TANZANIASPORTS imelitazama pambano la fainali hiyo kama njia nyingine ya miamba ya Italia kurudi katika ramani ya soka kwenye mashindano ya Ulaya.
PEP GUARDIOLA ameingia katika vitabu vya historia mara mbili baada ya kutwaa taji la tatu la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na klabu mbili tofauti. Historia ya pili ni kutwaa mataji matatu msimu mmoja na kufikia rekodi ya aliyekuwa kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson aliyoweka mwaka 1999.
Ferguson alitwaa mataji ya EPL, FA na Ligi ya Mabingwa akiwa na nyota kama vile Andy Cole, Dwight Yorke,Ole Gunnar Solskaer katika safu kali ya ushambuliaji. Guaridola amefikia rekodi nyingine ya kutwaa mataji matatu ya Zinedine Zidane ambaye alifanya hivyo mfululizo mara tatu akiwa na Real Madrid pekee.
Hadi sasa Guardiola amebakiwa na rekodi ya Carlo Ancelotti ambaye ametwaa mataji manne ya Ligi ya Mabingwa. baada ya kutamba kwenye EPL, sasa Guardiola ameingiza rekodi hiyo mbele ya miamba ya soka Serie A, Inter Milan.
TANZANIASPORTS imelitazama pambano la fainali hiyo kama njia nyingine ya miamba ya Italia kurudi katika ramani ya soka kwenye mashindano ya Ulaya. Ni misimu mingi imepita tangu vilabu vya Italia kutamba kwenye mashindano ya Ulaya. Ni kama vile Ligi Kuu Italia ilipoteana kwenye anga za ushindani.
Serie A kwenye Ligi ya Mabingwa
Wataliano wameweka rekodi ya kwanza kucheza fainali tatu msimu mmoja huku wakipoteza zote. Inter Milan walipepetana na AC Milan katika mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Inter Milan walishinda 2-0 mchezo wa kwanza, kabla ya kuibuka na ushindi mwembamba wa 1-0 kwenye marudiano. Ilikuwa nusu fainali ya Wataliano watupu, huku timu hizo zikionesha kuwa zinarudi kwenye ramani.
Hata hivyo Inter Milan wamepoteza mchezo wa fainali baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 toka kwa Manchester City ya Pep Guardiola. Haukuwa mchezo rahisi, Inter Milan walivuruga utulivu na uchezaji wa Man City na kuifanya fainali hiyo isiwe na mwenyewe. Licha ya matarajio kuwa Man City wangeweza kuisambaratisha Inter Milan, lakini kikosi cha Simone Inzaghi kilikuwa imara, kilipoteza nafasi nyingi za kufunga. Lakini Man City ya Pep Guardiola ilikuwa imara zaidi ya Inter Milan.
Fainali ya Europa League
Katika michuano hii miamba ya Italia pia ilikuwa imeshika hatamu. Kocha maarufu Jose Mourinho alikuwa anakiongoza kikosi cha AS Roma kucheza fainali ya Europa League. AS Roma walimenyana na Sevilla ya Hispania katika mchezo wa fainali wa Europa League. Mourinho alikuwa akiongoza kikosi cha AS Roma katika fainali ya pili mfululizo baada ya msimu uliopita kunyakua taji la Europa Conference League akiwa na miamba hiyo. Hii ilikuwa fainali ya kwanza kwa Jose Mourinho kupoteza. Katika maisha yake ya ukocha ameshinda fainali zote alizocheza isipokuwa Conference League. Hata hivyo aliongeza rekodi ya timu ya Wataliano kutinga fainali katika mashindano ya ulaya kabla ya kushindwa hatua ya matuta mbele ya Sevilla.
Serie A ndani ya Conference League
Ushindani uliooneshwa msimu huu katika mashindano ya Ulaya, timu za Serie A zina kila sababu ya kujivunia kuwa zimepiga hatua na kurudisha ramani ya soka la Kitaliano. Kwenye mchezo wa fainali ya Europa Conference League mimba mingine ya Italia, Fiorentina walichuana na West Ham United ya England. Katika mchezo huo West Ham ya David Moyes iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 na hivyo kutawazwa kuwa mabingwa wa Europa Conference League.
Kutoka Ligi ya Mabingwa, Europa League hadi Conference League unaona dhahiri kuwa Ligi Kuu Italia imeanza kurejesha makali yake ya miaka ya nyuma. Miaka hiyo iliyokuwa na miamba ya soka na iliyotikisa barani Ulaya na mashindano ya Kombe la Dunia.
Inter Milan waliocheza fainali ya Ulaya, kwenye ligi ya nyumbani wamemaliza msimu wakiwa nafasi ya tatu nyuma ya Napoli na Lazio. Hii ina maana msimu ujao Inter Milan watakuwa kwenye mashindano Ligi ya Mabingwa Ulaya sambamba na Napoli na Lazio, pamoja na AC Milan.
Vilevile umahiri wa Napoli unafahamika, licha ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu na AC Milan. Hata hivyo upo uwezekano wa timu za Serie A kufanya vizuri msimu ujao hasa kwa kuangalia namna walivyoshiriki msimu huu. Misimu kadhaa iliyopita timu nyingi za Italia zilikuwa hazina makali na zilichukuliwa kama vibonde kabla ya kuamka msimu huu.
Pep Guardiola ataweza?
Wakati akifanikiwa kuwafunga miamba ya Italia, Inter Milan kocha wa Man City amesema mbio za kusaka rekodi ya Real Madrid zinaendelea. Akizungumza baada ya mchezo wa fainali kumalizika huko Uturuki, amesema watu wasije kushangaa wanataka mataji 13 ya Ulaya, na safari yao imeanza kwa kutwaa taji lao la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Guardiola anaona mlima mrefu uliopo kuifikia rekodi ya Real Madrid kama kitu rahisi, lakini uhalisi wa mambo unasema je ataweza kufikia rekodi na kisha kuivunja? Huenda ikawezekana, lakini muda utazungumza.
Comments
Loading…