in

Yanga wanapanda na kushuka

Yanga FC

MABINGWA wa zamani Ligi Kuu Tanzania Yanga wapo kileleni kwa Ligi hiyo baada ya kushinda mabao 2-0 dhidi ya waliokuwa wenyeji wao KMC kwenye dimba la CCM Majimaji Mjini Songea mkoani Ruvuma.  

Ushindi wa Yanga ni muhimu katika kujenga imani kwa mashabiki,wachezaji na benchi la ufundi ambalo limejaa watu wa mpira haswa. Ni ushindi ambao wanauhitaji  zaidi na tena kutoka timu ngumu ya watoto wa mjini Kinondoni. 

Yanga ni timu ambayo inataka kunyakua taji hilo, lakini ukitzama mechi zao kuna jambo linaweza kuwagharimu siku zijazo. Gharama ya jambo hilo ndio hswa hoja yangu ninayotaka kuzungumzia leo hii.  

Katika makala haya ninaeleza namna Yanga inavyopanda na kushuka. Nikianza upande wa kupanda na kutengeneza nafasi za kufunga kisha nitamaliza kuonesha namna Yanga wanavyoshuka kadiri mchezo unavyoendelea na kuhatarisha lango lao.

NAMNA WANAVYOPANDA 

Safu ya ulinzi ya Yanga imejaa wacheza mahiri mno kuliko msimu uliopita. Kuanzia langomi kuna Djgui Diarra, Bakari Nondo Mwamnyeto,Dickson Job na Kibwana Shomari. Hicho ni kipande cha kwanza ambacho kinaipa uhai Yanga katika mbio zao za kuwania taji la Ligi Kuu ya NBC.

Kipande cha pili cha mafanikio ya Yanga ni safu ya kiungo. Safu hiyo iko chini ya Khalid Aucho,Yannich Bangala,Feisal Salum na Zawadi Mauya ambao wanampa nafasi kocha wako Nasredine Nabi kuwa na uchaguzi murua wa kupanga kikosi cha kwanza. Katika safu hiyo bado kiungo machachari  Tonombe Mukoko ambaye alikuwa anatumikia adhabu ya kukosa mechi kadhaa.

Eneo la Kiungo linawapa nafasi Yanga kutanua na kujidai mno. Wanaweza kupiga pasi fupi fupi kutoka kwa Aucho, kisha wanaweza kupata huduma ya ubabe na kuzima mipango ya mashambulizi dhidi yao kupitia Yannick Bangala. 

Pia wanaweza kupata faidi za kiufundi kutoka kipaji cha Feisal Salum. Kimsingi sasa Yanga wamepata watu wa kumngā€™arisha Fei Toto kwa sababu awali alikuwa analzimika kutumikia eneo la kiungo mkabaji. 

Sasa Fei Toto anatumika kama kiungo wa ushambuliaji au mshambuliaji namba mbili yaani nambari kumi. Ufanisi wa Fei Toto unatokana na kipande cha viungo kuwa hodari na imara wakati wa mchezo. 

Aucho na Bangala ni wachezaji imara zaidi, wanapokezana majukumu yao kukaba kutoka eneo lao kwenda kulia na mwingine kwenda kushoto. Aucho anatumia zaidi mguu wa kushoto yeye hukaba kwenda kushoto, wakati Bangala anakaba zaidi kwenda kulia. Hilo linamwezesha Fei Toto kuwa kiungo huria anayelindwa zaidi na ndio kitakuwa chanzo cha kupachika mabao ya kutosha.

Kipande cha safu ya ushambuliaji pia kina wachezaji wenye ushindani. Eneo hili linaundwa na mawinga wazuri Jesus Moloko, Deus Kaseke na Farid Mussa. 

Eneo la ushambuliaji lina Herieter Makambo,Fiston Mayele,Saido Ntizonkiza,Ditram Nchimbi na Yusuf Athuman. Ni eneo linalompa kocha wakati mgumu kuchagua nani wa kuanza mechi. 

Mayele ndiye anaonekana kuwa chaguo la kwanza la Nabi, na kisha wanafuata wengine. Safu hii imeanza Ligi vizuri kwa kutumia nafasi za kufunga wanazopata. Kwenye mchezo dhidi ya wapinzani wao tumeona namna wanavyojitahidi kupachika mabao kila wanapopata nafasi. 

Upo uwezekano wa kupata mabao mengi msimu huu kutoka kwa washambuliaji tofauti. Lakini pia kupata mabao machache ni jambo la kawaida kwa sababu mabeki wa timu pinzani watakuwa wanapania kuwadhibiti.

