in , , ,

Waarabu wameshtuka nini kwa soka la Ulaya?

KUNA nini? Ndilo swali ambalo linapaswa kuulizwa sasa juu ya hatua ya Matajiri wa Kiarabu kugeukia soka la nchi zao. Miaka miachache iliyopita matajiri wengi wa Kiarabu walikuwa wanahaha kupata nafasi ya kudhamini timu mbalimbali zianzoshiriki Ligi za Ulaya. Kuanzia Hispania (La Liga), England (EPL), Italia (Serie A), Ujerumani (Bundesliga) na Ufaransa (Ligue 1). Timu nyingi zilikuwa zinadhaminiwa na makampuni ya kutoka kwa matajiri wa Asia hasa nchi za Kiarabu. Baadhi ya nchi kama Malaysia,Indonesia,Singapore zilikuwa zinatamba kwenye udhamini, lakini matajiri wa Saudi Arabia, Qatar walikwenda mbali zaidi katika udhamini wao. Matajiri wenzao walikimbilia kununua timu hizo, miongoni mwake ni Liverpool na Manchester United, pamoja na Chelsea iliyouzwa kwa bilionea wa Kirusi, Roman Abromavich. 

UDHAMINI WA KAMPUNI MOJA

TANZANIASPORTS katika uchunguzi wake wa meizi sita umebaini kuwa wakati mabilionea wa Marekani wakimiliki timu, wenzao wa Asia walikuwa wakidhamini tu. Iliwezekana kampuni ya kiarabu au kutoka Asia ikadhamini timu nyingi barani Ulaya, kwa mfano Real Madrid, Arsenal,AC Milan,PSG, na baadhi ya timu toka Ujerumani zimo chini ya mdhamini mmoja. Hali kadhalika matajiri wa Qatar nao walivamia soko la udhamini hapo awali, kisha wakaingia upande wa pili kununua klabu za soka ikiwemo PSG ya Ufaransa.

UNUNUZI WA NEWCASTLE NA MAN UNITED

Tanzania Sports

Katika uchunguzi huo TANZANIASPORTS imehitimisha kuwa miaka ya hivi karibuni matajiri wa Saudi Arabia waliokuwa wakihangaika kuinunua klabu ya Newcastle United huenda kumewabadili mtazamo wao kuhusu fedha zao na soka kwa ujumla bila kujali nguvu ya soka la Ulaya kwa Dunia. Ununuzi wa Newcastle United ulijaa siasa nyingi na vita vikali vya nje ya uwanja pamoja na kisheria, kutokana na masharti kadhaa. Vikwazo vingi walivyokutana navyo kutoka serikali ya England ni miongoni mwa mambo ambayo yanaweza kuwabadili mitazamo mabilionea wa kiarabu. Upande mwingine sakata la ununuzi wa klabu ya Manchester United limekuwa mfupa mgumu huku familia ya Malcolm Glazer haionekani kuachia kwa urahisi. Ofa mbalimbali zilizotolewa, ikiwemo bilionea mwingine wa Kiarabu kutoka Saudi Arabia zimekosa kukubaliwa na familia ya Glazer kwa kile kilichoitwa kutokidhi matakwa yao. Vikwazo hivi vimewafanya waarabu aangalie namna nyingine ya kutamba kwenye mchezo wa soka.

FAINALI ZA KOMBE LA DUNIA

TANZANIASPORTS imebaini sababu nyingine ni mashindano ya Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2022 yaliyofanyika nchini Qatar. Uzoefu wa kuandaa fainali za Kombe la Dunia, shughuli nzima ya uendeshaji wa soka pamoja na elimu waliyopata huenda ikawa imewabadili Mabilionea wa Kiarabu na kampuni zao kubadili mwelekeo. . Fainali hizo za Qatar zimeleta hamu na ghamu kwa mabilionea wa Qatar kuamua kubadili mwelekeo wa kushughulika na soka. Ilikuwa mara ya kwanza kwa taifa la Kiarabu kuandaa fainali za Kombe la Dunia. Licha ya mashambulizi mengi yaliyoelekezwa kwa Qatar lakini shirikisho la soka duniani liliziba pamba masikioni na kuendeleza mipango hadi michuano hiyo ilipomalizika. Michuano hii imekuwa darasa kwa serikali za nchi za kiarabu na mabilionea wao. Hivyo zimetoa mchango mkubwa wa mabadiliko yanayoendelea sasa.

