in , , ,

Vilabu vyetu vinaajiri falsafa za kocha au wasifu?

Katika Ligi Kuu Tanzania makocha Charles Boniface Mkwassa na Fred Minziro wanafahamika kwa falsafa yao ya kutandaza kandanda kiufundi…

KUAJIRI kocha wa mpira wa miguu ni moja ya mambo yanayochanganya mashabiki na viongozi wengi nyumbani Tanzania. Inafahamika kuwa kila kocha anayeajiriwa katika timu anakuwa vigezo vinavyotakiwa na waajiri. Kwa mfano uongozi wa klabu yangu ya Arsenal ulipomwajiri Mikel Arteta ulijua sifa zake lakini kuna kingine cha zaida, nitawaambia baadaye. 

Vilevile wakati Alberto Carlos alipoajiriwa kuwa kocha wa Bafana Bafana kuelekea fainali za Kombe la Dunia alikuwa na sifa zake. Jose Mourinho alipoajiriwa mara ya kwanza Chelsea alijulikana kwa sifa zake. Hata sasa akiwa kocha AS Roma anafahamika kwa sifa yake. 

Hali kadhalika Yule gwiji aliyeipaisha Senegal kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002 Bruno Metsu anajulikana kwa sifa zake. Hilo lipo pia kwa Pep Guardiola, Zinedine Zidane, Pitso Mosimane,George Lwandamina, Roberto De Zebri, Boniface Mkwasa, Fred Minziro,Seleman Matola na makocha wengine. 

Tanzania Sports

Nafahamu kigezo ama sifa ya kuajiriwa ukocha wa klabu fulani lazima uwe na vyeti halisi. Kitu kingine kinachotakiwa ni wasifu wa kocha anayetakiwa kuajiriwa katika klabu yoyote duniani. Hivyo basi, kila uongozi wa klabu au chama cha soka unajua sababu za kumwajiri mwalimu fulani kuwa kocha wa Timu ya Taifa au ngazi ya klabu. 

Kwa mfano, Waholanzi wamepata nafasi ya kuwa na makocha wazuri sana akiwemo Louis van Gaal na Frank Rijkaard. Wawili hawa kwa nyakati tofauti waliwakochi Barcelona. Sifa zinazompa kocha nafasi ya kuchukuliwa na timu fulani ndizo zinafahamika zaidi kwa mashabiki kote duniani. 

Mashabiki wanataka kujua kocha huyo alishinda ubingwa gani, mfano wa Ligi Kuu, Klabu Bingwa, Kombe la Shirikisho au mashindano yoyote anayoshiriki. Hiyo ni sifa inayowekwa kwenye wasifu wake. Viongozi wanaweza kusoma wasifu huo na kukutana na makombe kedekede au kiasi fulani cha ushindi. 

Hata hivyo ipo njia nyingine inayotumiwa kuajiri makocha. Hii ndiyo njia ambayo haina umaarufu miongoni mwa mashabiki wa mpira wa miguu nyumbani Tanzania. 

MBINU NA FALSAFA ZA MAKOCHA

Kwa mfano, Jose Mourinho anapoajiriwa kufundisha timu yoyote anafahamika mbinu zake. Hili la mbinu za kusaka ushindi ndilo linalochukua nafasi kwa viongozi makini na wenye uelewa na weledi katika mchezo wa mpira wa miguu. Mbinu na falsafa ya kocha ni kigezo muhimu cha kutumia pale viongozi wanapoajiri mwalimu yeyote. 

Unafahamu kabisa Jose Mourinho akiajiriwa kufundisha Barcelona maana yake utambulisho wao wa falsafa ya Tikitaka utapoea. Mourinho anafahamika wazi wazi mbinu zake za kujihamia kama zile za Bruno Metsu. 

Hali kadhalika Marcio Maximo alizitumia mbinu hizo. Kwahiyo njia ya kumpata kocha mzuri hapo si kuangalia wasifu (CV) yenye makombe bali kujali msingi wa falsafa ya timu. Kocha anayeajiriwa kufundisha Klabu ya Simba anatakiwa kufahamu bayana falsafa ya timu.

