KIUNGO wa kimataifa wa Ivory Coast na Manchester City, Yaya Toure amesema wachezaji weusi wanaweza kugombea fainali za Kombe la Dunia 2018 zilizopangwa kufanyika Urusi.
Toure alisema hayo kutokana na ubaguzi aliooneshwa wakati City wakicheza nchini Urusi, ambapo mwamuzi hakuchukua hatua licha ya Toure kumjulisha kilichotokea.
Weusi hao wanaweza kufikia hatua hiyo iwapo Urusi haitafanya jitihada za kukomesha vitendo vya kibaguzi na Toure anasema ikiwa hali itabaki ilivyo, wasitarajie wachezaji weusi kwenye mashindano hayo makubwa.
“Na kama kweli wachezaji wote watasema hawaendi Urusi, basi hilo halitakuwa Kombe la Dunia,” akasema Toure na kuongeza moto kwa Fifa ambayo tayari inaweweseka kwa kupanga fainali za 2022 nchini Qatar ambako joto lake halihimiliki.
Toure alitoa madai ya washabiki kumfanyia vitendo na ishara za kibaguzi Jumatano wiki hii wakati City walipocheza na CSKA Moscow.
Pamoja na kuwa nyuma kwa bao moja, City walifanikiwa kusawazisha na kuongeza la ushindi, kupitia kwa mchezaji wa Argentina, Sergio Aguerro.
Uefa imesema inachunguza jambo hilo huku klabu hiyo mwenyeji ikisema kwamba walipitia mkanda mzima wa mchezo wa siku hiyo lakini hawakuona chochote.
Klabu hiyo ilidai imeshangazwa na kuchukizwa na tuhuma za Toure, ambapo klabu hiyo itaitwa mbele ya kamati ya nidhamu ya Uefa kwa ajili ya shauri hilo Oktoba 30.
Vitendo vya ubaguzi kwenye soka vimekuwa vikiongezeka, lakini pia harakati za kupiga vita zimeendeshwa, ikiwa ni kwa kiasi kikubwa na wachezaji wenyewe weusi, ambapo ilipata kutokea mechi ikavunjwa.
Rais wa Fifa, Sepp Blatter amekuwa akipiga vita ubaguzi lakini pia akisisitiza haja ya kuunganishwa nguvu kwa wadau kukabili wachache wabaguzi badala ya kufuta mechi, jambo ambalo lingekuwa ushindi kwa wabaguzi hao.
Comments
Loading…