SAHAU habari ya kikosi cha vijana wadogo wa Simba kilichotengenezwa mwaka 1971 na kufanya makubwa mwaka 1974, kuna vikosi vinne vya Yanga na Simba vilivyotengenezwa kisayansi na matunda yake kuonekana. Kuna viwili vya Yanga na viwili vya Simba.
Vya Yanga ni kile kilichotengenezwa mwaka 1972 na kingine cha mwaka 1995 huku vya Simba ni kile cha mwaka 1977 na hiki kinachoanza kupewa uwajibikaji mkubwa mkubwa sasa.
Vijana ndani ya Simba 1971
Baada ya Yanga kubeba ubingwa wa Tanzania mfululizo tangu mwaka 1968, mwaka 1971, Sunderland, walionza kuitwa Simba mwaka huo, jina alilowapa Mheshimiwa Abeid Aman Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar, walijiuliza hali hiyo ya kutawaliwa na Yanga ingeishaje. Wakapata jibu ambalo ni kusuka upya kikosi chao kwa kuingiza vijana wengi.
Waliingiza vijana wadogo kina Haidar Abeid, Khalid Abeid (hawa hawakuwa ndugu ingawa wote walikuwa waarabu- Haidar wa Shinyanga na Khalid wa Mwanza). Aliingizwa pia kijana Abdallah Kibaden na kijana Willy Mwaijibe. Vijana wengine walichukuliwa toka Morogoro nao ni kina kipa Iddi Salum, mabeki Shaaban Baraza na Omari Choggo pamoja na mshambuliaji aliyekuwa na nguvu Adam Sabu.
Iliwachukuwa miaka miwili vijana hawa kukomaa na kucheza kitimu ya ushindani kwani mwaka 1973 walivunja mwiko wa Yanga wa ubingwa wa mfululizo kwa kuubeba ubingwa wa Tanzania wakiwa wameongezewa nguvu ya vijana wengine kina kipa Athumani Mambosasa na winga machachari Abbas Dilunga.
Mwaka 1974 walibeba ubingwa wa Afrika Mashariki wakiwa na nguvu ya vijana wapya kina Saad Ally toka African Wanderers ya Iringa pamoja na Athumani Juma, Aloo Mwitu na Hamis Ally “Askari” toka Lake Stars ya Kigoma waliyotoana nayo jasho jingi kwenye fainali ya ubingwa wa Tanzania mwaka 1973 na Simba kushinda 2-0 kwa mabao ya Willy Mwaijibe.
Ni vijana hao ndiyo walioifikisha Simba kwenye nusu fainali za ubingwa wa Afrika mwaka huo 1974 na kuzuiwa kwa fujo na vitisho na Mehalla El Kubra ya Misri kuingia fainali. Hapa nyumbani Simba walishinda 1-0 kwa bao la dakika ya mwisho la Saad Ally kufuatia kona ya dakika hizo.
Kwenye marudiano, Simba walilala 1-0 na dakika 30 za nyongeza hazikuzaa bao. Kwenye penalti tano tano zilizopigwa katikati ya vitisho, Simba walikosa tatu mwanzo za Kibaden, Sabu na Mohammed Kajole na Mehalla kupata zote tatu za mwanzo, Mambosasa akiwa kasimama tu katika kuogopa wachezaji wa Simba kuuawa kama wangefanya lolote la manufaa kwa timu yao (Sabu, Kajole na Mambosasa kwa sasa ni marehemu).
Hiki kikosi kimewekwa kwenye kumbukumbu hii kuonesha umuhimu wa kutengeneza timu imara ya vijana kwa matunda ya kupatikana baada ya miaka kadhaa. Hawa walianza kujengwa mwaka 1971 lakini matunda yake yakavunwa 1974. Sasa hivi soka ya nchi yetu inalazimisha mafanikio kijinga kabisa kwa kubadili vikosi kila mwaka.
Tofauti na vikosi vinne vinavyohusu kumbukumbu hii, hiki cha Simba cha 1971-74 kilitengenezwa kwa vijana toka timu tofauti za sehemu tofauti za nchi. Hivyo vinne ni vya vijana wa kuanzia Yanga na Simba na ndiyo maana mazungumzo haya yameanza kwa kushauri mambo ya kikosi hiki cha Simba cha 1971-74 yasizingatiwe sana katika madhumuni ya mazungumzo haya.