YANGA WANAVYOSHUKA

Kama unadhani bao la kwanza la Ligi Kuu ya NBC Tanzania lililofungwa dakika 49 na William Edgar wa Mbeya Kwanza kuwa ndilo la mapema zaidi basi unakosea. Ni kweli Edgar ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao la NBC Premier League msimu huu 2021/2022, lakini bao lake si la mapema. Na pia hajafikia rekodi za Yanga.

Katika mechi za Yanga zipo dakika 11 za hatari. Mechi zao nyingi chini ya kocha Nabi wanatafuta ushindi ndani ya dakika 11 za kwanza za mchezo. Katika dakika hizo Yanga wanacheza kwa kasi,maarifa,nguvu na ufundi wa hali ya juu kusaka mabao. Wanalitia presha lango la adui na muda wote wanaitengeneza mechi kuwa ya presha kubwa kwa wapinzani.

Ushindi wao dhidi ya KMC mjini Songea ni ushahidi ulionipa nafasi ya kuona namna wanavyoshuka. Katika dakika 11 za mchezo huo Yanga walishapata mabao mawili kutoka kwa Feisal Salum na Fiston Mayele. Zilikuwa dakika za hekaheka ambazo zinamfanya mpinzani apoteze mwelekeo. 

Yanga wanakumaliza dakika za awali kabisa kiasi kwamba mpinzani anapokuja kushtuka anajikuta hana maarifa mengine. Ni kwamba Yanga wanakuvuruga katika dakika 11 wanapata mabao,kona,faulo au penalti. 

Wataliweka lango lako katika shinikizo. Hakika presha yao inakuwa kubwa kiasi kwamba msimamizi wa benchi la ufundi KMC alikuwa katika wakati mgumu kuwakumbusha wachezaji wake namna ya kutuliza akili. Yanga wameshafanya hivyo dhidi ya Simba ndani ya dakika 11 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii walishamaliza kazi. Iko hivyo katika mechi. 

Ndani ya dakika 11 Yanga wasipopata bao timu yao inakuwa na hali tofauti. ikimaliza dakika 45 pasipo kufumania nyavu za adui yake, hali ya Yanga inashuka zaidi. Kadiri muda unabvyokwenda utaona kasi yao inashuka, nguvu zao zinashuka na zaidi wanajirundika nyuma ili kupiga pasi ndefu. 

Ni kama vile mpango wa kwanza ukishindikana timu inakosa namna nyingine ya kuibuka na ushindi. Kuanzia dakika ya 70 Yanga hawana ule ubora wanaoanza nao. Unaweza kusema wachezaji wanakuwa wamechoka, lakini kadiri muda unavyokwedna ndivyo timu inashuka zaidi. 

Kushuka kwao kunchangiwa na mambo mawili; kupata mabao mapema na hivyo kutaka kulinda ushindi tu. Pili wakishindwa kupachika mabao ndani ya 11 au 45 za kipindi cha kwanza ni kama uwezo wao unapotea. 

Kipindi cha pili wanazo dakika 11 za kusaka bao, lakini wakikosa hilo huwa hawana ujanja mwingine. Timu inapoa, inashuka, inaanza kutafuta namna ya kujilinda zaidi kuliko mipango ya kufunga. 

Huo ndio wakati ambao Yanga wanawategemea zaidi Aucho na Bangala kuzima kasi na mashambulizi ya wapinzani wao. Katika eneo hili siku wakipata viungo watakaowadhibiti Aucho na kuwarudisha nyuma zaidi itakuwa hatari kwao. 

Faida pekee watakayotegemea ni umahiri wa Dickson Job na Bakari Nondo ikiwa watakuwa ā€˜wameamka vizuriā€™. Nao wakipoteana ipo hatari langoni mwao. 

Kilichopo sasa ni kwamba Yanga wanawatengeneza wapinzani wao kuogopwa ndani ya dakika 11 za kipindi cha kwanza, mambo yasipoleta matokea chanya huwa kinyume kwao. 

Ndiyo maana kuanzia dakika 70 Yanga huwa wanashambuliwa zaidi kuliko wao kushambulia. Ikitokea timu ngangari inaweza kutumia dakika 20 za mwisho kuiadhibu pakubwa Yanga. Je, ni lini Yanga wataondokana na udhaifu huu? Kazi iko mikononi mwa benchi la ufundi.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Newcastle United kutikisa Ligi Kuu Ulaya

Michael Edward

Siku Michael Edward akingā€™oka Liverpool