FEDHA ZA MAFUTA

Upepo unaobadilika sana, ambapo Matajiri wa Asia wanaelekea kuondoka kwenye soka la Ulaya. Badala ya kumiliki timu za Ulaya, wanalekea kuimarisha timu zao. Fedha za mafuta ndizo zinazowapa kiburi na wameamua kufanya biashara kupitia mpira wa miguu. Fedha walizopata kwenye fainali za Kombe la Dunia zimewanogea na sasa vilabu vya nchi za Kiarabu vimeanza matanuzi sokoni. Nchi inayonufaika zaidi kwenye upepo huo ni Saudi Arabia. Maelfu ya wachezaji kutoka Ulaya wanahamia Ligi Kuu ya nchi hiyo maarufu kama Saudi Pro League (SPL). Badala ya kuendeleza kuhangaika kuzitafuta klabu za kumiliki kama Manchester United, mabilionea hao wanavuta wachezaji walioko Ulaya kwenda kucheza soka katika ardhi ya Kiarabu. Kwa ukiritimba wa kununua timu za EPL ulivyotanda na kudhibitiwa na serikali ina maana mabilionea wa kiarabu wameamua kubakisha fedha zao nyumbani. Wanawavutia wachezaji wakacheze Saudi Arabia. Qatar nao wanaelekea kuamka licha ya kuwa wenyeji wa  Fainali za Kombe la Dunia. Qatar wanamiliki timu ya PSG ya Ufaransa, na sasa wameanza hekaheka kama za Saudi Arabia kwa kuinua soka lao kuwavutia wachezaji toka Ulaya.

CRISTIANO RONALDO NI CHAMBO

Tanzania Sports

Tathmini ya TANZANIASPORTS inaonesha kuwa barani Ulaya Cristiano Ronaldo amefanya kila kitu. Amecheza Ligi Kuu ya kwao Ureno, akahamia England na kutamba katika kikosi cha Manchester United, kisha akaelekea Real Madrid ya Hispania. Ametwaa makombe muhimu ngazi ya klabu na timu ya taifa. Kwa sasa Ulaya ni kama walikuwa hamhitai Roinaldo. Lakini mabilionea wa Kiarabua wamemchukua na kukuza mvuto wa Ligi yao. Ronaldo amekuwa chambo cha kuvutia mastaa wengine. Hakuna aliyetarajia nyota wakali na wenye majina makubwa wakahamia Ligi Kuu Saudi Arabia. Hakuna aliyedhania nyota wa Senegal aliyekuwa akikipiga Bayern Munich, Sadio Mane kama angejiunga Al Nassr anayocheza Ronaldo. Haikuwa ikitarajiwa kumwona nahodha wa Liverpool, Jordan Henderson akiondoka kwa majogoo hao na kwenda Saudi Arabia kwa ushawishi wa fedha za Waarabu. Steven Geard kocha kijana kabisa, pamoja na staa mwenzake wa zamani pale Liverpool, Robbie Fowler wote wamekwenda Saudi Arabia kufuata marashi na fedha za Waarabu. Wachezaji kutoka mataifa mengine ya Amerika kusini kama vile Brazil, imeshuhudia nyota Neymar Junior akiondoka PSG kwenda Saudi Arabia, kisha kiungo wa kutajika Fabinho naye ameondoka Liverpool. 

NYOTA WAPYA

Wachezaji wengine waliokuwa wanatamani kucheza Ulaya wanabadilika sasa na kuangalia macho kwenye fedha za Waarabu. Ule mvuto wa kwenda ulaya utabki kuwa nguvu ya historia ya timu na sifa za umahiri wa  wachezaji lakini huwezi kupuuza nguvu ya fedha ya waarabu. Nguvu ambayo imezinunua timu za Ulaya na kutamba kisha wamaeamua kubakiza fedha zao kwenye ardhi yao na kuwavutia nyota wa nchi mbalimbali waende kwao. Hii ni biashara ambayo serikali za nchi za Kiarabu zinawaunga mkono mabilionea wao kusajili wachezaji kwa gharama ya kufuru ambayo haijawahi kutokea. Nyota wapya wataanza kulitazama soka la nchi za Kiarabu kama sehemu ya kwenda kuchota fedha. Inawezekana huenda kukawa hakuna miundombinu mikubwa kama ya Ulaya lakini waarabu fedha wanazo, wameajiri wataalamu kutoka huko huko Ulaya. Hawashindwi lolote.  

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Eric Ten Hag amekosea..

Tanzania Sports

Kutoka Manchester hadi Mwanitesa United