in

Makipa Euro, Pickford ni kinara wangu

Jordan Pickford

MAKIPA wanne katika mashindano yaliyomalizika Julai 11 mwaka huu ya EURO 2020 walikuwa katika orodha yangu ya wachezaji waliofanya vizuri. Walikuwa Jordan Pickford (England), Rui Patricio (Ureno), Yann Sommer (Uswisi) na Gianluigi Donnaruma (Italia). 

Kwa mara ya kwanza nimevutiwa na namna mchezaji wa England alivyowajibika uwanjani. Aliyenivutia zaidi ni golikipa wao, Jordan Pickford anayekipiga katika klabu ya Everton nchini humo. Sina uhakika kama klabu yake ya Everton ya England wataweza kumbakisha nyanda wao  katika timu yao msimu ujao, kwa sababu naona wazi anaweza kwenda timu kubwa zaidi zenye kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya au Europa League. 

Golikipa wa waliokuwa mabingwa watetezi Ureno, Rui Patricio alinivutia lakini hakufua dafu mbele ya watatu hao. Pia golikipa wa Uswisi Yann Sommer alinivutia kwa uhodari wake kwenye mchezo dhidi ya Hispania, ambapo alipangua hataru 10 na penati moja ya La Roja kwenye hatua ya kuamua mshindi wa matuta. 

Hata hivyo Sommer hakupewa zawadi ya mchezaji bora wa mechi ya Uswisi na Hispania, ambapo golikipa wa Unai Simon wa Hispania alinyakua tuzo hiyo na kutamka maneno yafuatayo wakati akizungumza na vyombo vya habari baada ya kukabidhiwa, “Niwe muungwana, hii tuzo ilipaswa apewe Yann Sommer,”

Nafasi ya golikipa inakuwa na mambo mengi ya kutazama; uwezo wa kukabiliana na wapinzani, kupanga safu ya ulinzi,kuibeba timu nyakati ngumu,uwezo wa kuanzisha mashambulizi pamoja na uwezo wa kukabiliana na wpaigaji penati. 

Pickford si sawa na makipa wengine maarufu wa England, kama Gordon Banks, David James au David Seaman. Hata golikipa msaidizi wake Johnstone naye alionesha umahiri katika mchezo wa kirafiki na ulionesha wazi atakuwa moto wa kuotea mbali siku zijazo. 

Kama ningeambiwa nielezee udhaifu wa nyanda Pickford, ningepewa jukumu la kumpa neno, basi ningesema anatakiwa kuimarisha uwezo wake wa kukotroo mipira tu. Pickford hana zile ‘touch’ kama za Manuel Nueur au Ederson. Pickford hana uhuru wa kukokota mpira kama waliona0 Wajerumani wawili Nueur na Ter Stegen.

Tofauti iliyopo ni kwamba Pickford ameonesha kutoa amri, kuhamasisha,kukumbusha,kuelekeza na kujitoa mhanga. Kati ya wachezaji ambao wametokwa jasho jingi nyakati ngumu Pickford ni mmojawapo. 

Unaweza kusema labda alikuwa safu imara ya ulinzi, kuanzia Harry Maguire,John Stones,Mings,Kyler Walker,Luke Shaw lakini umahiri wake umeonekana katika vipindi vyote vya dakika 90,120 na wakati wa kupiga penati. 

Pickford namna anavyoanzisha mipira, anavyookoa na kupangua mashuti hatari ilisisimua kumtazama uwanjani. Labda eneo moja ambalo hakuonesha umahiri ni kupangua kwa kutumia miguu. Eneo hilo ndilo linawapa nafasi akina Donnarumma,Manuel Nueur na Sommer. 

Hata kwenye suala la penati, England sidhani kama wamewahi kuwa na nyanda anapangua penati kama Pickford. Nimewashuhudia David James, hakuwa hodari kama Pickford. Nimemshuhudia David Seaman, hakuwa mahiri kama Pickford. Sidhani kama Godon Banks pamoja na sifa zake zote kama alikuwa na uwezo kama Pickford.

Kwangu Pickford anakuwa nyanda ambaye amenishangaza kama nilivyokuwa nashangaa kipaji cha Jack Wilshere ambaye majeraha yamemaliza kipaji chake cha soka.

Pickford nilitarajia angeibuka kuwa mchezaji bora wa mashindano haya. Lakini shirikisho la soka la Uropa lilimpatia tuzo hiyo Gianluigi Donnarumma. Ukweli ni kwamba mshindi wa mchezo au tukio huchukua vyote; hivi ndivyo ilivyotokea kwa Donnarummma. 

Kama England wangetwaa taji la Euro 2020 tuzo ya mchezaji bora bila shaka ingekwenda kwa Pickford. Pana sifa nyingine muhimu ambayo ilikuwa inampa ushindani Donnarumma; kwamba Pickford alikuwa amefungwa bao moja tu hadi siku ya fainali. Kwahiyo bado la kusawazisha la Leonardo Bonucci kwa Italia katika mchezo wa fainali pale Wembley lilikuwa la pili kufungwa Pickford. 

Hii ina maana lango la Pickford lilikuwa imara katika mashindano yote na kuruhusu nyavu zake kutikishwa mara mbili ni ishara ya uimara. Hapo hapo amefanikiwa kupata ‘cleansheet’ za kutosha. Ni sababu tosha kwangu kuamini Pickford ndiye alikuwa mchezaji bora wa mashindano hadi dakika 120 zilipokwisha. 

Na hata zilipoanza dakika za kupiga matuta, Pickford aliibeba England kwa umahiri wa hali ya juu ukizingatia alizuia penati ya mpigaji mahiri Jorginho. 

Kiungo huyo Mtaliano ni kama ‘muuaji’ wa mwisho linalofika suala la upigaji wa penati. Amefanya hivyo mara nyingi na kuipa Italia ushindi na kusonga mbele. Hata hivyo Jorginho alikwama mbele ya umahiri wa Jordan Pickford. 

Baada ya kudaka penati ya Jorginho tuliona wazi jinsi alivyoshangilia na kwa sababu kuu ilikuwa kuirudisha England mchezoni yaani kuendelea kwenye hatua ya matuta na kuwapa ari zaidi wenzake. Umahiri ule sijawaon kuuona kwa David James,David Seaman na makipa wengine wa England katika ulimwengu wa soka.

Pickford alicheza dakika 722 bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa na kuvunjilia mbali rekodi ya Gordon Banks. Kwahiyo kila nikirejea mipambao aliyokaa langoni nauona umahiri ambao unawapa nafasi England kujivunia naye. Kwangu mimi alikuwa nyanda wangu hodari na mshindi wa mashindano ya Euro 2020.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Raheem Sterling

Waingereza wajivunie kizazi hiki

Timu ya Taifa ya Italia

Mkuu wa waamuzi amzungumzia Sterling