Hili ndilo linalowapa nafasi viongozi makini kuelewa msingi wa ufundishaji wa mwalimu yoyote. Mikel Arteta ni kocha ambaye anafuata misingi ya ufundi wa mwalimu wake wa zamani Arsene Wenger, lakini ameongeza kasi ya mchezo kuwa kubwa kuliko wakati wa Wenger. 

Kwahiyo uamuzi wa Mkurugenzi wa Michezo wa Arsenal, Edu Gaspar kuwashawishi Bodi ya klabu hiyo kumwajiri kocha huyo wakati akiwa Msaidizi wa Guardiola pale Man City kilichoangaliwa ni falsafa yake. Uongozi unatumia falsafa ya mwalimu kama njia ya kumtaka kuwa kocha wao. 

Vilevile unapomwajiri Pep Guardiola kuwa kocha wa klabu yako au Timu ya Taifa unafahamu kabisa mbinu na falsafa zake  zilivyo na namna timu inanvyocheza. Msingi huo unawapa nafasi wataalamu wa ufundi kubaini mambo mazuri ya kifalsafa na mbinu za makocha wanaotakiwa kuajiriwa. 

Makocha wanaajiriwa ili kulinda,kuendeleza na kukuza uwezo kutoka kwenye falsafa yao katika kutafuta mafanikio. Katika Ligi Kuu Tanzania makocha Charles Boniface Mkwassa na Fred Minziro wanafahamika kwa falsafa yao ya kutandaza kandanda kiufundi. Sisemi wao ndio wanastahili kufundisha vilabu vya Tanzania badala yake wanaweza kutazamwa kama mifano ya makocha wanaotakiwa kuajiriwa. 

KUACHANA NA CV

Tanzania Sports

Wasifu wowote wa makocha wenye mafanikio lazima uwe na mbinu na falsafa. Lakini viongozi wa vilabu vingi Tanzania huangalia wasifu peke yake ili waweze kujitetea mbele ya mashabiki. Hii ni dosari ambayo viongozi wa vilabu kongwe wanatakiwa kujifunza. 

Kiwango cha Yanga na Simba hawapaswi kukaribisha makocha wala kutazama CV zao, badala yake wanatakiwa kuwafuata wale ambao wanaendana na falsafa ya timu zao. Kocha aajiriwe Simba ili kuendeleza falsafa inayotumika na utambulisho halisi wa soka la Simba. 

Hali kadhalika Yanga nao hawapaswi kuingia kwenye mkumbo wa kukaribisha CV za makocha kwenye klabu yao kupata mrithi wa Nasreddine Nabi badala yake waende kwa Yule kocha wanayehisi anamudu kuendana na falsafa yao. Kinyume cha hapo kila mara watakuwa wanatimua makocha kwa sababu kuangalia CV peke yake. Makocha waangaliwe mechi za timu zao zinavyocheza. Kwa sababu uchezaji wa timu hizo ni maelekezo ya Mwalimu wao. 

Ni muhimu makocha wanaoajiriwa vilabu vya Ligi Kuu Tanzania kuangaliwa kwa misingi hii ya falsafa na mbinu za kuyafikia mafanikio. Kuketi ofisini kusubiri CV za makocha zije ni mtindo wa kubabaisha. CV kubwa lazima iambatane na mbinu na misingi ya klabu husika katika kucheza mpira. 

Zama za kungojea makocha wa kuleta CV ni kiini cha kujutia baadaye kwenye mchezo wa soka. Yanga,Simba, Azam, Mtibwa Sugar na nyinginezo ziwajue aina ya makocha wanaowahitaji sio orodha ya mambo yaliyoandikwa kwenye CV. Wafahamu aina ya walimu wanaostahili kuzinoa timu kwa kuhuisha misingi yao ya kifalsafa.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Presha kubwa Kocha mpya wa Yanga

Tanzania Sports

Makocha wa Ulaya wanatoka kichwani mwa Pep Guardiola