine watakuwepo Eden Hazard, Isco na Marcelo, ambao watatumika kiufundi zaidi msimu huu. Kikosi cha kwanza kinatarajiwa kupangwa; Courtois, Carvajal, Varane, Ramos, Marcelo, Casemiro, Kroos, Modric, Isco, Hazard na Benzema.
Aghalabu Zidane hushangaza watu pale anapopanga kikosi chake, kwahiyo inawezakana kabisa kukawa na kikosi ambacho kitawashangaza wengi msimu huu. Lakini naye atakuwa njia panda kufanya uamuzi wa kuchagua wachezaji wa kuanza mechi msimu huu 2020/2021.
Comments
Loading…