Mabao ya Donald Ngoma na Amis Tambwe yameizamisha Simba jioni hii ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam kwenye mchezo wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baina ya watani wa jadi.
Timu hizo ziliuanza mchezo zikifanya mashambulizi ya kupokezana katika dakika za awali huku kila moja ikionekana kuwa na tahadhari pengine kuepuka kufungwa bao la mapema. Ni Simba SC ambao walifika langoni mwa wapinzani mara nyingi zaidi.
Wekundu hao wa Msimbazi waliweza kupata kona nne ndani ya dakika ishirini za mwanzo huku Yanga wakiwa hawana kona yoyote katika kipindi hicho.
Dakika ya 22 ikamshuhudia mwamuzi Jonnesia akionyesha kadi ya njano ya kwanza ya mchezo iliyokwenda kwa Abdi Banda baada ya mlinzi huyo wa kati kumchezea madhambi mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma.
Dakika tatu baadae Banda alionyeshwa kadi ya pili ya manjano na kutolewa nje ya uwanja baada ya kumwangusha Donald Ngoma kwa mara nyingine nje kidogo ya eneo la hatari.
Ni kadi ambayo wengi waliitilia mashaka lakini mashaka hayo hayakuweza kutengua maamuzi ya mwamuzi Jonnesia na hivyo Simba kulazimika kucheza pungufu kwa zaidi ya saa nzima iliyokuwa imebakia.
Kasi ya mashambulizi ya Simba ilionekana kupungua pengine kucheza pungufu kulichangia hilo.
Mnamo dakika ya 39 makosa ya Ramadhani Kessy yakaigharimu Simba baada ya mlinzi huyo wa kulia kurudisha mpira finyu kwa golikipa Vincent Angban, ambao ulinaswa na mshambuliaji Donald Ngoma aliyefunga bao rahisi na kuiweka Yanga mbele.
Bao hilo lilidumu mbaka filimbi ya kuashiria tamati ya dakika 45 za mwanzo ilipopulizwa. Yanga kwa mara ya pili mfululizo wakaenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao moja dhidi ya watani wao baada ya kufanya hivyo hivyo Septemba mwaka jana.
Baada ya kurejea kutoka mapumziko mwalimu Jackson Mayanja akalazimika kufanya mabadiliko yake ya kwanza kwa kumtoa Mwinyi Kazimoto na kumuingiza Novat Lufunga aliyesajiliwa miezi miwili iliyopita kutoka African Sports ya Tanga.
Hayo yalikuwa mabadiliko ya kiufundi ambapo Mayanja alikuwa akijaribu kuliweka sawa eneo lake la ulinzi akiziba pengo la Abdi Banda aliyekuwa ameonyeshwa kadi nyekundu.
Katika dakika ya 53 Yanga wakafanya mabadiliko yao ya kwanza wakimtoa Haruna Niyonzima na nafasi yake kuchukuliwa na Simon Msuva.
Mfungaji huyo bora wa msimu uliopita akaonyesha makali yake punde tu baada ya kuingia kwa kutengeneza nafasi ambayo hata hivyo haikuweza kuzaa bao baada ya Amis Tambwe kupiga shuti butu.
Simba wakafanya mabadiliko yao ya pili kwenye dakika ya 59. Safari hii aliyetolewa alikuwa kinara wa mabao msimu huu, Hamis Kiiza na kumpisha Danny Lyanga. Deus Kaseke wa Yanga naye akatolewa mnamo dakika ya 64 akimpisha Geofrey Mwashiuya.
Kwenye dakika ya 69 Amis Tambwe wa Yanga naye akaingia kwenye kitabu cha mwamuzi Jonnesia baada ya kuzawadiwa kadi ya manjano. Dakika tatu baadae mshambuliaji huyo akafunga bao lake la 15 la msimu baada ya walinzi wa Simba kufanya uzembe kwa mara nyingine.
Mnamo dakika ya 79 Simon Msuva pia akalambwa kadi ya manjano baada ya kuupiga mpira kwa makusudi wakati mwamuzi alishaamuru usimame.
Kipindi chote hiki Simba hawakuwa wakionyesha dalili zozote za kurudisha bao. Kuwa nyuma kwa mabao mawili huku wakiwa pungufu kuliishusha morali ya Wekundu hao kwa kiasi kikubwa.
Mwalimu Jackson Mayanja akafanya mabadiliko yake ya mwisho ya mchezo mnamo dakika ya 80 akimtoa Ibrahim Ajib na kumuingiza Bryan Majwega.
Dakika 10 baadae kipenga cha mwamuzi Jonnesia kikaashiria kumalizika kwa mchezo huo. Ushindi wa Yanga unawarudisha kileleni mabingwa hao watetezi wakiwa na alama 46 baada ya kucheza michezo 19.
Vijana wa Jackson Mayanja wanarudi kwenye nafasi ya pili wakiwa na alama 45 baada ya kucheza michezo 20.