Tuchukue suala lililovuma sana katikati ya juma hili England
Mara nyingi kelele zozote zinapopigwa kwetu vingo’ra vya polisi na FFU husikika na wananchi kunyamazishwa. Haya hutokea shauri viongozi wetu wengi Afrika ni watu wa mabavu, wengine wamekaa madarakani zaidi ya awamu mbili zinazotakiwa. Afadhali Watanzania tuna uungwana.
Tukirejea mada yetu ya michezo maana hii ndiyo burudani tunayoipenda hutokea pia mambo yasiyofaa. Kiundani dunia ya michezo ni maendelezo ya kila kitu kilichoko katika jamii yaani biashara, siasa, tabia, mila na desturi.
Utafiti uliofanywa na BBC ulikiri kwamba malipo ya tikiti kuingia mpirani yanawalalia sana washabiki na wapenzi wa klabu. Utafiti huo ulioitwa “Bei ya Mpira” (Price of Football) uliangalia vilabu 227 katika michuano 13 ya ligi za kitaifa.
Mbali na tikiti, utafiti uligundua kuwa vitu vingine vinavyopendwa kununuliwa na wapenzi wa timu kubwa kubwa kama jezi ulikuwa juu sana ukilinganisha na vipato vya watu na hali ya uchumi. Mpambe mmoja wa timu ya Manchester United mathalan alipoulizwa fulana aliyovaa ya timu hiyo anayoifagilia ni bei gani akasema ni £50 ( karibu shilingi laki moja na nusu). Lakini mshabiki huyo huyo alidai hata bei isiposhuka mwaka ujao ataendelea kununua tu jezi za Manchester United!
Bei za kuingia mipira mikubwa zilianzia £30 hadi £65 (Shilingi laki moja hadi laki mbili). Malalamishi yaliyofanywa yalisikitishwa na namna klabu zinavyopata fedha nyingi na kuwalipa wachezaji, wakala na mameneja mishahara minono. Kila mtu hulalamika namna wacheza mpira wanavyolipwa fedha nyingi kupindukia.
Karibuni klabu ya Manchester City imetangaza faida ya zaidi ya paundi milioni kumi ( shilingi laki milioni tatu na uchafu juu) katika kipindi cha mwaka 2014 na 2015. Kiasi hicho cha faida kinakaribia mshahara wa mshambuliaji Sergio Aguero (anayelipwa paundi milioni 11.7 kwa mwaka). Mwenzake toka Ivory Coast, Yaya Toure, hulipwa zaidi ya paundi milioni moja kwa mwezi.
Kifupi wachezaji wanavuna fedha nyingi zinazotokana na washabiki kama huyo aliye tayari kununua fulana ya shilingi laki moja na nusu kila mwaka hata kama mshahara wake haumtoshi.
Lakini kuna walioona mambo haya si sawa.
Kuna klabu zinazofikiria zaidi mapenzi ya washabiki na kuonesha kujali.
Klabu ya Everton iliamua kutopandisha bei ya kuingia mpirani na kuiacha vile vile ilivyokuwa mwaka jana. Kwa sasa Everton imeshikilia nafasi ya saba katika Ligi ya England. Wanajitahidi.
Hata hivyo malalamishi bado yanaendelea.
Malalamishi yapo pia katika makocha wanaokataa hali ya klabu kubwa kama Manchester City na Chelsea kununua wachezaji kwa bei aghali kupindukia. Miezi miwili iliyopita Man City walimnunua mshambuliaji chipukizi wa Liverpool, Raheem Sterling kwa paundi 49. Kiasi hiki ni kikubwa kuzidi vyote vya wachezaji wa Kiingereza.
Aliyewahi kuuzwa kwa bei ghali kihivyo, alikuwa mlinzi maarufu aliyeshastaafu Manchester United, Rio Ferdinand, aliyelipiwa paundi milioni 30 mwaka 2002. Wakati huo zilionekana fedha nyingi sana.
Mshahara wa Raheem Sterling ni paundi 180,000 kwa juma. Alianza kwa kulipwa paundi 400 tu akiwa timu ndogo ya Queen Park Rangers
Kelele zinaendelea kupigwa kuhusu matumizi ya fedha nyingi kuuza na kununua wachezaji, kuhusu vilabu vinavyofukuza makocha kila wanaposhindwa mechi chache; kuhusu wachezaji kupanda viburi wanapoanza kuchoshwa na vilabu vyao huku washabiki wakiendelea kuwapenda na kuwa tayari kufa nao kisabuni.