KUFUNGWA katika mchezo wa fainali ya mashindano ya Mataifa ya Ulaya maarufu kama Euro ni jambo baya kwa England. Takwimu zinaonesha kwa miaka 27 England wamekuwa vibonde wa Italia katika mchezo wa soka.
Katika mchezo wa soka kabla ya fainali hizo kuna timu nyingi zimetolewa. Wachezaji wa timu zilizotolewa walilia na kurudi nyumbani wakiwa na majonzi. Hiyo ina maana wote walitaka kufika fainali na kuchukua kombe hilo. Kwa maana hiyo England licha ya kutochukua kombe hilo bado wamefanikiwa kufika fainali jambo ambalo ni mafanikio.
Chini ya Gareth Southgate tumeona England ikicheza kwa mafabnikio katika mashindano mbalimbali. Mwaka 1996 England waliandaa fainali za Euro lakini wakatolewa hatua ya nusu fainali na Ujerumani.
Mashindao ya Euro 2020 yalishirikisha majiji 11 kama njia ya kukumbukumbu ya kuanzishwa kwake tangu mwaka 1960. Hata hivyo rekodi za England kwenye mashindano miaka ya karibuni yanampa ahueni Gareth Southgate, ndio maana kiungo Jack Grealish amesema ni lazima kocha huyo aheshimiwe kwa sababu kwenye mashindano hayo tangu mwanzo hadi mwisho amefanya maamuzi mengi yaliyowafikisha kwenye mchezo wa fainali.
Kuna kitu cha kujivunia kwa Southgate na chama cha soka England licha ya shinikizo la mashabiki kutaka kombe la Euro. Jambo lingine lililojitokeza ni kuzomewa kwa wachezaji waliokosa penati kwenye mchezo wa fainali.
Marcus Rashford, Jadon Sancho na Bukayo Saka walikosa penati zao na kuinyima ushindi England. Lakini ushindi wa England umekosekana kwa sababu kundi zima la wachezaji halikumaliza kazi yao ndani ya dakika 90 ambapo wangeweza kufanya hivyo.
Ukiangalia kikosi cha England alichokuwa nacho Gareth Southgate utabaini kuwa nusu ya wachezaji wametokana na wazazi wahamiaji. Kama suala la damu za kuzaliwa England basi ni nusu ya wachezaji wao ndio walikuwepo kikosini.
Mifano, kiungo mshambuliaji Jakc Grealish kutoka Aston Villa, na Declan Rice kutoka West Ham wamezaliwa kwa wazazi kutoka Jamhuri ya Ireland, lakini wameamua kupeperusha bendera ya England. Hawa ni wachezaji wahamiaji.
Raheem Sterling ana asili ya Jamaica. Marcus Rashford ana asili ya Afrika. Bukayo Saka amezaliwa kwa wazazi wenye asili ya Nigeria. Kalivin Philips na Kyle Walker nao ni zao la wazazi wahamiaji. Hii ina maana hiki ni kizazi kipya cha England ambacho wazazi wao ni wahamiaji. Ni kizazi chenye uraia kytoka kwa wazazi wan je ya England.
Kwa maana hiyo England inatakiwa kuwaheshimu wachezaji hao wahamiaji ambao wametumia sehemu ya mapato ya mchezo wa fainali kuchangia sekta ya afya ili kuwawezesha watumishi ambao wanapambana kuhudumia wagonjwa wenye maambukizo ya ugonjwa corona.
Kama utazingatia kizazi cha dhahabu kati ya hiki alichokiongoza Gareth Southgate na kile kilichoongozwa na akina Glenn Hoddle, Sven Goran Ericksson utagundua tofauti kubwa. Kwanza kuanzia mitindo yao ya kucheza, vipaji na akili ya mpira imeonesha vijana hawa ni tofauti kabisa.
Soka la timu ya taifa ya England lilikuwa na kiugumu ugumu mno na wengi wachezaji wao walikuwa wagumu gumu. Chini ya Southgate tumeona kizazi kipya kikicheza kandanda maridadi na vipaji vyao vinajionesha bayana kuwa ni wachezaji wa aina tofauti.
Utofauti huo unaletwa kwa sababu wana damu za nje ya England, yaani watoto wa wahamiaji wenye uraia halali wa nchi hiyo. Zamani ulikuwa unaona Darius Vassel ndiyo winga wao, lakini hawezi kufikia hata robo ya kipaji cha Raheem Sterling au Jude Belligham.
Southgate ana vijana wa aina yake ambao wameonesha utofauti wa vizazi katika uchezaji wa mpira. Ninaamini ni wakati ambao England wanatakiwa kujiamini zaidi kwa kizazi hiki kuliko kuwaponda au kuwabagua. Nchi yao imejaa vipaji vya wahamiaji ambao ni raia halali.
Kwahiyo kuwagawa kwa msingi wa rangi haiwezi kuwafanya wawe na msuatakabali wa peke yao wakati walipokuwa na kizazi chenye damu zao hakikuwa na vipaji vya kutisha kama hawa vijana wa sasa. Wachezaji wenye damu zao kamwe hawataweza kufika pale ambapo Southgate amewafikisha.
Kwahiyo lazima tukubali kuwa kizazi hiki cha England cha sasa wanatakiwa kujivunia kwa kile walichokifanya, na inawezekana wakawa na mafanikio kwenye michuano ya kombe la dunia ikiwa wataendelea kubakizwa na kuaminiwa hivi hivi.
Na zaidi ikiwa Southgate atabakia kuwa kocha maana yake atakuwa ameimarisha mbinu zake kwenye michuano ya kombe la dunia ambako kunakuwa na mataifa mengi ambayo wanaweza kuyatumia kama ngazi kupata mafanikio.
Tofauti ya Kombe la dunia na Euro, ni kwamba kwenye Euro mataifa hayo yanafahamiana zaidi katika kandanda, lakini kwa kombe la dunia kila kitu kinakuwa kigeni kuanzia utamaduni,mitindo ya kucheza na hata vipaji vya wachezaji na viwango hutofautiana.
Nazidi kusisitiza England wanatakiwa kujivunia kizazi hiki kuliko kukitupia kila aina ya matope. Umri wao unawaruhusu kuendelea kutesa kwenye soka ikiwa kutakuwa na mwendelezo wa kocha mwingine akafuata kukiendeleza kikosi chao.
Southgate si kocha wa mashabiki ambaye anaweza kushawishiwa kuwaita wachezaji wazee na maarufu tu, ameonesha taofauti kwenye uongozi wake. Na kama ataachwa aendelee anaweza kuwatengenezea England kizazi kizuri cha kandanda.
Comments
Loading…