Kuna habari kwamba Liverpool wangependa kumsajili winga wa Arsenal, Theo Walcott na kuwapa The Gunners mshambuliaji wao, Raheem Sterling.
Mazungumzo kati ya Arsenal kumwongezea Walcott (26) mkataba hayajaanza na muda unaelekea ukingoni wakati baina ya Liverpool na Sterling (20) yalishindikana kwa mchezaji huyo kukataa dau jipya la mshahara wa pauni 100,000 kwa wiki.
Wakati Walcott amekanusha tetesi za kubwatukiana na Wenger huku kocha akisema mazungumzo yangeanza, aliachwa benchi muda wote wa mechi muhimu dhidi ya Liverpool wikiendi iliyopita.
Inaelezwa kwamba wawakilishi wa Walcott wanatarajia kufanya mazungumzo na Wenger wiki ijayo, ambapo mkataba wake umebakia msimu mmoja tu na akikataa ofa ataweza, msimu ujao kujadiliana na klabu yoyote, huku Chelsea wakimtaka.
Ni wazi kwamba Walcott angependa kupata muda zaidi wa kucheza, ambapo amekuwa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha na akiwa huko wachezaji wengine wakapanda viwango.
Hata hivyo, Wenger amenukuliwa akisema kwamba huu si wakati wa kuwauza wachezaji wao mahiri. Pia alidai kwamba suala la yeye kutaka kumsajili Sterling lilikuzwa na vyombo vya habari.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers kwa upande wake alidai kwamba Sterling hangeenda popote na kwamba ikiwa wamiliki wa timu wanataka abaki, atabaki hadi mkataba wake umalizike miaka miwili ijayo.
Sterling kwa upande wake, katika mahojiano na BBC wiki iliyopita alisema anapenda kucheza Arsenal na kwamba alifurahishwa kusikia akihusishwa na Gunners. Hakuwa ameruhusiwa kufanya mahojiano na Rodgers akasema alikosea lakini angejifunza maana bado mdogo.
Habari mpya ni kwamba huenda mazungumzo yakaanza baina ya klabu hizo, ambapo licha ya Arsenal kuwapa Liver Walcott watatoa pia pauni milioni 20 kujazia.
Msimu uliopita Arsenal walikuwa wakimtaka kwa udi na uvumba mshambuliaji wa kati wa Liverpool, Luis Suarez lakini akaamua kwenda Barcelona.
Inajulikana kwamba Rodgers ni shabiki wa jinsi Walcott anavyocheza na baada ya kujaribu kumzuia Suarez kuondoka, alitoa wazo la kubadilishana na Walcott na sasa hali kama hiyo inajirudia.
Starsport wanasema kwamba makubaliano hayo yakifikia, utekelezaji utafanyika kiangazi kinachowadia na kwa kufanya hivyo kila mchezaji ataridhika.
Rodgers ana wakati mgumu kumshawishi Sterling abaki Anfield, kwani chipukizi huyu mwenye asili ya Jamaica amesema anataka kwenda kwenye klabu inayotwaa vikombe.
Ilikuwa siku chache baada ya kusema hivyo alikabiliana na Arsenal na kufungwa 4-1 kwenye Ligi Kuu ambako Liverpool huenda wakashindwa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Timu zote mbili, hata hivyo, zimeingia nusu fainali ya Kombe la FA na zikishinda hatua ya wikiendi ya Aprili 18/19 zitakutana kwenye fainali Wembley na matokeo yanaweza kutoa ushawishi kwa Sterling.
Pamoja na hayo, kijana huyu angependa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambayo Arsenal wana nafasi kubwa zaidi kufuzu, kwani wapo nafasi ya pili msimamo wa ligi na Liverpool ni wa tano, kwa pengo la pointi tisa.
Walcott, kwa upande mwingine angependa kubaki Arsenal klabu aliyokulia tangu atoke Southampton kwani amejenga marafiki wengi lakini ikiwa atakosa namba itakuwa ngumu.
Inatambulika kwamba amekuwa akitaka achezeshwe kama mshambuliaji wa kati japokuwa hadharani husema angecheza kokote.
Ni ngumu kwake kupangwa hapo, ikizingatiwa ujio wa wachezaji Olivier Giroud aliyetokea kupanda kiwango sana na pia Alexis Sanchez na Danny Welbeck, achilia mbali uwapo wa chipukizi wengine.
Wenger aliposema Arsenal hawana shinikizo la kuuza tena wachezaji wao bora alipoulizwa juu ya madai kuwa Manchester City wanamtaka kiungo Jack Wilshere.
Nyota ambao Arsenal imewauza ni Robin van Persie, Emmanuel Adebayor, Samir Nasri, Gael Clichy na Bacary Sagna lakini katika miaka ya karibuni wameshuka viwango kwa kiasi kikubwa.
Wenger amedai walikuwa wakiwauza kwa sababu ya tatizo la fedha na sasa wanazo. Hata hivyo, hakuna sababu ya kukataa kumtoa mchezaji ikiwa unapata mzuri zaidi.
Comments
Loading…