in

Yanga na Ajib wanahitajiana..

Ibrahim Ajibu Yanga

Moja ya kitu ambacho nilifurahia ni baada ya mimi kusikia kuwa Yanga wamepeleka ofa ya kutaka kumsajili Salum Abubakary “SureBoy”. Furaha yangu ilitokana na mimi kuona weledi mkubwa uliofanya na viongozi wa Yanga.

Kwanini nasema hivi? Kumekuwa na taratibu mbovu za usajili nchini kwetu ambapo viongozi wengi wa timu hapa nchini humsubiri mchezaji amalize mkataba ili amsajili. Lakini kitendo cha Yanga kwenda moja kwa moja Azam FC kutaka kumsajili Salum Abubakary kilikuwa kitendo cha mapinduzi.

Mapinduzi ya usajili, mapinduzi ya kiweledi. Pamoja na Yanga kupeleka ofa hiyo na kukataliwa mimi nitazidi kuwapongeza Azam FC na Yanga. Turudi kwa Yanga sasa, walitaka huduma ya Salum Abubakary “SureBoy”.

Ukiniuliza kwanini walitaka huduma yake nitakujibu kitu kimoja tu, Yanga msimu uliopita safu yake ya kiungo haikuwa na viungo ambao ni wabunifu, viungo ambao wangeisaidia Yanga kufunga na kutengeneza magoli. Salum Abubakary “SureBoy” alikuwa sahihi kwenye eneo hili.

Kwa bahati mbaya biashara hii imeshaisha. Haitofanyika tena kwenye dirisha hili la usajili. Naamini Yanga mpaka sasa hivi bado inahitaji kiungo ambaye atakuwa na majukumu ambayo yatakuja kuziba udhaifu wao katika eneo la kiungo cha kati.

Yanga wanahitaji njia mbadala ndani ya uwanja. Msimu uliopita walikuwa wanahangika sana kufunga magoli kwa sababu safu butu ya ushambuliaji. Kuwa butu kwa safu ya ushambuliaji ya Yanga kulihitaji njia mbadala ya Yanga kupata magoli.

Njia sahihi ambayo ni mbadala ni kuwa na viungo ambao wanaweza kufunga. Kuwa na viungo ambao wanaweza kuisaidia timu yao kipindi ambacho safu ya ushambuliaji inapokuwa haina uwezo wa kufunga magoli.

Watani wao Simba mwanzoni walikuwa wanamtegemea sana Meddie Kagere kwa ajili ya kufunga magoli. Meddie Kagere alifikia hatua ya yeye kutokuwa na uwezo mkubwa wa kufunga magoli kama mwanzo lakini safu ya kiungo cha Simba kiliisaidia timu kufunga magoli.

Hiki kitu hakipo Yanga na wanahitaji kukitatua. Kama Yanga wameshindwa kumsajili Salum Abubakary “SureBoy” wanatakiwa kufikiria namna ya kwenda Simba kwa ajili ya kumsajili Ibrahim Ajib. Wanahitaji huduma yake kabisa.

Aliwahi kupita Yanga, alifanikiwa kutoa pasi za magoli 20 huku akifunga magoli 7 katika msimu wake wa mwisho na Yanga. Kwa sasa Simba hana nafasi kubwa sana. Anatakiwa kwenda sehemu ambayo atakuwa na nafasi kubwa ya kucheza na kuisaidia timu.

Yanga inamwihitaji Ibrahim Ajib na Ibrahim Ajib anaihitaji Yanga. Kama Yanga waliweza kwenda kwa Azam FC ili kumsajili Salum Abubakary “SureBoy” wanatakiwa kwenda Simba kwa ajili ya kuomba kumsajili Ibrahim Ajib.

Weledi ambao waliutumia kwa Salum Abubakary “SureBoy” unatakiwa uendelezwe. Ibrahim Ajib ana mkataba na Simba. Yanga wanatakiwa kuongea na Simba kwa ajili ya kumsajili Ibrahim Ajib tena ili wazibe mapungufu ndani ya kikosi chao.

Yanga inamwihitaji Ibrahim Ajib kwa sababu haina viungo ambao wanauwezo mkubwa wa kufunga magoli pamoja na kutengeneza nafasi nyingi za magoli. Ibrahim Ajib anaihitaji Yanga kwa sababu Simba hana nafasi kubwa, wote wawili wanahitajiana.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

72 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Senzo

Yanga Walimnyatia Senzo Kitambo

Manara, Muro, Nugaz nani zaidi?

‘Midomo’ inayonogesha timu za Ligi Kuu Bara