Yanga Kids 1972
Hii ni timu ya watoto ya Yanga iliyoanzishwa na uongozi makini wa Yanga ya Mwenyekiti Mangara Tabu Mangara, uongozi uliyoifanyia Yanga mambo makubwa kuliko uongozi wowote wa klabu hiyo kwa kipindi chote cha uhai wa klabu hiyo; kuwa na kocha mwenye sifa aliyefanya kazi kwa uhuru, ziara za mafunzo nje kama Rumania na Brazil na mialiko ya timu nyingi toka nchi za soka kama Brazil ikiwemo ziara ya hii hii Aston Villa ya Birmingham Uingereza mwaka 1973.
Mafanikio mengine ni kujenga jengo la klabu mwaka 1972 na uwanja wa Kaunda 1974, umiliki wa mabasi sita ya klabu na kutengeneza timu bora. Ni uongozi huo ndiyo uliokamilisha kumleta Pele na timu yake ya Santos ya Brazil hapa nchini, mpango uliovurugika baada ya serikali kuingilia kwenye dakika za mwisho. Yaani hili lingefanyika leo lingekuwa kumleta Lionel Messi na timu yake ya Barcelona. Pele kwa dunia wakati huo alikuwa kama Messi kwa dunia wakati huu.
Katikati ya mafanikio hayo ya uongozi huo usio wa kisomi uliofanikisha mambo bila kutazama runinga, bila simu za mkononi, fax, barua pepe na kadhalika, ndipo kilianzishwa kikosi cha watoto chini ya kocha Victor Stanculescu wa Rumania ambaye kwa sasa ana uraia wa Marekani.
Kikosi hicho cha watoto kilitengeneza wanasoka wakali wa baada ya hapo kama kipa Juma Pondamali, Jaffar Abdulrahman, Mohammed Mkweche, Mohammed Rishard Adolph, Bona Max, Gordian Mapango, Mohammed Yahya “Tostao”, Kassim Manara na wengine. Utaratibu ulikuwa kuwapandisha kidogo kidogo wachezaji hao ambapo Bona Max alitangulia kupandishwa, kisha wakafuata Adolph na kipa Pondamali.
Ni kwa bahati mbaya sana Yanga haikunufaika sana na wachezaji hao kwani mwaka 1976 wale waliokuwa wamepandishwa tayari kama Pondamali, Jaffar, Adolph na wengine wachache walifukuzwa pamoja na wachezaji wengine wa kikosi cha kwanza kama ilivyowahikukubushiwa hapa hivi karibuni.
Waliobaki wakaajiriwa na kampuni ya bia kuchezea timu ya Tanzania Breweries. Hao walifuatwa na wenzao waliokacha kujiunga na Nyota ya Morogoro na wakubwa zao waliofukuzwa nao. Wakaenda Breweries kujiunga na vijana wenzao.
Ilipoanzishwa na kina Mzee Mangara Pan African mwaka 1976 mwishoni kabisa ikichukua wachezaji wote walioenda Nyota Afrika isipokuwa kipa Patrick Nyagga ambaye alikwenda Mseto badala ya Nyota Afrika, wachezaji hao vijana wote waliitosa Breweries na kujiunga na Pan African.
Kwa kipindi walichoichezea timu hiyo waliifanyia makubwa mno ikiwemo kuipa ubingwa wa nchi hii huku taifa likinufaika na mchango wao kwa timu ya Taifa ambapo Manara na Tostao waliwahi kuihudumia timu hiyo wakitokea Ulaya walikokuwa wakicheza soka ya kulipwa. Tuliona magoli ya tik-tak ya wote wawili wakionesha kwa vitendo thamani ya soka ya kulipwa.
Hiki ndicho kikosi cha kwanza kati ya vinne vya Yanga na Simba vilivyotengenezwa kisayansi. Tutaona kuhusu vikosi vingine kwenye sehemu zifuatazo za makala hii.
——-
Kwa wale wanaochukuwa kazi za watu-tafadhali toa credit, tunatumia pesa kupata hizi taarifa.
Comments
Loading…